Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu na Siku ya 57 ya Kuombea Amani, 2024
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Utangulizi: Leo ikiwa ni tarehe Mosi, Januari 2024 Mama Kanisa anatualika wote tumtafakari Mama yetu mpendwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Malkia wa Amani. Hili ni kati ya mafundisho makuu matano ya Kanisa Katoliki kuhusu Bikira Maria, Mengine ni Mkingiwa dhambi ya asili, Bikira daima, Kupalizwa Mbinguni na Mwombezi wetu. Bikira Maria amepata tuzo la kuitwa mama wa Mungu kwa kuwa mfuasi kamili wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ikiwa leo pia ni siku ya kuombea amani duniani kote tunahimizwa kumtumia mama huyu kama kiunganishi katika juhudi zetu za kuomba na kutafuta amani. Tena kama tujuavyo tarehe mosi mwezi wa kwanza ni sikukuu ya mwaka mpya ambapo tunafanya majumuisho ya yote tuliyofanya mwaka uliyopita na tunajiandaa vipi kuukabili mwaka huu mpya. Mama kanisa ameweka siku hii kuwa ni ya kuombea amani duniani kama tujuayo tunu hii ya amani kila mtu anahitaji na ni haki msingi kutoka kwa Mungu kwa Maombezi ya Mama wa Mungu dunia inapata amani na usalama. Siku ya 57 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2024 inanogeshwa na kauli mbiu: “Teknolojia ya Akili Bandia na Amani”: Artificial Intelligence and Peace: Au “Akili Mnemba na Amani.” Baba Mtakatifu katika ujumbe huu anagusia kuhusu: Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia kuelekea ujenzi wa amani; Wakati ujao wa akili mnemba: kati ya ahadi na hatari; Teknolojia ya siku zijazo: mashine ambazo "hujifunza" peke yake; Hisia ya kikomo katika dhana ya kiteknolojia; Masuala motomoto kwa maadili; Je, tugeuze panga ziwe majembe? Changamoto za kielimu na hatimaye ni changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa.
UFAFANUZI: Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu ni sherehe muhimu kwetu sisi wakristo wa leo kwani inatukumbusha nafasi ya pekee aliyonayo Mama yetu Mpendwa Bikira Maria. Kwanini basi Maria anaitwa mama wa Mungu? Swala hili limekuwa ni swala tete sana na lisiloeleweka vizuri tangu karne ya pili. Lakini kwa juhudi za mababa wa kanisa wakaweza kulieleza na kuliweka wazi maana kamili ya Bikira Maria kuitwa mama wa Mungu. Lakini ingawa mababa wa kanisa walishaweka wazi swala hili katika Mtaguso wa Efeso wa mwaka 431, na likathibitishwa tena katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican hasa katika hati ya Fumbo la Kanisa (Lumen gentium.n.53) inayosema “Bikira Maria, aliyepokea kwa ujumbe wa Malaika Neno wa Mungu moyoni mwake na mwilini mwake na kuuletea ulimwengu Uzima, anatambuliwa na kuheshimiwa kuwa kweli MAMA WA MUNGU na wa MKOMBOZI.” Pamoja na hayo bado swala hili bado ni gumu kwa baadhi ya watu kulielewa vizuri mpaka leo hii fundisho hili la mama kanisa mtakatifu Kwa kuwa wakatoliki wote twaamini na katika sala ya KANUNI YA IMANI (Nasadiki) twakiri wote kuwa Yesu ni mwana wa Mungu na ni Mungu kweli, twasali hivi “Nasadiki kwa Bwana Mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba, tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli.” Kwahiyo twakiri na kuamini kuwa Yesu ni mwana wa Mungu aliyezaliwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa Mwanadamu. Ikiwa Bikira Maria ni mama wa Mwana wa Mungu, kwahiyo ni halali kwake kuitwa Mama wa Mungu. Kweli mbili kwa Mama Maria kuitwa Mama wa Mungu.
Bikira Maria ni Mama wa Mungu. Ukweli huu wa imani yetu ni muhimu kwetu kwani inatukumbusha nafasi ya pekee aliyonayo Mama yetu Mpendwa Bikira Maria katika Historia ya Ukombozi. Kwanini basi Maria anaitwa Mama wa Mungu?Tujaribu kupata maelezo machache ili kulielewa fumbo hilo na si kulifumbua. Hata hivyo, kamwe hatusemi kuwa Mama Maria ni Mungu bali ni binadamu aliyepewa neema ya pekee na Mungu. (lk 1:28). Bikira Maria ni Mama kweli wa Yesu, kwakuwa hali ya ubinadamu wa Yesu ilichangiwa na Mama Bikira Maria kwa ukamilifu wote, kama ilivyo kwa mama zetu walivyochangia kwa kikamilifu katika uundwaji wetu na kuitwa binadamu tuliokamilika. Kwenye somo la Pili “Mungu alimtuma Mwanaye ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao walikuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana (Gal 4: 4 – 5)”. Kwahiyo Yesu ingawa ni Mungu lakini alizaliwa kwa kufuata utaratibu wa kibinadamu kama ilivyokawaida kwa kukaaa tumboni mwa Maria kwa miezi tisa na baadaye kuzaliwa, kuwa mtoto, na baadaye mtu mzima. Ingawa Mungu alikuwa na uwezo wa kufanya vinginevyo lakini hakutaka kwa sababu alitaka atukomboe sisi tulio chini ya sheria kwa kumtumia mwanaye ambaye yupo juu ya sheria, bali alijishishusha na kuwa chini ya sheria ili atukomboe sisi. Basi huu ndiyo ukweliwa Bikira Maria kuitwa mama wa Mungu, sifa hii ambayo mama yetu mpendwa amepewa ni halali kabisa na wala haitakiwi kutiliwa mashaka na Mkisto yeyote ambaye anaamini na kusadiki kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu na ni Mungu kweli.
Yesu aliye Mungu kweli na mtu kweli, Nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu, alizaliwa (kwa namna ya kibinadamu) na Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwa namna hii, Mungu aliye Mwenyezi, Mkuu kuliko vyote, akafanya makao yake katika tumbo la Mama Maria, akazaliwa kama mimi na wewe. Ndio maana ya maneno haya “Neno wa Mungu akatwaa Mwili na akakaa kwetu” (cf Sala ya Malaika wa Bwana, Yohane 1:14). Kwa hivyo, Mama Maria ni Mama wa Mungu kwasababu yeye ni Mama wa Kristo ambaye ni Mungu kweli na mtu kweli. Mama Maria ni mkristo wa kwanza kwa maana kwamba alikubali kwa hiari yake kumchukua tumboni mwake mtoto Yesu. Hivyo, tuamini fundisho hili na tumwombe Mama Maria ili kwa maombezi yake, sisi sote tujaliwe moyo wa utii kwa mapenzi ya Mungu. Kila mmoja wetu aimarike katika imani kuwa ameitwa na Mungu na hivi ajibidishe katika kufanya yale anayoagizwa na Mungu kupitia Kanisa lake. Mama Bikira Maria aliyakubali mapenzi ya Mungu katika maisha yake kwa imani,matumaini,sadaka na mapendo makubwa.Na hivyo Mungu alimtuza zawadi ya kuwa mama wa Mungu na hata baadaye kupalizwa mbinguni mwili na roho.Tukakubali mapenzi ya Mungu katika maisha yetu ili tukaishi kwa amani ambayo ni lulu adimu na ilisitirika zama za leo na hivyo kwa maombezi ya Bikira Maria mama wa Mungu tuwe na iwepo amani ya kudumu nay a kweli kati yetu na Mungu,ndani ya mioyo yetu na amani na wenzetu.