Sherehe ya Kesha la Noeli Mwaka B wa Kanisa: Yesu Ni Mwanga wa Mataifa!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu katika Liturujia ya Misa ya mkesha wa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni Sherehe ya umwilisho, Neno wa Mungu kutwaa mwili, Emmanueli, Mungu pamoja nasi. Kristo Yesu anajifunua kuwa ndiye mwanga wa Mataifa aliyekuja kuiangazia Yerusalemu, kuiamsha na kuirejeshea utukufu wake. Yeye ndiye Mwanga ambao Mataifa watatembea katika njia zake. Huu ndio ujumbe wa unabii wa Nabii Isaya tunaousikia katika somo la kwanza, ujumbe unaokamilika kwa kuzaliwa kwake Kristo Yesu. Na wimbo wa mwanzo unatufungulia maadhimisho haya ukisema; “Bwana aliniambia, ndiwe mwanangu, mimi leo nimekuzaa” (Zab.2:7). Kuzaliwa kwake Yesu Kristo, kunatuwezesha kumfahamu Mungu kuwa ni Baba yetu na kuuonja upendo wake kwetu sisi wanadamu “hata akamtoa mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16). Ndiyo maana katika usiku mtakatifu wa kuzaliwa kwake Yesu Kristo, tunaalikwa kufurahi maana Nuru imetushukia duniani na giza la dhambi na uvuli wa mauti kuondolewa. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu, uliyefanya usiku huu mtakatifu kung’ara kwa Nuru ya mwanga wa kweli, tunakuomba sisi tuliofahamu mafumbo ya Mwanga huo hapa duniani, utuwezeshe pia kuzipata furaha zake mbinguni.” Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa 9:2-7). Somo hili ni wimbo wa Kimasiha unaotoa wasifu wa Emmanueli - Mungu pamoja nasi, mfalme wa amani. Itakumbukwa kuwa Jeshi la Assyria lilipowashambulia waisraeli, liliteketeza makazi yao, wakawaua walioleta upinzani, wengine wakawachukua mateka, wengine wakaachwa wakiwa na majeraha yaliyowafanya wawe walemavu kama vile vipofu, viwete na viziwi. Waliobaki salama ni wale waliobahatika kujificha ndani ya mahandaki. Hali hii ni kama “uvuli wa mauti.”
Ndiyo maana Nabii Isaya anapowatangazia amani na kuwapa matumaini mapya anasema; “wale waliokwenda katika giza wataona Nuru na wale wanaokaa katika uvuli wa mauti Nuru itawaangaza”. Nuru hii ni Masiha, mkombozi Bwana wetu Yesu Kristo aliyezaliwa kama kiitikio cha wimbo wa katikati kinavyoimba na kushangia kikisema; “Leo amezaliwa kwa ajili yetu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana” (Lk. 2:11). Mzaburi katika mashairi anaimba hivi; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana nchi yote, mwimbieni Bwana, libarikini jina lake. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku, wahubiri mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, bahari na ivume na vyote vijazavyo. Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha mbele za Bwana, kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, na mataifa kwa uaminifu wake” (Zab. 96: 1-3, 11-13). Furaha hii inaelezwa kwa lugha mbili za ishara; furaha ya mkulima wakati wa mavuno ya kwanza, na furaha ya wanajeshi wanapogawana nyara baada ya kushinda vita. Kuna mambo matatu ambayo kwayo dunia inapaswa kufurahi. Kwanza ni kukombolewa kutoka kwenye manyanyaso na mateso ya utumwa. Ndiyo maana ishara na alama za utumwani kama vile nira ya mzigo mzito, gongo mabegani na fimbo, vyote zitavunjwa na kuondolewa. Pili ni silaha zote za kivita kuteketezwa. Na tatu ni zawadi ya mtoto kutoka kwa Mungu, ndiye Imanueli, Mungu pamoja nasi, mfalme wa amani. Mtoto huyo ni wa kiume, ana uweza wa kifalme mabegani mwake. Jina lake ni mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Alama na viashiria vya ujio wake ni uhuru, upendo, haki na amani. Yesu Kristo ndiye Nuru inayoangaza usiku wa Krismasi ili watu wasitembee tena gizani; maana Yesu mwenyewe anasema; “Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye mimi hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima wa milele” (Yn.8:12).
Somo la Pili ni la Waraka Mtume Paulo kwa kwa Tito (Tit 2:11-14). Somo hili ni sehemu ya Katekesi ilivyotolewa kwa waamini wa Kanisa la mwanzo. Nalo linaeleza kuwa Yesu Kristo ni ufunuo wa neema za ukombozi ambazo Mungu anatujalia kwanza kwa kuzaliwa kwake. Utimilifu wa neema hizi ni kifo na ufufuko wake kwa wafu, kilele cha fumbo la ukombozi wetu. Na ili tuweze kuwa watakatifu, tunapaswa kuukataa ubaya na tamaa za kidunia hii na kuifumbata neema ya Mungu iliyofunuliwa kwetu katika fumbo la umwilisho la Mungu kujifanya mtu na kukaa nasi. “Maana neema ya Mungu mwokozi wetu inayowaokoa wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na uchaji (utauwa) katika ulimwengu huu wa sasa” (Tito 2:11, 12). Tukifanya hivi tutajaliwa utakatifu katika maisha ya sasa na uzima wa milele mbinguni. Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 2:1-14). Sehemu hii ya Injili ni simulizi la kuzaliwa kwake Yesu Kristo. Nalo linatoa taarifa muhimu za kihistoria na kijiografia kutoa ushahidi kuwa habari za kuzaliwa Yesu ni za kweli. Yesu amezaliwa wakati wa utawala wa kirumi chini ya Kaisari Augusto. Wakati huo ilifanyika sensa ya kwanza, Kirenio alipokuwa liwali wa Shamu. Yesu amezaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi Yosefu alipoenda kuhesabiwa. Mahali na hali alikozaliwa Yesu panatajwa kuwa ni Bethlehemu katika mji wa Daudi, katika zizi la kulishia wanyama. Habari za kuzaliwa kwake wanapewa kwanza wachungaji wakiambiwa; “Leo katika mji wa Daudi, amezaliwa kwa ajili yenu, Mwokozi ndiye Kristo Bwana”. Nao wachungaji walikuwa ni watu waliodharauliwa: hawakuruhusiwa kusali Hekaluni, wala kutoa ushahidi mahakamani, walionekana ni wadhambi na wadanganyifu. Ishara wanazopewa ni za kawaida: Mtoto mchanga, aliyevikwa nguo za kitoto, akiwa amelazwa katika hori la kulishia wanyama.
Mazingira duni aliyozaliwa mtoto Yesu, yanaashiria hali yetu nyonge ya kibinadamu chini ya himaya ya ibilisi. Yeye anaichukua hali hii duni ili aturudishie hadhi yetu tuliyoipoteza; hali ya kimungu. Mazingira haya yanaficha umungu wake, uchanga na nguo za kitoto vyaficha umungu wake, ubinadamu waficha umungu wake, mateso na kifo cha aibu vyaficha umungu wake. Mtakatifu Thomaso wa Aquino aliimba; waficha umungu Msalabani na ubinadamu Altareni na fahamu yangu yadanganya, yanapokuona na kugusa. Utabiri wa Nabii Isaya unaanza kudhihirika kuwa; Kristo amekuja kwa ajili ya wanyonge, watu wanaoteswa na kukandamizwa na dhambi, Yeye amekuja kuwarudishia hadhi na utu wao kwa kuwajalia uhai na uzima mpya wa kimungu. Nasi ili tuweze kumpokea, yatupaswa kwanza tutambue unyonge wetu, udhaifu wetu, tujishushe na kujinyenyekeza. Kumbe, kuzaliwa kwake Kristo ni mwaliko kwetu wa kuyamulika na kuyaweka hadharani yote yanayodhalilisha hadhi na utu wa mwanadamu – manyanyaso ya kimwili, kiakili, kiroho, na kisaikolojia. Ni mwaliko wa kupambana na matendo yote yanayovunja heshima ya mwanadamu; utumwa mamboleo, biashara haramu ya binadamu, hali nyonge za kazi, kuwatumikisha wengine kama vyombo. Haya yote tunawajibika kuyatokomeza ili tuweze kufurahia kuzaliwa kwa mtoto Yesu, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Basi tujiombee sisi wenyewe, tuziombee tawala za duniani ziondoe sheria zinazotetea mambo ya giza na ya uovu. Tuzingatie maadili ya utu na kutetea haki na amani. Tushikilie mafundisho ya Kanisa yatupatie mwelekeo wa maisha, “tutupilie mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga. Na tuishi kwa adabu kama inavyostahili wakati wa mchana, na wala sio kwa ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugonvi na wivu. Bwana wetu Yesu Kristo awe vazi letu” (Rum.13:12-13). Kwa namna hii Noeli itakuwa na maana na tutakuwa na haki ya kuimba; “Leo amezaliwa kwa ajili yetu Mwokozi, ndiye Kristo Bwana” na sala baada ya komunyo anayotuombea mama Kanisa akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, sisi tunafurahi kufanya sikukuu ya kuzaliwa kwake Mkombozi wetu. Tunakuomba utujalie kuishi vema, tupate kustahili kufika kwake”, itafika mbele za Mungu na kupata kibali machoni pake. Nawatakieni heri na baraka tele za kuzaliwa mtoto Yesu, Emanueli, Mungu pamoja nasi. Tumsifu Yesu Kristo!