Sherehe ya Noeli Mwaka B wa Kanisa: Misa ya Alfajiri: Ukombozi Wetu Umetimia!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu katika liturujia ya Sherehe ya Noeli, Misa ya alfajiri. Kanisa linakumbuka na kuadhimisha katika Sherehe hii kuzaliwa kwake Yesu Kristo, Mwana wa Mungu na linatuongoza kwenye pango ili kutuonyesha Neno wa Mungu aliyetwaa mwili katika Bikira Maria. Kwani ni katika sura hii ya mtoto mchanga, Mungu alishuka toka mbinguni akaja duniani, akajifanya sawa nasi, akawa nasi, akakaa nasi ndiye Emanueli, Mungu pamoja nasi. Ndiyo maana katika liturujia ya kipindi hiki Kanisa halichoki kumshangilia Mtoto Yesu. Linafurahi na kutushirikisha sisi furaha yake kama mama mwenye heri aliyepata mtoto. Lakini furaha hii si furaha ya nje tu, yaani furaha ya kidunia, kwani ni Mungu mwenyewe anayetuzawadisha. Katika mtoto huyu hutimilika matumaini na tamaa zote za binadamu za kupata wokovu kama alivyoagua Nabii Isaya akisema: “watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza” (Isaya 9:2). Nia ya Kanisa katika kipindi hiki ni kutufunulia zaidi na zaidi ukuu wa mtoto huyu aliye Mwana wa Mungu Mwenyezi na kutushirikisha neema zake. Wimbo wa mwanzo umebeba kiini cha maadhimisho haya nao unasema; “Nuru imetuangazia leo, maana kwa ajili yetu amezaliwa Masiha; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu, Mfalme wa amani, Baba wa milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho” (Isa. 9, 2. 6; Lk. 1: 33). Na katika sala ya mwanzo mama Kanisa anatuombe akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, sisi tumemulikwa na mwanga mpya wa Neno wako aliyejifanya mwanadamu. Tunakuomba utujalie tuonyeshe kwa matendo yetu ile imani inayong’aa akilini mwetu.”
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 62:11-12). Somo hili ni fupi sana nalo limebeba hitimisho la sura ya 62 ya kitabu cha Nabii Isaya. Katika sura hii, Mungu anaialika Yerusalemu ifurahi kwa furaha kubwa. Mji wa Yerusalemu ulikuwa umejengwa juu ya kilima kilichoitwa Sayuni au Sioni. Hii ndiyo maana katika Maandiko Matakatifu mji huu unaitwa binti Sioni. Katika matukio mbalimbali manabii waliufananisha mji wa Yerusalemu na mwanamke au mama. Kumbe Maandiko Matakatifu yanaipoongelea Yerusalemu kwa namna hii, hayazungumzii mji wenyewe, bali watu walioishi ndani yake. Mungu anaialika Yerusalemu ifurahi kwa sababu mbili; Kwanza, Mwokozi wake anakaribia kufika kuja kuwaokoa na kuwaongoza watu wake nyumbani baada ya kukaa uhamishoni Babeli kwa miaka mingi (Is 62:11). Katika kuwaleta nyumbani, Mungu atawatakasa dhambi zao na kuwapa jina jipya; “watu waliookolewa”, “watu watakatifu”. Sababu ya pili ni kufurahia upendo wa pekee ambao Mungu atauonesha kwa mji wa Yerusalemu. Upendo huu ni kama wa Bwana arusi kwa bibi arusi (Is 62:5). Hivyo kama mwanamwali anavyofurahia upendo wa Bwana wake ndivyo Yerusalemu anavyopaswa kufurahi kwani Bwana atamlinda na hatari zote. Yerusalemu atapewa jina jipya. Itakubukwa kuwa alipokanyagwa na maadui zake kwa sababu ya dhambi zake, aliitwa “aliyeachwa”, kama mwanamke aliyeachwa na mume wake. Lakini kutoka sasa na kuendelea ataitwa “Yule ambaye mume wake anamtamani”, mpendwa wa Mungu.
Hii ndiyo lugha ya Maandiko Matakatifu inavyotumika kueleza upendo wa kina wa Mungu kwa watu wake. Ndiyo maana anaahidi ukombozi kwao wote wakaao katika utumwa wa dhambi na kuundwa kwa taifa jipya takatifu litakaloitwa “watu watakatifu” yaani waliokombolewa na Bwana. Ndio sisi tuliokombolewa kwa mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Na hii ndiyo sababu tunaalikwa kufurahi na kushangalia kama wimbo wa katikati unavyosema; “Mwangaza utatung’aria leo: kwa maana Mwana amezaliwa kwetu. Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, Visiwa vingi na vifurahi. Mbingu zimetangaza haki yake, na watu wote wameuona utukufu wake. Nuru imemzukia mwenye haki, na furaha wanyofu wa moyo. Enyi wenye haki mfurahieni Bwana, na kulishukuru jina lake takatifu (Zab. 97:1, 6, 11-12). Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Tito (Tit. 3:4-7). Tito alikuwa kijana ambaye Paulo alimteua kuongoza Kanisa katika kisiwa cha Krete. Katika somo hili Mtume Paulo anaeleza mabadiliko makubwa yaliyoletwa na ujio wa Kristo. Somo hili katika Misa ya Alfajiri linaanza na aya ya nne ya sura ya tatu. Lakini tukirudi nyuma kidogo katika aya ya tatu tunasoma hivi; “Kumbuka kuwa kuna wakati, sisi pia tulikuwa wajinga, wasio watii, tuliopotea na kutawaliwa na vionjo na aina zote za tamaa tulipoishi katika uovu na utashi potovu tukichukiana wenyewe” (Tit 3:3). Paulo kwa maneno haya makali anatueleza hali halisi ya kusikitisha ya mwanadamu kabla ya kuja Kristo ulimwenguni na hali yetu kabla hatujaipokea imani. Sote tulikuwa wajinga, wajinga wa upendo wa Mungu kwetu na wa njia ya kufika kwake. Tulipotea na kuwa mbali na Mungu sababu ya dhambi zetu. Hatukuwa watii kwa maana tuliishi kinyume na mapenzi ya Mungu. Tulikuwa watumwa wa shetani tuliofungwa na minyororo ya dhambi zetu. Tulichukiana kwa sababu ya ubinafsi, tuliwatumia jirani zetu kama vyombo kwa tamaa zetu.
Kwa ujio wake, Yesu amebadili hali hii yetu ya kusikitisha. Tumetakaswa dhambi zetu na kupewa maisha mapya, maisha ya roho na kuwa watoto wa Mungu. Tumekuwa warithi na kushiriki uzima wa kimungu na kujazwa furaha hapa duniani, furaha ambayo itakamilika tutakapofika mbinguni. Huu ni upendo mkubwa mno wa Mungu kwetu wanadamu. Kwa maana hakuna kitu chochote chema tulichofanya kustahilishwa haya yote, isipokuwa ni upendo na huruma yake tu. Ni upendo wa Mungu tu usio na kipimo uliomleta Yesu duniani. Nasi tunapaswa kutambua ukarimu na upendo wa Mungu uliofunuliwa kwetu kwa kuzaliwa mtoto Yesu, Yeye aliye “chapa halisi ya sura ya Mungu” (Ebr. 1:3) tukipendana sisi kwa sisi. Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 2:15-20). Sehemu hii ya Injili ni mwendelezo wa kupaswa habari kwa wachungaji kuhusu kuzaliwa mtoto Yesu, kama ilivyosimuliwa katika Misa ya mkesha. Katika simulizi hili tunaona kuwa hata wachungaji ambao hakuna chochote walichofanya walistahilishwa kuwa wa kwanza kupokea habari njema za kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Nao kwa unyenyekevu waliupokea ujumbe wa Mungu kwa njia ya Malaika kwa imani kubwa wakaenda kwa haraka Betlehemu kumwona mwokozi aliyezaliwa. Walimsifu Mungu kwa upendo wake wa kumtuma Mwokozi. Kwa upande mwingine tunakutana Bikira Maria, mama wa mkombozi ambaye aliyaweka mambo yote moyoni mwake kama hazina ya thamani kubwa na yakutafakari tena na tena upendo wa Mungu katika maisha yake na ya mwanadamu. Naye Yosefu mwenye heri akiwa ndiye baba mlishi akiwatunza.
Hili ndilo Fumbo la Umwilisho, Mungu kujichukua mwili wa kibinadamu na kuja kukaa nasi kama anavyokiri mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akituombea kwa kusema; “Ee Bwana, tunakuomba dhabihu zetu zifae kuadhimisha Fumbo la sikukuu ya leo ya kuzaliwa Bwana. Na tena kwa kuwa mtu huyu aliyezaliwa ni Mungu pia aliye mtukufu, hivyo dhabihu hizi za hapa duniani zituletee baraka za Mungu.” Baraka hizi zintuletea furaha kama antifoa ya wimbo wa Komunyo inavyoimba; “Furahi sana, ee binti Sayuni; piga kelele, ee binti Yersalemu; tazama, Mfalme wako anakuja; ni mtakatifu na mwokozi wa dunia” (Zek. 9:9). Na katika sala baada ya komunyo mama Kanisa anatuombe akisema; “Ee Bwana, sisi tunaoadhimisha kwa ibada na furaha kuzaliwa kwake Mwanao, tunakuomba utujalie tutambue kwa imani kubwa siri ya fumbo hili kulipenda kwa moyo wote.” Basi tuige mfano wa wachungaji, Bikira Maria na Yosefu tutambue upendo na huruma kuu ya Mungu kwetu vinavyojidhihirisha katika mtoto Yesu ili tujichotee neema za kutusaidia kuwa watakatifu. Niwatakieni heri na baraka tele za kuzaliwa mtoto Yesu, Emanueli Mungu pamoja nasi. Tumsifu Yesu Kristo!