Tafuta

Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Familia ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana.   (Vatican Media)

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu: Wito wa Familia

Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Ndugu yangu mpendwa, Mama Kanisa Mtakatifu ametupangia dominika ifuatayo adhimisho la Noeli, iwe ni kwa ajili ya kuadhimisha Utakatifu wa ndoa. Ni siku aambapo kwa namna ya pekee sana tunaienzi na kuiheshimu sana Familiya Takatifu ya Nazarethi, Familia ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia hii inapata heshima ya shule takatifu ambamo mtoto Yesu alikuzwa, akijifunza utii kwa wazazi wake, akijifunza sala, akijifunza kazi pamoja na fadhila nyingine nyingi. Ni kwa mfano wa familia hii takatifu ya Nazateti, Mama Kanisa Mtakatifu anataka kwa namna ya pekee kabisa kutufundisha sisi sote juu ya maan ana umuhimu wa familia katika Kanisa na Taifa kwa ujumla. Tunaelekezwa maneno yayo hayo na wazee wetu wa Kanisa katika Mtaguso wa II wa Vaticano. Familia ni shule; ni shule ya sala, shule ya upendo, shule ya utii, shule ya uaminifu, tena ni shule ya fadhila nyingi. Watu safi, wenye kukubalika, wenye kutimiza wajibu kiadilifu, hupatikana kutoka katika shule hii ya mwanzo kabisa yaani FAMILIA. Waalimu wakuu kabisa katika shule hii, ni WAZAZI. Pia majirani, na marafiki wa familia, jamii nzima yenye kuizunguka familia, nao pia ni waalimu. Kumbe, kila huyo ajihibiti hivi ili apate kuwa mwalimu mwema mwenye kuirithisha tunu bora kwa wanafunzi wake.

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu
Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu

UFAFANUZI: Si mara chache neno “familia” linatumika vibaya katika mazungumzo ya kila siku. Mathalani utasikia mtu akisema nina familia tano, au familia zangu mbili zinaumwa. Kumbe, anataka uelewe kuwa ana watoto watano, au watoto wake wawili wanaumwa. Mtoto au watoto si familia. Familia ni baba na mama na watoto katika ujumla wao na si kila mmoja peke yake. Wala hakuna familia halali yenye baba au mama wawili kwenye familia moja. Familia ya namna hii ni batili. Utaratibu wa kawaida wa kuwataja wana familia ni huu wa baba, mama na watoto, mama na baba; yaani Yesu, Maria na Yosefu. Kwa vile Yesu ni Mungu, lazima apewe nafasi ya kwanza. Maria au mama wa Mungu ni binadamu, lakini amepata upendeleo mkubwa wa kumzaa mwana wa Mungu, ndio maana anachukua nafasi ya pili. Yosefu ni baba mlishi wa Yesu. kwa hiyo anachukua hiyo nafasi ya tatu. Kwa makusudi Mungu aliamua mwanae azaliwe katika familia ya kibinadamu. Lengo halikuwa tu mwanae apate uhalali wa kijamii, yaani kuzaliwa katika ndoa si nje ya ndoa; lakini pia aweze kujifunza kimaisha na matendo halisi ya familia, toka hatua ya mwanzo mpaka mwisho. Wazazi wa Yesu Kristo, Maria na Baba mlishi Yosefu, walikuwa na fadhila zote za kila mzazi. Imani, unyenyekevu, uvumilivu, uchaji, uthabiti, upendo n.k. Yesu alishuhudia jinsi hao wazazi wake walivyokuwa wakiziishi, na hivyo kujifunza toka kwao.

Familia Takatifu ni Shule ya Utakatifu na Kanuni maadili
Familia Takatifu ni Shule ya Utakatifu na Kanuni maadili

 

Na tena Mama Kanisa anazidi kutufundisha kuwa, Familia ni Kanisa la Nyumbani. Kanisa ni Sakramenti ya jumla ya Ukombozi. Ni chombo cha ukombozi wa mwanadamu. Kwa mantiki hiyo hiyo, Familia ambayo ni Kanisa la nyumbani, lina wito wa kuwea chombo cha Ukombozi. Kwa maisha adilifu ndani ya familia, kila mwanafamilia akuzwe katika kumjua Mungu, kumpenda na kumtumikia. Pamoja nalo kuna wito pia wa kukuza roho ya sala katika familia. Familia ya Kikristo ili kweli iweze kuakisi yale ambayo yanatengemewa kutoka kwao, roho ya Sala ni vema sana ikuzwe. Leo hii katika familia zilizo nyingi, Sala zinapuuzwa. Tunamshukuru Mungu kwa kumfunulia mwanadamu kila siku leo tuna maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) tunaweza kuwasiliana kwa urahisi kama hii nayofanya sasa , kwa bahati mbaya sana nyakati zetu hizi ambapo tuna ongezeko la dini za TV, watu wanafikiri kwa kukaa mbele ya runinga na kutizama watu wanavyorukaruka na kusikiliza radio wakiimba mapambio eti yatosha hana haja ya kwenda kanisani, jumuiya ndogondogo, wala kushiriki sakramenti kama ekaristi takatifu kitubio, nk wakati uwezo na nafasi anayo kabisa. Hilo si sahihii ni vema kabisa kila mmoja akaujenga vizuri sana uhusiano wake na Mungu. Kukosa uhusiano na Mungu kunasababisha mwanadamu kuwa na dhamiri butu sana isiyo na gavana Katika Injili tunasoma “Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.” Katika familia, baba na mama ni viongozi wanaotakiwa kushikana mikono ili waishi vyema hapa duniani yaani kwa furaha, amani na upendo na mwisho wafikishane mbinguni kama mwili mmoja. Ndipo hapa tunaona baba ana wajibu mkubwa kwa mama na vivyo mama kwa baba lakini pia wazazi kwa mtoto.

Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii
Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii

Familia Takatifu ni mfano kwa familia zetu: Katika Oktava ya Noeli kanisa limetuwekea leo sikukuu ya familia takatifu. Kanisa linataka familia zote za kikristo ziige maisha ya familia takatifu, hata kama hazitafikia ukamilifu huo, lakini jitihada za makusudi zifanyike kufikia lengo hilo. Akina baba wa familia wanapata mfano wao katika Yosefu. Yeye kwa uvumilivu na unyenyekevu mkubwa alifanya kazi yake ya useremala. Kutokana na kazi hiyo aliweza kumudu mahitaji muhimu ya familia. Akina baba tuwe wachapa kazi ili tuweze kuzitunza familia zetu. Mahitaji ya msingi kama nyumba, chakula, mavazi, elimu, matibabu n.k. hayawezi kupatikana kama akina baba hatufanyi kazi. Na mbaya zaidi, ni wale akina baba wanaozikimbia familia zao. Akina baba tusikwepe majukumu yetu, tuwe wachapa kazi hodari, hakuna sababu ya kuwakimbia wake na watoto wetu. Kuitwa baba ni hadhi kubwa n acheo kikubwa ebu tuendelee kudhilisha hadhi hii ya kuwa baba bora na mwajibikaji Mama Bikira Maria ni kielelezo kizuri kwa akina mama wa ndoa. Jinsi mama Maria alivyokuwa mchapakazi, mwaminifu na mpendevu kwa familia yake, ndivyo inavyowapasa akina mama kuwa hivyo. Akina mama tusiwe watu wa kulalamika tu mara bwana haleti chumvi, wala nguo, wala sabuni, au mwingine kuishia kudai nguo mpya tu kila toleo linalotoka yeye anataka apate na bila hivyo basi ni ugomvi tu kila kukicha n.k. lakini tujiulize pia ni nini mchango wako katika kuiboresha familia yako? Katika ulimwengu huu wa usawa wa kijinsia tunasifu baadhi ya akina mama wamekuwa na mchango mkubwa kwa famila zao, jamii, zao na kwa kanisa. Ila bado pia wapo wenye dhana ya utegemezi wa kila kitu kutoka kwa akina baba ni vema kubadilika na kuiga mfano wa mama Maria na kuwa kweli walezi wa jamii, Kanisa na taifa.

Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo
Familia ni msingi bora wa malezi na makuzi ya Kikristo

Mfano mwingine ndugu zangu wa kujifunza kutoka kwa Mama Maria hasa kwenu nyinyi akina Mama ni huu wa kuiishi fadhila ile ya uvumilivu ambayo hata mume wake Yosefu aliishi. Ndugu zangu wapendwa katika Kristo, hasa kwenu nyinyi akina Mama, uvumilivu ndio fadhila ambayo ni msingi katika familia zetu hasa kwa siku hizi, utasikia kuwa mama fulani amemuacha mumewe eti kwa sababu tu baba ni mlevi, hana kazi, au mgonjwa, hii si sababu ya kukufanya umuache mumeo bali yakupasa uvumilie na kutafuta njia mbadala za kumbadilisha na hatimaye akabaki kwenye njia sahihi za misingi bora kwa malezi ya Kikristo na akina baba hvivyo hiyo wanadaiwa uumilivu Watoto tuna mfano toka kwa Yesu. Yatupasa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwatii wazazi wetu. Yesu licha ya kwamba alikuwa Mungu, lakini aliwatii Yosefu na Maria. Watoto, muwe faraja na kitulizo kwa wazazi wenu. Onesheni shukrani zenu kwao kwa kutimiza yale wanayowaelekeza yasiyopingana na mapenzi ya Mungu. Wakati mwingine hamwezi kujua kwa nini wanawakataza hili au lile. Muwatii tu kwani daima wanawatakia mema. Ni baadaye tu mkiwa watu wazima mtakuja kutambua mapendo hayo ya wazazi wenu. Kuweni baraka na neema kwa wazazi na familia zenu na epukeni kabisa kuwamajuto na adhabu kwa wazazi wenu, jamii, na kanisa Mungu mwema awajalie makuzi mema.

Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii
Familia ni kitovu cha maisha ya kijamii

Wazazi wawapatie malezi bora watoto wao ili wawajengee na kukuza utu wa kibinadamu,fadhila za upendo,nguvu na akili timamu na mwisho kukuza tamaduni zilizo bora. Pia, Familia takatifu ni jawabu la rasmi la matatizo mbalimbali katika ndoa kama mitala na uzinzi,kiburi na majivuno,mmomonyoko wa maadili katika familia,umaskini,ujinga,maradhi nk.Dawa madhubuti tunayofundishwa na familia takatifu ya Nazareth ni uchaji wa Mungu,kuishi mapendo ya kweli, uaminifu, unyenyekevu, msamaha ili kuepuka matatizo kabla hayajaja lakini zaidi kutibu pale yalipotokea. Tuige mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ili sisi akina baba, nanyi kina mama na ninyi watoto tujenge familia bora ambazo zitakuwa paradiso ndogo hapa duniani. Inawezekana kama tutatimiza wajibu wetu Tuanze sasa, mfano tunao na njia tunayo, kazi kwetu kuangalia na kuishi. Familia takatifu itusaidie kuilinda imani yetu na matendo mema katika familia tuishi kwa amani na furaha na mwisho tuufikie uzima wa milele. Lakini katika yote yatuypasa kukumbuka kwamba hakuna familia yeyote itakayo simama imara. Kufanikiwa na kudumu muda mrefu kama haina mapendo ya kweli na Mungu hayuko katikati. Mang’amuzi yanaonesha kuwa kusali pamoja, kula pamoja na kuishi pamoja ni kati ya mambo ya msingi kabisa kwa wanafamilia, iwapo wanapenda familia zao zidumu na kupata maendeleo ya kimwili na kiroho. Kupuuza moja kati ya mambo hayo matatu hupelekea familia kulegelega kabisa.

Familia Takatifu 2023
29 December 2023, 15:47