Tafakari Dominika 4 ya Kipindi cha Majilio Mwaka A: Fumbo la Umwilisho
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Nne ya Kipindi cha Majilio mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa. Hii ni dominika ya mwisho katika kipindi cha majilio. Kumbe kipindi cha majilio kiko ukingoni na Noeli imekaribia kama wimbo wa mwanzo umavyoashiria ukisema: “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi” (Isa. 45:8). Masomo ya dominika hii yanatukumbusha jinsi mpango wa ukombozi wa mwanadamu ulivyoanza na kutilika kwake. Itakumbukwa kuwa Mungu alitangaza mpango wa kumkomboa mwanadamu mara tu alipoanguka dhambini kwa kumlaani Ibilisi akisema; “Kwa sababu umefanya hivyo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote na hayawani wa mwituni. Kwa tumbo utakwenda na kula mavumbi siku zote za maisha yako”. Kisha akatangaza mpango wake wa kumkomboa mwanandamu kutoka katika hila za shetani akisema: “Nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke na kati ya uzao wako na uzao wake, huo utakuponda kichwa na wewe utamgonga kisigino” (Mwanzo 3:14-15). Uzao wa mwanamke unaotajwa hapa ndiye Bwana wetu Yesu Kristo Mkombozi wetu, ndiye Imanueli Mungu pamoja nasi, anayechukua mwili kwa Bikira Maria kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kuja kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Pili cha Samweli (2Sam. 7:1-5, 8-11, 16). Somo hili linatueleza mpango wa mfalme Daudi kutaka kumjengea Mungu nyumba ili aliweka Sanduku la Agano ndani mwake. Mungu kupita Nathani anakataa, na badala yake anaahidi Yeye mwenyewe kumjengea Daudi nyumba na kuwa ukoo wake utatawala milele yote. Ili kulielewa vizuri jambo hili yahitaji kufanya marejeo ya kihitoria. Historia inasimulia kuwa Mungu alimteua Daudi kuwa Mfalme mahali pa Saul na kumuahidi kuwa ufalme wake hautakuwa na mwisho. Katika utawala wake, mfalme Daudi aliifanya Yerusalemu kuwa makao yake makuu akaliweka huko Sanduku la Agano walilopewa wana wa Israeli na Mungu kama alama ya uwepo wake Mungu, alama ya mshikamano na utii wao kwake (2Sam 2:1-4; 5:5-10; 1Sam 16:1-13). Sanduku hili lilikaa katika hema, nyumba ya mapazi kama anavyosema Daudi mwenyewe; “Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia”. Hivyo Daudi akataka kujenga Hekalu ili kulihifadhi Sanduku la Agano.
Nabii Nathani aliyekuwa Mshauri wake, alimtia moyo afanye hivyo. Lakini Mungu alimtokea Nathani na kumtuma kwa Daudi amweleze mpango wake wa kuifanya nyumba na ufalme wake kuwa ni wa kudumu milele. Hapa kuna ujumbe mzito wa kiteolojia. Daudi kutaka kujenga hekalu na kuliweka Sanduku la Agano ni kama kutaka kummiliki Mungu na kumuweka katika sehemu moja ili kila anapohitaji msaada wake amwite. Mungu sio wa namna hiyo ndiyo maana Yeye mwenyewe anakataa na kusema kuwa Yeye atakayelijenga Hekalu na kuthibitisha uwepo wake wa kila mahali duniani kote. Ni katika muktadha huu tunapata zaburi ambayo ndiyo wimbo wa katikati inayosema; “Fadhili za Bwana nitaziimba milele; kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako. Maana nimesema, fadhili zitajengwa milele; katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako. Nimefanya agano na mteule wangu, nimemwapia Daudi, mtumishi wangu, wazao wako nitawafanya imara milele, nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu. Hata milele nitamwekea fadhili zangu, na agano langu litafanyika amini kwake (Zab. 89:1-4, 26, 28). Lakini hekalu aliloahidi Mungu sio hili la kujengwa na mikono ya mwanadamu, bali ni Kanisa fumbo la mwili wa Kristo nalo litadumu milele yote hata milango ya kuzimu halitaishinda. Ni utabiri wa Fumbo la Umwilisho, na kuzaliwa kwake Kristo Yesu, Mfalme pekee wa milele. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 16:25-27). Katika somo hili mtume Paulo anawaasa Warumi wamshukuru Mungu kwa kuwaletea Mkombozi, Bwana wetu Yesu Kristo. Ujumbe huu ni wetu kuwa tuwe watu wa shukrani kwa Mungu kwa kujifanya mtu kwa njia ya mwanae Bwana wetu Yesu Kristo mkombozi wetu. Ukweli huu wa mwana wa Mungu kuwa mtu ni fumbo. Akili zetu haziwezi kulielewa jinsi lilivyo. Imani tu yaelewa. Kristo kujimwilisha, kuwa mwana familia ya kibinadamu, mwana wa Adamu na mwana wa Mungu; mambo haya yote yanatuonjesha upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu, nasi hatuna budi kumshukuru.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 1:26-38). Sehemu hii ya Injili inasimulia kutimia kwa ahadi ya Mungu kwa Daudi katika Yesu Kristo. Ni simulizi la kupashwa habari Bikira Maria na Malaika Gabrieli. Nalo linaweka wazi kuwa Yesu ni mwana wa Mungu, atazaliwa na Bikira Maria na ni wa ukoo wa Daudi. Naye ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho. Ni katika unyenyekevu, upole, unyofu na utakatifu wa Bikira Maria, Yesu Kristo mwana wa Mungu alichukua mwili, akawa mwanadamu. Hivyo mwili wake Bikira Maria ukawa Hekalu takatifu na makao ya Mungu. Kumbe Bikira Maria akawa sanduku la Agano, makao mapya ya Mungu kati ya watu kwa kuupokea mpango wa Mungu kwa moyo wote, na kujitoa bila kujibakiza akisema: “Tazama mimi ni mtumishi wa Bwana nitendewe kadiri ulivyonena” (Lk 1:38). Namna hii utabiri wa Nabii Isaya kama tunavyouimba katika antifona ya wimbo wa komunyo tukisema; “Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli” (Isa. 7:14), ndivyo ulivyotimia. Kristo ndiye atakaye lijenga Hekalu la milele, ndilo Kanisa: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Mama Kanisa anatualika kufanya maandalizi ya kumpokea Mwokozi katika maisha yetu, katika jumuiya zetu, katika familia zetu na katika nafsi ya kila mmoja katika sherehe za Noeli, ili atujaze furaha na amani ya kweli. Tunaalikwa tukampokee kama Bikira Maria alivyompokea. Ndiyo maana katika sala ya kuombea dhabihu mama Kanisa anasali hivi; “Ee Bwana, Roho yule ambaye kwa uwezo wake Maria mwenye heri alipata mimba, azitakase dhabihu zetu tulizoweka juu ya altare yako”. Dhabihu hizi ndizo sadaka na majitoleo yetu, zawadi zetu kwa Mungu zinazotuwezesha kwa unyofu tutambue unyonge na utupu wetu, ili tujibidishe kupokea mpango wa Mungu katika maisha yetu kwa furaha na kwa moyo wote pasipo kujibakiza. Tukifanya hivyo tutaweza kusherehekea kwa shangwe, furaha, nderemo, na vifijo tukiwa na amani tele sherehe za kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo kama anavyotuombea mama Kanisa katika sala baada ya komunyo akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi tunavyoikaribia hiyo sikukuu takatifu, hivyo tuzidishe ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa kwake Mwanao.” Tumsifu Yesu Kristo.