Tafuta

Masomo ya sehemu hii ya pili ya kipindi cha majilio yanatuandaa kusherekea kwa furaha sikukuu ya Noeli, kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu. Masomo ya sehemu hii ya pili ya kipindi cha majilio yanatuandaa kusherekea kwa furaha sikukuu ya Noeli, kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu.  

Tafakari Dominika III ya Majilio Mwaka B wa Kanisa: Furaha!

Masomo ya sehemu hii ya pili ya kipindi cha majilio yanatuandaa kuzaliwa kwake Yesu Kristo katika maisha yetu. Papa Francisko anasema furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya tatu ya majilio mwaka B kiliturujia katika Kanisa. Tupo katika sehemu ya pili ya kipindi cha majilio. Masomo ya sehemu ya kwanza yalituongoza kujiandaa kwa ujio wa Kristo wakati wa hukumu ya mwisho ya wazima na wafu Kristo atakapokuja kama mfalme kutawala na kama hakimu mwenye haki anayemhukumu kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Naye atakuja siku tusiyoijua kwa kumtuma mjumbe wake ndugu yetu kifo kuja kutuita, kila mmoja zamu yake ikifika. Masomo ya sehemu hii ya pili ya kipindi cha majilio yanatuandaa kusherekea kwa furaha sikukuu ya Noeli, kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo katika maisha yetu. Papa Francisko anasema furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka.

Furaha ya Injili inakolezwa kwa waamini kukutana na Kristo Yesu; katika Neno.
Furaha ya Injili inakolezwa kwa waamini kukutana na Kristo Yesu; katika Neno.

Ndiyo maana katika sala ya mwanzo Mama Kanisa anatuombea akisema; “Ee Mungu, unatuona sisi taifa lako tukingojea kwa imani sikukuu ya kuzaliwa kwake Bwana. Tunakuomba utujalie kuifikia hiyo sherehe kubwa ya wokovu wetu, na kuiadhimisha daima kwa ibada kuu na furaha”. Nao wimbo wa mwanzo unatualika tufurahi ukisema; “Furahini katika Bwana siku zote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu” (Flp. 4:4-5). Mwaliko huu wa furaha unaipa domenika hii jina la “Gaudete” kwa kilatini ikimaanisha dominika ya furaha. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 61:1-2, 10-11). Somo hili ni utabiri wa habari njema na ya matumaini ya ujio wa Mkombozi mpakwa mafuta wa Bwana nalo linasema hivi: “Roho ya Bwana Mungu I juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu” (Isa. 61:1-2). Ujumbe huu wa furaha, ni kama tangazo la mwaka wa jubilei, mwaka wa ukombozi na neema. Kila msimu wa Mmajilio ni wakati wa ukombozi, utakaso na wongofu unaofumbatwa katika kulisikiliza neno la Mungu, ndilo neno la amani, neno la msamaha na neno la furaha. Nabii Isaya anaielezea ukubwa wa furahi akisema; “Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu” (Isa. 61:10-11).

Furaha ya waamini kukutana na Kristo katika Sakramenti zake
Furaha ya waamini kukutana na Kristo katika Sakramenti zake

Na hii furaha sio kitu kingine isipokuwa kujisikia huru na kuishi katika uhuru wa watoto wa Mungu. Ni furaha ambayo Bikira Maria anaishangilia katika wimbo wa katikati akisema; “Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, na roho yangu imemfurahi Mungu Mwokozi wangu; kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa. Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi, kwa hao wanaomcha. Wenye njaa amewashibisha mema, na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; ili kukumbuka rehema zake (Lk. 1:46-50). Nacho kiitikio chake wimbo huu kinakazia kusema; “Nafsi yangu itashangilia katika Mungu mwokozi wangu” (Isa.  61:10). Somo la pili ni la Waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes. 5:16-24). Katika somo hili mtume Paulo anaelezea namna gani mtu anayengoja kuja kwake Kristo anapaswa kuwa na kuishi. Mtu huyu anafuraha daima, anaomba bila kukoma, anashukuru kwa yote na ana mwenendo mwema. Ndiyo maana anasisitiza akisema: “Furahini siku zote, tena nasema furahi; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”. Il furaha hii iwe ya kweli mtume Paulo anatoa mwongozo na masharti akisema; “Msimzimishe Roho Mtakatifu; msitweze unabii, lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna”. Tukiyazingatia haya mambo Paulo anasema; “Mungu wa amani mwenyewe atawatakasa kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu ili mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo”. Hivi ndivyo tunavyopaswa kuwa na kuishi tunapongojea kwa matumaini kuzaliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo.

Furaha ya waamini ni kukutana na Kristo Yesu katika Kanisa lake
Furaha ya waamini ni kukutana na Kristo Yesu katika Kanisa lake

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 1:6-8, 19-28).  Sehemu hii ya Injili inaonesha furaha ya Yohane Mbatizaji katika kutimiza mapenzi ya Mungu kwa kutangaza kuja kwake Masiya, Mwana wa Mungu, mwanga wa kweli wa ulimwengu. Yeye alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie nuru inayowaangazia watu wote walio katika giza la dhambi na mauti, ili wapate kuuona utukufu wa Mungu. Ni katika kuipokea Nuru hii ambaye ndiye Bwana wetu Yesu Kristo, ndipo tunapokuwa na furaha ndani mwetu. Uaminifu wa Yohane Mbatizaji katika kutimiza mapenzi ya Mungu uliwavutia watu kutoka pande zote wakaja kubatizwa mtoni Yordani. Sehemu hii ya Injili inasema kuwa Wayahudi waliposikia habari hizi waliwatuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Yeye ni nani? Anasema nini juu yake? Na kwanini anabatiza? Yohane alikiri, wala hakukana, Yeye si Kristo, wala si Eliya, wala si nabii yule waliomsubiri bali ni “sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana yanyosheni mapito yake” ili nuru ya kweli ipate kuingia ndani mwao na kuwaangazia. Nuru hii ni yule Ajaye nyuma yake, ambaye yeye hastahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Maneno haya ya Yohane Mbatizaji kuwa yeye hastahili kulegeza gidamu ya kiatu chake ni mzito sana na yana maana kubwa mno. Tukisoma kitabu cha Ruthu 4:1-11 tunapata maana ya kulegeza gidamu ya kiatu. Ilikuwa hivi; mwanamke aliyefiwa na mume wake akabaki mjane, kaka ya mume wake au ndugu wa karibu alipaswa kumchukua yeye pamoja na mali zake ili amtunze. Kama akimkataa alipaswa kufungua gidamu ya viatu vyake na kumkabidhi ndugu anayefuata kama ushahidi wa kudhibitisha kuwa ameikataa haki na hadhi ya kupokea huo urithi.

Dominika ya furaha kwani Kristo Yesu anakaribia kuzaliwa
Dominika ya furaha kwani Kristo Yesu anakaribia kuzaliwa

Katika historia ya wokovu uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu unaelezwa kama uhusiano wa mume na mke uliopoteza uzuri wake sababu ya dhambi. Kristo anapokuja kurejesha uhusiano huu ni kama kumuoa mwanamke mjane aliyeachwa na mume wake. Yohane Mbatizaji kusema kuwa yeye hastahili kufungua gidamu ya viatu vyake ni kukiri kuwa mwenye uwezo wa kurudisha uhusiano kati ya Mungu na mwanadamu ni Masiha, Kristo Yesu peke yake, ndiye mpakwa mafutwa wa Bwana. Yeye Yohane Mbatizaji anafurahia kuwa sauti tu ya kumshuhudia Kristo aliye nuru ya kweli, furaha ya kweli, amani ya kweli. Kumbe furaha ya kweli ya Mkristo imo katika kuinua sauti yake ili kumtangaza na kumleta Kristo kwa wengine. Hii ni kumpa Mungu nafasi ya kwanza. Tukifanya hivyo Mungu pamoja nasi, Emanueli, atakuwa karibu nasi hivyo tutakuwa na sababu ya kufurahi. Lakini furaha yetu itadumu kama watu tunaoishi nao kama maskini, walemavu, wagonjwa na wenye shida mbalimbali watakuwa na furaha. Hii inatudai sisi kuwa sababu ya faraja na matumaini kwao. Ndivyo inavyosisitiza antifona ya wimbo wa komunio ikisema; “Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wetu atakuja na kutuokoa (Isa. 35:4). Tukifanya hivi Masiha atazaliwa ndani ya mioyo yetu na kukaa humo akitimiza mpango wa Mungu katika maisha yetu. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisema; “Ee Bwana, tunaomba tukutolee daima sadaka ya ibada yetu. Sadaka hii itimize mipango ya fumbo takatifu na kutuletea kweli wokovu wako”. Na katika sala baada ya komunyo anatuombea akisema; “Ee Bwana, utujalie huruma yako; utuondolee dhambi zetu; na neema zako hizi zituweke tayari kuadhimisha sikukuu zijazo kwa furaha.” Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari Majilio D3
14 December 2023, 07:48