Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Kristo Yesu ndiye chemchemi ya furaha ya waja wake. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Majilio: Kristo Yesu ndiye chemchemi ya furaha ya waja wake.   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika III ya Majilio: Kristo Yesu Ni Kiini cha Furaha Yetu!

Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Huu ni mwaliko wa kukutana na Yesu ili kuonja wokovu na furaha inayoletwa na Yesu, na hatimaye kuonja huruma na msamaha wa dhambi.

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama- Pozzuoli (Napoli), Italia

Dominika ya tatu ya Kipindi cha Majilio huitwa Dominika ya furaha “Domenica Gaudete.” Tunapaswa kufurahi kwa kuwa ujio wa Mwokozi wetu u karibu. Hata antifona ya kuingia inasema “Furahini katika Bwana sikuzote, tena nasema furahini. Bwana yu karibu.” Baba Mtakatifu Francisko anasema furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Kristo Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka. Huu ni mwaliko wa kukutana au walau kumkaribisha, ili kuonja wokovu na furaha inayoletwa na Kristo Yesu, na hatimaye kuonja huruma na msamaha wa dhambi Rej. Evangelii gaudium,1-4. Somo la kwanza (Isa. 61:1-2,10-11) Somo letu la kwanza linatupatia ujumbe kuwa “sisi sote tumewekwa wakfu (tumetengwa rasmi) kuwa watangazaji wa habari njema”. Somo linatueleza juu ya mjumbe wa Bwana aliyetiwa mafuta na anayetumwa na Mungu kuwapatia Waisraeli walioko uhamishoni Babeli habari njema ya matumaini: waliovunjika moyo watagangwa, mateka watapata uhuru (yaani watarejea Israeli), wafungwa watafunguliwa na wanyenyekevu watapokea habari njema. Huko Babeli Waisraeli walikuwa ni mateka, hawana uhuru, wamekata tamaa kutokana na ugumu wa maisha na hata kufikiri kuwa Mungu amewaacha. Mungu anamtuma nabii Isaya kuwapa matumaini mapya. Nabii huyu ni mletaji tu wa habari njema, anayetenda hayo yote ni Mungu. Sisi sote kwa Ubatizo na Kipaimara (na Sakramenti ya Daraja- kwa Mapadre) tumepakwa mafuta kuhubiri habari njema. Maisha na utume wetu unapaswa kuwa faraja na tiba ya kuwaganga watu waliovunjika mioyo kutokana na changamoto za maisha, familia, ndoa, imani au kudharauliwa, kutengwa na kutokupendwa. Je, sisi Mapadre, kwa mfano, ni faraja kwa waamini wetu waliovunjika mioyo? Tunapaswa kuwahubiria uhuru wa kweli uletwao na Kristo, ndugu zetu ambao wametekwa na dhambi, anasa, mali na vivutio vya ulimwengu. Wapo wenzetu ambao ni wafungwa, si wa gerezani bali wamefungwa akili zao ili washindwe kuelewa na kuishi kweli za kiimani na kimaadili, na pia wamefungwa macho ili wasione mahitaji ya watu wengine, hasa maskini na wasiojiweza. Wapo ambao wamefungwa na tamaduni na mila potofu. Hawa nao tumetumwa kuwatangazia habari njema ya kufunguliwa kwao.

Kristo Yesu ndiye chemchemi na kiini cha furaha yetu
Kristo Yesu ndiye chemchemi na kiini cha furaha yetu

Somo la pili (1 Thes. 5:16-24): Somo letu la pili linatutaka kuwa watu wenye furaha, wenye kusali bila kukoma na wenye kushukuru katika kila jambo. Tunapaswa kuwa na furaha daima kwa kuwa tumeunganika na Kristo ambaye ni chanzo cha furaha yetu nyakati za furaha na nyakati za uchungu. Furaha tunayoalikwa kuwa nayo ndiyo imefanya Jumapili ya 3 ya Majilio iitwe “Jumapili ya Furaha- Gaudete Sunday.” Furaha ya kweli inatoka kwa Kristo wala siyo kwenye wingi wa mali, ngono, pesa, vileo, madaraka au wingi wa akili za mtu. Tunapaswa kusali bila kukoma ili kuendelea kuunganika na Mungu na kupata neema za Roho Mtakatifu. Hatupaswi kusali tu nyakati za shida. Tusali bila kukoma hata kama tunaona hatujibiwi kwa wakati yale tunayoomba: tumuache Mungu ajibu kile anachotaka, kwa wakati anaotaka na kwa namna anayotaka. Tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kila jambo liwe baya au zuri kwani kwalo Mungu huwezesha roho zetu kupata utakaso na utakatifu. Mwisho, kama ambavyo Paulo anawaonya Wakristo wa Thessalonike kuwa (1) wasidharau unabii, lakini wayapime mambo yote (2) washike yaliyo mema na kujitenga na ubaya wa kila namna. Maonyo haya ni yetu pia. Kila siku tunapata unabii juu ya maisha yetu ya duniani na ya mbinguni kupitia kwa viongozi wetu wa dini. Jambo la busara ni kuomba Roho Mtakatifu atuwezeshe kutofautisha kati ya unabii wa kweli na wa uongo kwa maana kila kukicha wanazuka manabii wa uongo. Kadhalika, tunaonywa kujitenga na kila baya. Kwa bahati mbaya watu wa zama hizi tunapenda kujiambatanisha na ubaya/uovu badala ya kujitenga nao: midomo inapata ladha ikitamka uovu, macho nayo yanafurahi yakitazama puuzi za ulimwengu, miguu inafurahi ikikimbilia mabaya, mwili nao unasisimuka ukitenda mabaya. Tunahitaji utayari na neema ya Mungu kushinda uovu.

Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili
Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili

Somo la Injili (Yn. 1:6-8, 19-28): Somo letu la Injili linatupatia ujumbe kuwa “sisi sote tunapaswa kuwa mashuhuda wa Kristo na pia kumtumikia kwa unyenyekevu”. Sehemu ya kwanza ya Injili ya leo (Yn. 1:6-8) inatueleza kuwa Yohane [Mbatizaji] ametumwa kutoka kwa Mungu kwa lengo la kuishuhudia nuru. Nuru anayeshuhudiwa ni Yesu Kristo maana Yesu mwenyewe anasema “Mimi ni nuru ya ulimwengu” (Yohane 8:12; 9:5). Katika sehemu ya pili ya Injili ya leo (Yn. 1:19-28) Yohane Mbatizaji anakiri wazi kuwa yeye siyo Kristo/Masiha wala Eliya wala “nabii yule”. Wazo la Masiha lilitawala mawazo ya Wayahudi kwa kuwa waliahidiwa ujio wa Masiha. Kwa bahati mbaya mtazamo wao juu ya Masiha ulikuwa tofauti na Masiha halisi ambaye angekuja. Kwao Masiha ni mtu mashuhuri, mwenye nguvu na ushawishi na ambaye atawakomboa Waisraeli kutoka chini ya utawala wa Warumi. Walipomwona Yohane Mbatizaji walifikiri ndiyo Masiha maana alikuwa mashuhuri, mwenye ushawishi na hata kupata wafuasi wengi. Yohane anasema wazi kuwa yeye siyo Masiha. Walifikiri kuwa Yohane Mbatizaji ni Eliya kwa kuwa waliamini kuwa Eliya atatangulia kuja kwanza kabla ya ujio wa Masiha kwa lengo la kumwandalia Masiha njia (rejea Malaki 4:5). Pia walifikiri ni Eliya kwa sababu Yohane alivaa na kuishi kama alivyovaa na kuishi Eliya (rejea 2 Wafalme 1:8): Elia alivaa vazi la manyoya na mshipi wa ngozi kiunoni. Yohane naye alivaa mavazi kama hayo (rejea Mk. 1:6). Kadhalika walifikiri Yohane Mbatizaji ni “Nabii yule”- hapa Wayahudi walifikiri kuwa Yohane Mbatizaji ni nabii yule aliyeahidiwa na Musa katika Kumb. 18:15, 18. Katika nukuhu hiyo nabii anayeahidiwa siyo Yohane Mbatizaji bali ni Yesu Kristo. Pia Wayahudi waliamini kuwa zitakapofika nyakati za Masiha/Kristo kutakuwa na ubatizo (rejea Ezek. 36:25; Zek. 13:1) lakini waliamini kimakosa kuwa utatolewa na Masiha/Kristo peke yake. Hii ndiyo sababu wanauliza “Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?  Yohane anakiri kuwa yeye ni mjumbe tu (sauti iliayo nyikani) ambaye kazi yake ni (1) kumwandalia Masiha njia na (2) kuiandaa mioyo ya watu kwa ujio wa Masiha na (3) kuwajulisha watu kuwa Masiha tayari yupo miongoni mwa Wayahudi: “Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi”.

Injili itangazwe na kushuhudiwa kwa ari, unyenyekevu na moyo mkuu
Injili itangazwe na kushuhudiwa kwa ari, unyenyekevu na moyo mkuu

Injili ya leo inatufunza mambo matatu kupitia Yohane Mbatizaji: (1) sisi tuliobatizwa tunapaswa kumshuhudia Kristo Yesu ambaye ni nuru ya ulimwengu kwa maneno, mawazo na matendo yetu, kwa kuiishi Injili ambayo kiini chake ni upendo na msamaha, kwa kuwa na imani thabiti nyakati za furaha na huzuni, kwa kuifahamu imani yetu, kwa kuwafundisha wengine imani,  na zaidi ya yote kuwa tayari hata kumwaga damu yetu kwa ajili ya Kristo. Kwa bahati mbaya wengi wetu hatumshuhudii Kristo aliye nuru bali tunamshuhudia shetani kwa maneno, mawazo na matendo yetu kwa njia ya dhuluma, ulafi wa mali na madaraka, kupigia debe utamaduni wa ngono, kuhalalisha utoaji mimba na mapenzi ya jinsia moja, anasa, kushabikia ukabila na ukanda, kwa kukiuka misingi ya siasa safi, kwa kuwanyonya wanyonge na kuwadhalilisha watu kwa kuwazushia kashfa za uongo. (2) sisi sote tunapaswa kuwa wanyenyekevu/kujishusha katika utumishi wetu. Licha ya umaarufu, heshima na hadhi kubwa aliyokuwa nayo miongoni mwa Wayahudi, bado Yohane Mbatizaji anakiri wazi kuwa yeye si Kristo na ya kwamba “hastahili hata kuilegeza gidamu ya kiatu cha Kristo”- (gidamu ni kamba za kufungia viatu). Kazi ya kufunga au kufungua kamba za viatu iliyofanywa na mtumwa, tena asiye Myahudi kwa bwana wake. Yohane anakiri kuwa hastahili hata kuwa mtumwa wa Kristo kwa jinsi Kristo alivyo mkuu. Yohane Mbatizaji anajua wazi kuwa yeye si chochote mbele za Yesu. Yohane ni kinyume cha watu wengi. Leo hii watu wakipata umaarufu, vyeo, madaraka, hadhi ya juu au nguvu ya ushawishi wanajiona kama miungu, kama wapakwa mafuta (akina-kristo/masiha) na wakombozi ambao bila wao mambo hayaendi. Hata baadhi ya viongozi wa dini wameingia katika mtego huo. Watu wa namna hii wanataka kuabudiwa na kuogopwa. Wanataka jamii iwatazame wao badala ya kumtazama Kristo/Mungu ambaye ni mkubwa kuliko wao na ambaye wanapaswa kumtumikia. Yohane hakutaka watu wamtazame yeye bali wamtazame Kristo. Wote wenye madaraka tunapaswa kuwa na unyenyekevu katika kuwahudumia watu. Mt. Augustino anasema “Majivuno ndiyo yaliyowabadili malaika kuwa mashetani; unyenyekevu ndiyo unaowafanya watu kuwa kama malaika”. (3) Tunapaswa kutambua kuwa Kristo amesimama katikati yetu. Yohane Mbatizaji anatukumbusha kuwa tayari Kristo yupo katikati yetu katika maisha yetu ya kila siku ingawa wengi wetu bado hatujamjua. Yupo katikati yetu katika Sakramenti za Ekaristi na Kitubio, katika Neno lake, katika mikusanyiko ya sala, katika maisha ya familia na ndoa na katika changamoto zetu za maisha. Yupo pia katika majirani zetu, hasa wale wahitaji.  Je, tunaonja uwepo wa Kristo kati yetu? Tunapaswa kumwandalia Kristo njia kwa kufungua mioyo yetu ili atawale maisha yetu. Amani ya Bwana iwe nanyi.

15 December 2023, 11:32