Tafakari Dominika IV ya Kipindi Cha Majilio Mwaka B wa Kanisa: Bikira Maria
Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli (Napoli) Italia.
Tunapoelekea kuadhimisha Sherehe ya kuzaliwa Bwana Wetu Yesu Kristo, somo letu la Injili linatupatia simulizi juu ya namna Bikira Maria alivyopashwa habari ya kuzaliwa Bwana Wetu Yesu Kristo. Mafundisho yanayotokana na Injili yetu Lk 1: 26-38 yanaweza kuwekwa kwa namna mbili: Kwanza, mafundisho juu ya Bikira Maria, Yesu na Roho Mtakatifu; pili, mafundisho tunayopaswa kuiga/kuyaishi kutoka kwa Bikira Maria. Kutoka kwenye Injili yetu tunapata mafundisho makubwa ya imani yetu, hasa juu ya Bikira Maria. (1) Bikira Maria ni mkingiwa dhambi ya asili na dhambi nyingine zote. Malaika Gabrieli anamsalimu Mariamu akisema, “Salamu, uliyepewa neema.” Salamu hii inamstajabisha sana Mariamu. Ingawa somo letu limetuambia malaika alisema, “Salamu, uliyepewa neema” lakini tafsiri nzuri zaidi inapaswa kuwa, “Furahi, uliyejaa neema” (kwa Kigiriki ambayo ni lugha asilia ya Agano Jipya inasomeka, “Kaire, kecharitoméne”). Ninalenga kueleza maneno “uliyejaa neema” ambayo tunayatamka pia tunaposali sala ya Salamu Maria: “Salamu Maria, umejaa neema”. Kama ndoo imejaa mchanga, basi ukimimina chochote katika ndoo iliyojaa mchanga basi kinachomiminwa kitamwagika maana hakina nafasi ya kukaa kwa kuwa ndoo imejaa. Kadhalika, Bikira Maria “amejaa neema” na hivyo kama “amejaa neema” basi dhambi yoyote ile isingeweza kupata nafasi ndani yake maana mwili wake wote umejaa neema. Salamu ya malaika Gabrieli ni uthibitisho kuwa Bikira Maria hana dhambi ya aina yoyote ile. (2) Bikira Maria ni bikira daima (aliweka kiapo cha kuishi ubikira maisha yake yote). Bikira Maria anamuuliza Malaika Gabrieli, “Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Swali hili limekuja baada ya Bikira Maria kuambiwa kuwa atapata mimba na kuzaa mtoto.
Swali hili la Bikira Maria linatupa mwanga kuwa Mariamu alikuwa ameweka nadhiri ya kuishi ubikira maisha yake yote (yaani kutoingiliwa kimwili na mwanaume yoyote). Kama angekuwa na mpango wa kuingiliwa kimwili, kupata mimba na kisha kuzaa mtoto, basi asingeuliza swali hili maana kila mwanamke anajua namna mtoto anavyopatikana: anashiriki tendo la ndoa, anapata mimba na kisha kupata mtoto. Sasa kwa nini aliuliza swali hilo kama anafahamu jinsi mimba na mtoto vinavyopatikana? Hii ni kuonesha kuwa alikuwa ameweka nadhiri ya ubikira. Kwa maneno mengine ni kama Bikira Maria anauliza malaika Gabrieli: “Nitapataje mimba ilihali mimi nimedhamiria kuishi maisha ya kutoingiliwa kimwili? Na jibu la malaika lipo wazi: “hakuna lisilowezekana kwa Mungu.” Labda swali linalotusumbua wengi ni hili: Kama Bikira Maria alikuwa amekusudia kutoingiliwa kimwili maisha yake yote, iweje sasa aposwe kwa Yosefu? Aina hii ya ndoa ilikuwepo miongoni mwa Waisraeli: binti aliyeweka nadhiri ya kuishi ubikira maisha yake yote angeweza kutafutiwa mwanaume ambaye kisheria angetambulika kama mume wake lakini si kwa lengo la kuzaa naye (kumwingilia kimwili) bali kwa lengo la kumtunza na kumlinda ili aweze kutimiza vyema nadhiri yake. Hii ndiyo ndoa kati ya Yosefu na Maria. Tunaona jambo hili kama kitu kisichowezekana katika zama zetu maana siyo utamaduni wetu lakini kwa Wayahudi ni suala lililokubalika. Hivyo, hata Yosefu alijua wazi kuwa “hawezi kumwingilia kimwili Mariamu.”
Neno “kabla hawajakaribiana” kama lilivyotumika katika Mt. 1:18-24 halina maana “kabla hawajakutana kimwili” bali “kabla Yosefu na Mariamu hawajachukuana na kuanza kuishi ndani ya nyumba moja kwani baada ya tendo la kuposwa binti aliendelea kuishi kwao kwa mwaka mmoja au zaidi ili kumpa mume wake muda wa kujiandaa kwa arusi na kujipanga kuanza maisha ya ndoa ndani ya nyumba moja.” Ni ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja Mariamu na Yosefu wakiishi mahali tofauti tofauti ndipo Yosefu alipogundua kuwa Mariamu ana mimba. Swali la msingi ni hili: hivi mwanamke huyu aliyependelewa kwa kujazwa neema, binti aliyejitoa kwa Mungu na kufanywa kuwa Mama wa Mungu/Mwana wa Mungu anaweza kuwa sawa na mwanamke mwingine yoyote? La lasha! Anastahili kupendwa na kuheshimiwa sana. Tumpende bila aibu Mama yetu Bikira Maria. (3) Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Malaika anasema, “Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye Juu.” Ninataka kujenga hoja kwa kutumia maneno, “ataitwa Mwana wa Aliye Juu”. “Aliye Juu” ni nani? Ni Mungu. Kwa hiyo ni sawa na kusema, “ataitwa Mwana wa Mungu.” Tena Injili inazidi kusema: “kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.” Kwa hiyo ni dhahiri kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu. Hakuna ubishi. (4) Roho Mtakatifu ni nguvu tendaji katika fumbo la umwilisho. Bikira Maria hapati mimba kwa nguvu za kibinadamu bali ni kwa nguvu/uweza wa Roho Mtakatifu: “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli.
Baada ya kuona mafundisho ya imani yanayotoka kwenye Injili, ni vema sasa tuone mafundisho yanayoletwa kwetu sisi: (1) Tunapaswa kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha yetu. Bikira Maria anasema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” Kwa maneno haya Bikira Maria anaonesha utayari wake wa kuruhusu mpango/mapenzi ya Mungu yatendeke kupitia maisha yake. Maneno “na iwe kwangu kama ulivyosema” yanafupishwa kwa neno moja la Kilatini liitwalo “fiat”. Ni kwa “fiat” anayotamka Bikira Maria safari ya wokovu wa mwanadamu inaanza rasmi. “Fiat” (nitendewe kama ulivyonena) ya Bikira Maria ni uthibitisho wa imani yake thabiti kwa Mungu. Imani ni kuruhusu mapenzi au mpango wa Mungu utimizwe katika maisha yetu kwa njia mbalimbali: kwa njia ya mahangaiko yetu, kwa njia ya mateso tunayopitia, kwa njia ya utume wetu, kwa njia ya majitoleo yetu. Je, mimi na wewe tupo tayari kuruhusu mapenzi ya Mungu. Tujifunze kutoka kwa Bikira Maria: tunapoteseka, mwitikio wetu uwe “fiat” (nitendewe ulivyonena); tunaposumbuka kwa maumivu ya magonjwa daima tuseme “fiat” (nitendewe ulivyonena); unapoelemewa na changamoto za uzee, daima useme “fiat” (nitendewe ulivyonena); tunapokumbana na changamoto za maisha ya ndoa na utume, daima tuseme “fiat” (nitendewe ulivyonena).
Tusilalamike. Kama hatuelewi maana ya matukio tuyapatayo tusisite kuzungumza na Mungu kama Maria alivyokuwa anazungumza na Mungu kupitia malaika Gabrieli. (2) Tunapaswa kuzungumzana na Mungu (dialogue with God). Malaika Gabrieli anapotumwa kwa Bikira Maria anakwenda kama mjumbe wa Mungu, anamwakilisha Mungu. Kimsingi majibizano kati ya Bikira Maria na malaika Gabrieli ni mazungumzano kati ya Bikira Maria na Mungu (mazungumzano kati ya Mungu na mwanadamu). Bikira Maria haoni kigugumizi wala uwoga kuzungumzana na Mungu kwa njia ya malaika Gabrieli ili kupata ufafanuzi wa maswali yanayomtatiza na kumletea mawazo mengi. Na kwa kweli ni kwa njia ya mazungumzano haya Bikira Maria anaelewa kwa undani mpango wa Mungu juu yake na juu ya ulimwengu mzima. Bikira Maria anatufundisha kuwa ni lazima na sisi pia kufanya mazungumzano na Mungu. Mazungumzano kati ya Mungu na mwanadamu huitwa sala. Kumbe ni kwa njia ya sala tunapata muda wa kuzungumza na Mungu na kupata majibu ya maswali yanayotutatiza: maswali juu ya imani yetu, maswali juu ya matukio ya maisha tunayopitia, maswali juu ya changamoto zetu, maswali juu ya maana na umuhimu wa maisha, maswali juu ya mahusiano yetu na mengineyo. Bila sala hatuwezi kuelewa kwa undani mpango wa Mungu ndani yetu. (3) Tunapaswa kutambua unyonge na utumishi wetu mbele ya Mungu. Bikira Maria anatamka akisema, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana”. Katika tamko hili Bikira Maria anakiri mambo mawili: mosi, yeye ni mjakazi. Mjakazi ni mtumwa wa kike ambaye daima anapaswa kuwa mtii kwa bwana wake, ambaye kwa kweli mbele ya bwana wake ni kama hana faida, ni kama si kitu, ni wa hali ya chini, afanyaye kazi ambazo kwa macho ya wanadamu ni kazi duni. Naye Bikira Maria ni mjakazi mbele ya Mungu. Pili, Bikira Maria anakiri wazi kuwa yeye ni mjakazi wa Bwana- siyo mjakazi/mtumishi tu, bali ni mtumishi anayemtumikia Bwana. Kwa mambo haya mawili Bikira Maria anakiri udogo/unyonge wake mbele ya Mungu na anakiri pia utumishi wake kwa Bwana. Je, mimi na wewe tunatambua unyonge/udogo wetu mbele ya Mungu au tunajimwambafai? Je, mimi na wewe ni watumishi/wajakazi wa Bwana au ni watumishi/wajakazi wa malimwengu: tunatumikia pesa, tunatumikia matumbo yetu, tunatumikia waganga, tunatumikia anasa. Daima tunapaswa kuwa watumishi wa Bwana, na tufahamu kuwa “kumtumikia Bwana/Mungu ni yote katika yote.” Dominika njema ya Kipindi cha Majilio!