Tafakari Dominika ya Kwanza Majilio Mwaka B wa Kanisa: Kesheni na Salini
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Maingilio: Mwendo wa vipindi vya Liturujia ya Kanisa unafanana na ule wa maisha ya binadamu, ambayo yana maadhimisho ya pekee na majira ya kukua na kukomaa kwa utulivu. Vivyo hivyo mwaka wa Kanisa una sikukuu na siku za kawaida, vipindi vya pekee na ni Sehemu muhimu zaidi ya mwaka inategemea Pasaka na Noeli, sherehe kuu mbili zinazoendesha muda mtakatifu wote, ingawa zimo sikukuu nyingine pia. Katika mwaka wa liturujia ya Kanisa Katoliki, sherehe ya Noeli inaandaliwa na kipindi cha Majilio ambacho kina mambo mawili: kinakumbusha Mwana wa Mungu alivyotujilia mara ya kwanza, na papo hapo kinatuandaa kumpokea atakapo kuja siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu. Neno “Majilio” maana yake ni “ujio.” Katika Kalenda ya Kanisa Katoliki, ‘Majilio’ ni kipindi ambacho kimetengwa na Kanisa kwa ajili ya kuwaalika waamini wajiandae kumpokea Mungu anayekuja kwetu katika hali ya kibinadamu – Yesu Kristo, Mkombozi wa wanadamu wote. Kumbe wakati huu wa Majilio ni wakati ambao sote tunaalikwa kujitayarisha ili tumpokee Mkombozi katika hali njema. Kipindi hiki cha Majilio kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza huanza Dominika ya kwanza ya Majilio na huishia tarehe 16 Desemba. Katika sehemu hii Kanisa linawaalika wanawe wote kutafakari juu ya ujio wa pili wa Kristu katika utukufu wake. Sehemu ya pili huanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Hii ni sehemu ambapo masomo yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Kristo. Ni wakati wa matayarisho ya Sherehe ya kuzaliwa kwake Kristo yaani Sherehe ya Noeli.
UFAFANUZI: Tunapojiandaa kupokea zawadi ya “Uwepo” mtakatifu, zawadi ya Mungu Baba kwetu, ndiye Mwanaye mpendwa Yesu Kristo aliye Njia, Ukweli na Uzima, sote kabisa tunaalikwa tumgeukie Bwana, chemchemi ya wokovu wetu. Tumwabudu kwa uchaji tukisifu na kuomba baraka ya Mungu. Tunapaswa kutembea katika njia ya Bwana Yesu aliye Mwanga wa ulimwengu. Neno lake ni taa ya kutuongoza na ni njia ya miguu yetu, hakika “saa ya ukombozi i-karibu” Majilio yanatukumbusha kila mwaka matarajio ya kweli na hivyo yanaamsha hamu ya kuishi kwa bidii ya kiroho. Katika kipindi hicho tunaadhimisha tumaini la wana wa Israeli lililotimizwa Yesu alipokuja katika unyenyekevu wa umbile letu; pia tunangojea arudi kwa utukufu. Kama alivyotekeleza ahadi mara ya kwanza, atazitekeleza pia mara ya pili, ingawa kwake miaka elfu ni kama siku moja tu. Kati ya majilio hayo mawili, Bwana anatujilia mfululizo kifumbo katika Sakramenti (hasa ya Ekaristi Takatifu) na katika maisha ya kila siku kwa njia ya matukio na watu (hasa maskini). Basi tunapaswa kuwa tayari daima kumpokea ili siku ya mwisho tukamlaki, naye atukaribishe kwenye uzima wa milele. Pia tunapaswa kumuomba aje kutukomboa, yeye aliye tumaini letu. Katika safari ya Majilio manabii na watumishi watatu wa Mungu, wanatuongoza na kutusindikiza tukutane na Yesu: 1. Nabii Isaya, Nabii wa tumaini, mwenye kipaji cha pekee cha kuchochea matazamio ya binadamu na kumhakikishia atatimiziwa na Mwokozi yaani masiha. 2. Yohane Mbatizaji, mwenye kuhimiza toba kwa kuwa tunapaswa kupindua maisha yetu ili tukutane vema na Kristo. 3. Maria, Bikira aliyekuwa tayari kumpokea Masiha kwa upendo na kushirikiana naye katika kutimiza mpango wa wokovu.
Tukiwafuata hao watatu katika mwaka huu mpya wa liturujia yaani mwaka B tunaweza kujipatia maadili yale yanayotuandaa kumpokea Mwokozi anapotujilia, ambayo ndiyo matunda maalumu tunayotarajiwa kuyachuma wakati wa Majilio: 1. Kukesha katika imani, kusali na kutambua ishara za Bwana kutujilia katika nafasi yoyote ya maisha na mwishoni mwa nyakati. 2. Kuongoka kwa kufuata njia nyofu. 3. Kushuhudia furaha inayoletwa na Yesu kwa kuwa na upole na uvumilivu kwa wenzetu, kwa tumaini la kuwa bidii zetu zinawahisha ufalme wa Mungu wenye heri isiyo na mwisho. 4. Kutunza unyenyekevu kwa kufuata mifano ya maskini wa Injili ambao ndio waliompokea Mkombozi. Tusisahau kuwa na “majilio” yetu wenyewe, kuishi kwa matumaini ya mambo mema ya heri na baraka. Kijana uwe na matumaini, tegemea mambo mema, kwani asiyetegemea chochote amevunjika moyo, hana hamu ya kuishi tena. Wengine wana majilio ya ndoa, tuwashike mkono, wapo wenye majilio na matamanio ya kupata amani na mapatano na kuweka silaha chini na kupeana mikonno na kula meza moja, na kunyanyua glasi ya kidugu pamoja na kuvumilina, tuwatie moyo kwani daima wapanishi ni wana a Mungu, Wapo wenye majilio ya kurudi sehemu za ajira na biashara, zao tuwapee nafasi tena, Wapo wenye majilio ya kurudi kwenye masakramenti, tuwaombee. Wapo wenye majilio ya upadre, tuwaombee pia wapoo wenye majilio na shauku ya kuhuisha masha yao ya wakfu tuwakumbuke katika sala. Wapo wenye majilio ya elimu, ya kazi, ya biashara, ya kilimo nk. … wengine hawana majilio yoyote yaani hawana mpango wowote katika maisha yao, hawana sababu, bado ni wafungwa, tuwaombee.
Hata hivyo majilio ya kila mmoja yanapotimia hayamridhishi mtu moja kwa moja, ni Kristo tu ndiye anayetimiza hamu zetu zote kwa kututoa kwenye unyonge, kutukumbusha matarajio ya kweli na kuamsha hamu ya kuishi kwa bidii ya kiroho. Sisi ni watu wa Mungu naye ni Mungu wetu hivi ni lazima tujikabidhi kwake. Tuwe wasikivu kwake, tumsikie na kumsikiliza na halafu tuitende kazi yake. Maisha yetu ni maisha ambayo inabidi yatawaliwe na hali ya kukesha. Kukesha kwa ajili ya nini? Kukesha kwa ajili ya tukio kubwa – ujio wa Kristo. Ni lazima maisha yetu yawe maisha ya wakeshao kwa maana hatujui ni siku ipi Bwana atakayokuja. Tuwe tayari muda wote kwani hakuna mtu anayejua siku na saa ya kifo chake. Hali ya watu wanaokesha ni lazima ijitambulishe katika maisha ya kila siku. Kila mmoja wetu pale alipo ni lazima akeshe. Yesu anakuja katika mahali petu pa kazi, wakati wa kupumzika. Pia tunakutana na Yesu katika nafsi za wale tunaoishi nao, na katika matukio ya kila siku. Je, tupo tayari kumpokea wakati wowote ajapo?