2023.12.15 Tanzania:Misa kwa ajili ya nadhiri za kwanza,daima na Jubilei ya miaka 25 na 50 kwa masisita wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu,Bukoba,Tanzania. 2023.12.15 Tanzania:Misa kwa ajili ya nadhiri za kwanza,daima na Jubilei ya miaka 25 na 50 kwa masisita wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu,Bukoba,Tanzania. 

Tanzania,Ask.Kilaini kwa Watawa wa Mt.Theresia:Wamtegemee Mungu licha ya changamoto

Katika siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili,Masista 7 walifunga nadhiri za kwanza,8 nadhiri za daima,masista 4 Jubileiy a miaka 25,masista 11 Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya Utawa katika Shirika Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu,Nyaigando,Bukoba Tanzania.Askofu Kilaini aliwashauri kujitoa bila kujibakiza kumtumikia Mungu katika maisha yao.

Patrick Tibanga - Radio Mbiu-Bukoba na Angella Rwezaula-Vatican.

Watawa wa mashirika mbali mbali nchini wametakiwa kujitoa bila kujibakiza na kumtumikia Mungu katika maisha yao waliyoyachagua kupitia mashirika mbali mbali. Wito huo ulitolewa na Askofu Method Kialini Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Bukoba, Tanzania wakati wa homilia yake katika Misa Takatifu ya kufunga nadhiri na Jubilei kwa Wanashirika wa Shirika la Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu. Ibada ya Misa Takatifu ilifanyika katika nyumba Mama iliyoko Nyaigando katika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba Kashozi, Jimbo katoliki la Bukoba Tanzania, mnamo tarehe 8 Desemba 2023, ambapo Mama Kanisa huadhimisha Siku Kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili na Mashirika mengi ya kitawa, hutumia fursa hiyo katika maadhimisho ya kurudia viapo vyao vya kujitoa moja kwa moja katika njia ya kumfuata Yesu, kwa kuitikia “Tazama mimi hapa ya Maria.” 

Askofu Kilaini wakati wa Misa ya Nadhiri na Jubilei ya Watawa wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu Bukoba
Askofu Kilaini wakati wa Misa ya Nadhiri na Jubilei ya Watawa wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu Bukoba

Misa Takatifu iliadhimishwa na Askofu Method Kilaini Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Bukoba, kwa kushirikiana na Askofu mteule Jovitus Mwijage, Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga, Askofu Desiderius Rwoma, Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba pamoja na mpadre mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania, waamini ndugu na marafiki wa watawa hao.

Watawa wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wakifunga nadhiri za Kwanza
Watawa wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wakifunga nadhiri za Kwanza

Katika homilia yake Askofu Kilaini aliwataka mabinti walioweka nadhiri za kwanza kumtegemea Mungu kwa kila jambo na kujitoa bila kujibakiza licha ya changamoto watakazo kutana nazo, kuendelea kumtumikia Mungu daima na kujikabidhi kwa Mama Maria pamoja na kujitoa kwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu.

Misa ya Nadhiri za kwanza, daima na jubilei ya shaba na dhahabu, Bukoba Tanzania
Misa ya Nadhiri za kwanza, daima na jubilei ya shaba na dhahabu, Bukoba Tanzania

Katika homilia, aidha Askofu Kilaina alisema: “Mabinti zetu hawa bado ni wadogo licha ya kujitayarisha vizuri nao wameamua kuungana na hawa Batereza na kuwa Batereza kweli kweli karibu sana mkae na dada zenu na msiogope. Mmeingia mahali panapofaa kwani mkijitoa kwenu bila kujibakiza itakuwa ni Paradiso katika shirika hili. Kubali kuelekezwa na mtafika."

Washangwera wa Jubilei  katika Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Bukoba Tanzania
Washangwera wa Jubilei katika Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Bukoba Tanzania

Askofu Kilaini vile vile aliwataka masista walioweka nadhiri za kwanza katika Shirika hilo kujitoa maisha yao yote kwa Mungu na kuachana na mambo ya dunia kwani hayo mengine watayapata kwa ziada. Aliwasihi mabinti hao kukubali kuelekezwa na kuwatii wakubwa wao ili kuufikia utakatifu. “Shirika hili ni kongwe katika Afrika na hapa Bukoba ndio Shirika mama, hivyo mnavyojitoa katika shirika hili ninacho waomba wanangu mlioweka nadhiri za kwanza mkubali kujitoa katika shirika hili na mjisikie vizuri na wenzenu wanawakaribisha sana. Na katika jumuiya mtakapo kwenda wapende wakubwa zenu, waheshimu wakubwa zenu na kaa nao vizuri na kubali kuelekezwa ili muweze kufika adhma mnayoitiwa.” Akiendelea na mahubiri hayo  alisema kuwa "mnapoweka nadhiri katika shirika lolote njia ni moja licha ya changamoto zozote mtakazo kutana nazo" na kuwataka watawa "kulitangaza shirika na kujiamini, kutenda na kuwa karibu na watu na kuuonesha upendo wa Kristo kupitia wao."

Washangwera wa miaka 25 na 50 ya  utawa
Washangwera wa miaka 25 na 50 ya utawa

Askofu aliwahimiza hata waliofunga nadhiri za daima kwamba sasa wamefikia hatua muhimu ya kumtumikia Mungu katika maisha yao yote. Na wakati huo huo walioadhimisha Jibilei ya shaba ya  miaka 25 alisisitiza kuwa wameonesha mfano mzuri katika huduma yao na waendelee kama wana wa shirika na mfano wa Mama Maria, Wabaki hivyo hivyo.  Kwa upande wa waliosheherekea Jubilei ya miaka 50 alisema kuwa wamepigana vita vizuri ila mwendo hawajamaliza, na ndiyo maana walivikwa dhahabu iliyo safi, wameonesha hatua nzuri ile ya miaka 50 ya furaha na shida ambayo daima wamekuwa wakimkabidhi msulibiwa. Wao ni ishara kwa wengine hasa walioko nyuma  yao wanaoanza kwamba nao wanaweza kufikia kama wao

Wafunga Nadhiri za daima
Wafunga Nadhiri za daima

Katika misa  hiyo kwa hiyo kulikuwa na Masista 7 waliofunga Nadhiri za kwanza, Masista nane waliofunga  Nadhiri za daima, na wakati huo huo, kulikuwa na masista wanne walioadhimisha Jubilei ya  shaba ya miaka 25, na masista 11 walioadhimisha Jubilei ya dhahabu ya  miaka 50 ya Utawa. Kwa njia hiyo, misa ilipendeza kwa  maombi, sala, na nyimbo na vifijo, hasa wakati wa maandamano ya kuingia katika mis ana wakati wa kutoka katika ibada ya misa hiyo, watawa wakiwa na mishumaa inawaka, na wamevaa mataji vichwani mwao kama wamalkia. Katika siku kuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili, Masista 8 walifunga nadhiri za kwanza,8 nadhiri za daima, masista 4 Jubilei ya miaka 25, masista 11 Jubilei ya dhahabu ya miaka 50 ya Utawa katika Shirika Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, Nyaigando, Bukoba Tanzania.

Washangwera miaka 25 na 50 ya utawa,Shirika la Batheresia wa Mtoto Yesu Bukoba Tanzania
Washangwera miaka 25 na 50 ya utawa,Shirika la Batheresia wa Mtoto Yesu Bukoba Tanzania

Shirika la Masista wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu lijulikanalo (Batheresa) lilizaliwa Bukoba, mkoani Kagera, Tanzania mnamo mwaka 1933 kwa ajili ya kukabiliana na mahitaji makubwa ya kijamii, kiuchumi na kiroho ya wakazi wa eneo hilo. Nyumba Mama inapatikana  katika kijiji kiitwacho Nyaigando, kilomita chache kutoka Parokia ya Bikira Maria wa Mateso Saba, Kashozi, Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania. Mama Mkuu wa Shirika anaitwa Sr. Helena Bandiho. Shirika hili lina endelea kukua kimiito na watawa ambao wanajishughulisha katika utume wa hali zote za kibinadamu, kuanzia  na malezi ya miito, kutoa huduma ya Kanisa na kutunza usafi wa Makanisa(Sakrestia), aidha kufundisha dini na Elimu dunia hasa kwa Watoto, Wanawake na Vijana. Kwa njia hiyo Watawa hawa wanatoa huduma za shuleni kuanzia: Shule za Awali (chekechea) hadi Chuo Kikuu. Huduma nyingine za kijamimii ni huduma ya afya kwa wagonjwa katika  mahospitali. Katika huduma hizi ni wazi kwamba Watawa hawa wamegawanyika katika sekta mbalimbali za utume wa ndani na wa nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuendelea na mafunzo ya juu kwa watawa hao.

Askofu Kilaini wakati wa kuwavisha mataji wanaofunga nadhiri za daima
Askofu Kilaini wakati wa kuwavisha mataji wanaofunga nadhiri za daima

Kuhusu suala la mafunzo ya miito (Walelewa-Candidate),Shirika la Batheresa,aidha wanapokea wasichana  wote wakatoliki,(Come and see- Njoo na uone)hasa wenye nia ya kutaka kumjua Mungu, kupenda na kumtumika Mungu, kupitia shauri tatu za Kiinjili: usafi wa Moyo, Ufukara na Utii, na kwa njia hiyo wanawapokea wasichana hao kutoka pande zote waliohitimu Elimu ya Sekondari  na Vyuo.

Wanajubilei
Wanajubilei

Unaweza kusikiliza mahubiri ya Askofu Kilaini, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Bukoba Tanzania, aliyofanya tarehe 8 Desemba 2023 wakati wa nadhiri za kwanza, daima na maadhimisho ya jubilei ya miaka 25 na 50 ya Watawa wa Shirika la Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Jimbo Katoliki Bukoba:

Mahubiri ya Askofu Kilaini wakati wa misa za nadhiri na Jubilei miaka 25 na 50 kwa Batheresa
15 December 2023, 10:10