Tafuta

Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage anawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba tarehe 27 Januari 2024. Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage anawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba tarehe 27 Januari 2024. 

Askofu Jovitus Francis Mwijage Jimbo Katoliki la Bukoba! Mahojiano Maalum

Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage anawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba tarehe 27 Januari 2024, Ibada itakayoongozwa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania akisaidiana na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini pamoja na Askofu Almachius Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga. Ibada hii itatanguliwa na Masifu ya Jioni tarehe 26 Januari 2024 yatakayoongozwa na Askofu Flavian M. Kassala.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Oktoba 2023 alimteuwa Mheshimiwa sana Padre Jovitus Francis Mwijage kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Bukoba. Hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania, UMAWATA, Mjumbe wa Baraza la Seminari kuu Tanzania na pia Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS. Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage anawekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba tarehe 27 Januari 2024, Ibada itakayoongozwa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania akisaidiana na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Bukoba pamoja na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza wa Jimbo la Kayanga.

Nembo yake ya Kiaskofu: Sala, Uaminifu na Upendo
Nembo yake ya Kiaskofu: Sala, Uaminifu na Upendo

Ibada hii itatanguliwa na Masifu ya Jioni tarehe 26 Januari 2024 yatakayoongozwa na Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Katika Ibada hii, Askofu mteule atakabidhiwa ufunguo wa Kanisa kuu, atakula viapo na kukiri Kanuni ya Imani. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Askofu Flavian Matindi Kassala anamshukuru Mungu kwa uteuzi wa Askofu Jovitus, tayari kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu; uteuzi wake ni kilele cha sadaka na majitoleo yake kwa Kanisa; unyenyekevu na utii; msingi wa mafanikio katika majiundo yake ya elimu, maisha ya kiroho na utumishi wake ndani ya Kanisa. Ni mnyoofu katika maisha na utume wake!

Atasimikwa na Kardinali Rugambwa, Askofu Kilaini na Rweyongeza
Atasimikwa na Kardinali Rugambwa, Askofu Kilaini na Rweyongeza

Askofu mteule Jovitus Francis Mwijage alizaliwa tarehe 2 Desemba 1966 Jimboni Bukoba baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 20 Julai 1997 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, akabahatika kutekeleza dhamana na utume wake kama Paroko-usu Parokia ya Mwemage na Mwalimu na Mlezi Seminari Ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki la Bukoba. Kuanzia mwaka 2005 hadi 2011 alitumwa na Jimbo Katoliki la Bukoba kwa ajili ya kujiendeleza kwa masomo ya juu na hivyo kujipatia shahada ya uzamivu kwenye historia ya Kanisa kunako mwaka 2011. Kati ya mwaka 2011-2012 alikuwa ni Jaalimu wa historia ya Kanisa, Seminari kuu ya Segerea. Tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2023 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, Tanzania. Na tangu mwaka 2012 hadi uteuzi wake, alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania, UMAWATA na pia kuanzia mwaka 2020 ni Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS.

Askofu Jovitus

 

25 January 2024, 16:15