Askofu Odoki anatoa shukrani kwa Vatican kwa msaada wa Wakimbizi
Padre Isaac Ojok, - Lira na Angella Rwezaula ,– Vatican.
Askofu Sabino Ochan Odoki wa Jimbo Katoliki la Arua Kaskazini Magharibi mwa Uganda alitoa shukrani zake kwa niaba ya Kanisa kwa Vatican kufuatia na msaada uliotolewa kuwezesha ustawi wa wakimbizi waliopata hifadhi katika eneo hilo. Akizungumza katika mahojiano maalum siku ya Alhamisi tarehe 11 Januari 2024 na Mwandishi katoliki, Padre Isaac Ojok wa jimbo kuu la Lira nchini Uganda, Askofu huyo alisema jinisi alivyo na furaha kwamba Vatican kupitia Baraza la Kipapa la Maendeleo Fungamani ya Binadamu limetoa msaada kwa ajili ya Jimbo hilo katika kuhakikisha ustawi wao unahudumiwa.
Hata kama hakuweza kusema ni aina gani ya usaidizi uliotolewa, Askofu Odoki alisema ni furaha yake kwamba Jimbo la Arua kwa sasa limetambua huduma ya kichungaji inayotolewa kwa wakimbizi ambao wengi wao ni kutoka Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC. Kutokana na uhitaji huo wa kichungaji, Askofu huyo alitaja jimbo hilo kuwa limeunda Vikariati kwa ajili ya Wakimbizi na Wahamiaji na kwamba amemteua Padre Felix Drani kusimamia mawakala wa kichungaji wanaofanya kazi ya kupeleka huduma za kichungaji kwa wakimbizi. Hadi sasa Askofu huyo alisema Jimbo hilo limepokea mawakala wa kichungaji kutoka katika maeneo mengine yanayotoa huduma katika sekta mbalimbali za elimu, afya na katekesi ikiwa ni pamoja na kutoa ushauri nasaha katika maeneo ya kuhifadhi wakimbizi ndani jimbo hilo.
Pamoja na kuwasili kwa baadhi ya mawakala wa kichungaji ambao ni mapadre na watawa wa kike kutoka nchi nyingine, Askofu Odoki ametoa wito mpya kwa mashirika ya kidini ya ndani na nje ya nchi ili kufika jimboni kwake kusaidia katika kutoa huduma za kichungaji na kiroho kwa wakimbizi. Mapema mwaka 2023, Askofu Odoki alifichua kwamba Caritas Arua kwa usaidizi na ushirikiano kutoka kwa washirika wengine kama Caritas Ujerumani, Ubelgiji, Denmark na Caritas Italia walitoa mbengu na huduma nyingine za usaidizi kwa wakimbizi ili kusaidia na kuboresha maisha yao huku kukiwa na uhaba wa rasilimali.
Baadaye aliongeza kusema kuw jimbo hilo baadaye iliunganishwa na Shirika la Kijesuit kwa ajili ya huduma ya Wakimbizi (JRS) na programu maalum ya kutoa mafunzo kwa makatekista na mawakala wengine wa kichungaji kuhudumia katika kambi za makazi ya wakimbizi zilizoenea katika jimbo hilo. Jimbo la Arua lenye eneo lake la kijiografia Kaskazini Magharibi mwa Uganda likizungukwa na Sudan Kusini Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo upande wa Magharibi na linapongezwa kwa mapambano ya kutoa huduma ya kiroho na kichungaji kwa wakimbizi katika kambi zao za makazi. Wakongo, Wasudan Kusini na Wakimbizi kutoka nchi nyingine wanaopewa makazi nchini Uganda wanaendana na Sera ya Mlango Huria wa nchi kuhusu wakimbizi ambao unatoa haki salama kama vile uhuru wa kutembea, kupata ajira, elimu na huduma za matibabu.
Ikumbukwe Jimbo la Arua liko katika sehemu ya kaskazini-magharibi (pia inajulikana kama eneo la Nile Magharibi) nchini Uganda. Jimbo hilo limepakana upande wa kaskazini na Jimbo Katoliki la Torit na Jimbo la Yei (yote mawili yako Sudan Kusini); upande wa kusini na Jimbo Katoliki la Nebbi (Uganda); upande wa mashariki ni Jimbo Kuu la Gulu (Uganda); na upande wa magharibi na Jimbo la Mahagi-Nioka (katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo). Jimbo linashughulikia Wilaya tisa za kiraia na Jiji moja: Adjumani, Arua, Arua-mji, Koboko, Maracha, Moyo, Obongi, Terego, Yumbe na sehemu za Zombo. Makao makuu ya Jimbo na Kanisa Kuu yapo Ediofe, mjini Arua.
Eneo la Jimbo la Arua awali lilikuwa sehemu ya Jimbo la Gulu. Iliyoundwa kama Jimbo mnamo tarehe 23 Juni 1958, Wasimamizi wake ni Moyo Mtakatifu wa Yesu na Mama Yetu, Mpatanishi wa Neema zote. Eneo la asili lilijumuisha eneo ambalo sasa linaitwa Jimbo la Nebbi; Jimbo Katoliki la Nebbi lilijengwa mnamo tarehe 15Machi 1996. Askofu wa kwanza wa Jimbo la Arua alikuwa Askofu Angelo Tarantino wa Wamisionari wa Comboni. Alihudumu kuanzia mwaka 1958 hadi 1984. Askofu wa pili wa Jimbo la Arua alikuwa Askofu Frederick Drandua, aliwahi kuwa Msimamizi wa Kitume kwanza na kisha kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Arua tarehe 15 Agosti 1986. Alihudumu hadi alipostaafu tarehe 19 Agosti 2009. Askofu wa tatu na wa sasa wa Jimbo la Arua, ni Askofu Sabino Ocan Odoki, aliyewekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 21 Oktoba 2006 alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Gulu. Tarehe 19 Agosti 2009, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Arua. Na hatimaye aliteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Arua mnamo tarehe 20 Oktoba 2010.