Tafuta

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu: “Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa.” Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu: “Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa.”   (ANSA)

Baraza la Makanisa Ulimwenguni Ujumbe wa Noeli Kwa Mwaka 2023

WCC katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2023: Kauli mbiu: “Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa.” “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yn 1:3-5. Kwa hakika walimwengu wanaishi katika giza, kiasi kwamba, matatizo na changamoto zinaendelea kufifisha nuru ya matumaini pamoja na utashi mwema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anafundisha na kusadiki kwamba: “Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu. Akapata mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria akawa mwanadamu.” Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Vatican wanasema, Kristo Yesu ndiye Mwanga wa Mataifa na wanatamani sana kuona mwanga wake ukiwaangaza watu wote kwa mng’ao wa Kristo Yesu ung’aao juu ya uso wa Kanisa, kwa njia ya kuitangaza na kuishuhudia Injili kwa kila kiumbe. LG 1. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2023 unanogeshwa na kauli mbiu: “Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa.” “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu. Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.” Yn 1:3-5. Kwa hakika walimwengu wanaishi katika giza, kiasi kwamba, matatizo na changamoto za dunia zinaendelea kufifisha nuru ya matumaini pamoja na utashi wa kuweza kujipatia mahitaji msingi, mambo ambayo yanahatarisha pia ukweli na haki. Lakini kwa Wakristo sanjari na Jumuiya ya waamini, wakiwa wameungana na kuambata upendo wa Kristo Yesu, wanaitwa kusimama imara na thabiti dhidi ya woga, hali ya kukatisha tamaa, ubinafsi, uchoyo na kiburi na hivyo kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa walimwengu.

Wakristo wanaalikwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini
Wakristo wanaalikwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini

Kamwe Wakristo wasizamishwe na kutopea katika hali ya kukata na kujikatia tamaa, kwani ulimwengu unawahitaji sana wakati huu, pengine kuliko wakati wowote katika historia ya mwanadamu. Wakristo, kama wanafunzi wa Kristo Yesu pamoja na jumuiya za Kikristo zilizounganishwa katika upendo wa Kristo, wanaitwa kusimama kidete dhidi ya woga, kupinga uwongo, ubinafsi na uchoyo, na kutoa tumaini kwa ulimwengu wote. Waamini wasikate wala kukatishwa tamaa, kwa sababu Ulimwengu unahitaji zaidi kutoka kwao: ujasiri, ubunifu pamoja na msukumo sanjari na upendo wa kujitolea zaidi. Wakristo wakumbuke kwamba chemchemi ya nguvu ya uhai inapatikana katika kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, katika uchanga wake alionesha udhaifu na maisha yake yalikuwa hatarini; alikabiliana na umaskini kwa viwango mbalimbali mjini Bethlehemu na hatimaye, kukimbilia uhamishoni ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu.

WCC: Wakristo wawe ni nuru ya watu wa Mataifa
WCC: Wakristo wawe ni nuru ya watu wa Mataifa

Ni katika muktadha wa umaskini wa Mtoto Yesu, Kanisa linatambua mapokeo makuu ya Kiyahudi ya haki, aliyetangaza na kushuhudia ukaribu wa Mungu kwa waja wake, akawafunulia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kikomo pamoja ahadi ya Uumbaji Mpya. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumkaribisha katika nyoyo zao, Mwana wa Mungu ambaye sasa yuko karibu sana na waja wake; utakatifu wake umefumbatwa ndani ya ubinadamu, kiasi hata cha kushiriki asili ya binadamu na hatimaye, kuiinua juu kabisa. Yeye ni Imanueli - Mungu pamoja nasi milele. Ndiyo maana wachungaji kondeni wamepiga magoti kumwabudu na Malaika wanaimba: Utukufu kwa Mungu, juu mbinguni. Na amani duniani, kwa watu wenye mapenzi mema. Mashairi. Tunakusifu, tunakubariki, tunakuabudu, tunakutukuza. Tunakushukuru kwa ajili ya utukufu wako mkuu, Ee Bwana Mungu, Mfalme wa mbinguni, Mungu Baba, Ee Mungu Baba mwenyezi’ Ee Bwana Yesu Kristo, Mwana wa pekee, Mwanakondoo wa Mungu. Uondoaye dhambi za dunia, utuhurumie. Uondoaye dhambi za dunia, pokea ombi letu. Ewe mwenye kuketi kuume kwa Baba, utuhurumie. Kwa kuwa ndiwe uliye peke yako Mtakatifu, Ee Bwana Yesu, kwakuwa ndiwe uliye peke yako Mkuu, Yesu Kristo. Pamoja na Roho Mtakatifu katika utukufu wa Mungu Baba Mwenyezi, Amina.

Mtoto Yesu ni Mfalme wa haki na amani, upendo na mshikamano
Mtoto Yesu ni Mfalme wa haki na amani, upendo na mshikamano

“Gloria in excelsis Deo et in terra pax hominibus bonæ voluntatis. Laudamus te, benedicimus te, adoramus te, glorificamus te, gratias agimus tibi propter magnam gloriam tuam, Domine Deus, Rex cælestis, Deus Pater omnipotens. Domine Fili unigenite, Iesu Christe, Domine Deus, Agnus Dei, Filius Patris, qui tollis peccata mundi, miserere nobis; qui tollis peccata mundi, suscipe deprecationem nostram. Qui sedes ad dexteram Patris, miserere nobis. Quoniam tu solus Sanctus, tu solus Dominus, tu solus Altissimus, Iesu Christe, cum Sancto Spiritu in gloria Dei Patris. Amen. Sherehe ya Noeli ni chemchemi ya matumaini mapya, inayosheheni maisha pamoja na matumaini. Mtoto Yesu ni Mwanga wa Mataifa anayekuja kufukuzia mbali giza la dhambi na mauti na hivyo kuwakirimia waamini maisha yanayosimikwa katika ukweli pamoja na wokovu wa walimwengu. Kama watoto wa mwanga, Wakristo wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini katika ulimwengu unaoesheheni: vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, woga na wasiwasi wa maisha. Kama waamini wanaitwa kusimamia demokrasia, kutangaza na kushuhudia tunu msingi za kiinjili na utu wema pamoja na kuondokana na maamuzi mbele katika maisha. Sherehe ya Noeli iwawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha, matumaini kwa wagonjwa na wale wanaoelemewa na mtikisiko wa uchumi Kitaifa na Kimataifa, faraja kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linawaombea watu wote wa Mungu: haki, amani na usalama, ili kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbe, Noeli ni muda muafaka wa kumsherehekea Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, Mwanga wa Mataifa anayefukukiza mbali giza la dhambi na mauti. Kristo Mwanga wa Mataifa ayaangazie mapito ya wafuasi wake ili waweze kuwa kweli ni wafuasi amini wa haki na amani duniani. 

WCC Ujumbe Noeli 2023
02 January 2024, 13:45