Comece na Cec wanaomba Umoja wa Ulaya juhudi zaidi kwa ajili ya amani
Na Angella Rwezaula- Vatican.
Wajumbe wa kiekumene wanaowakilisha Baraza la Makanisa ya Ulaya (CEC) na Tume ya Mabaraza ya Maaskofu wa Umoja wa Ulaya (COMCE) walikutana na Balozi Willem van de Voorde, Mwakilishi wa Kudumu wa Ubelgiji katika Umoja wa Ulaya, tarehe 18 Januari 2024, mjini Brussels ili kujadili vipaumbele vya Urais wa Ubelgiji wa EU. Mkutano huo ulikuwa fursa nzuri ya kuwasilisha na kushiriki michango ya makanisa kwa maeneo makuu ya sera ya Urais wa Ubelgiji wa Baraza la EU. Makanisa ya Ulaya yalisisitiza haja ya kuimarisha demokrasia na umoja katika Umoja wa Ulaya, kushughulikia msingi na ubaguzi katika jamii. Katika muktadha huo, mchango chanya ambao makanisa yanaweza kuleta ili kuendeleza zaidi amani na haki katika Ulaya na nje ya nchi ulisisitizwa.
WASIWASI WA CEC NA COMECE
CEC na COMECE walielezea wasiwasi wao kuhusu matumizi mabaya ya dini, taarifa potofu, ubaguzi wa kijamii, utaifa na itikadi kali, hasa kwa kuzingatia uchaguzi wa 2024 wa Bunge la Ulaya. Makanisa pia yalisisitiza nia yao ya kufanya kazi pamoja na watunga sera wa Umoja wa Ulaya ili kuendeleza mazungumzo kuhusu nafasi ya dini katika jamii ya kidemokrasia, kuhakikisha kwamba haki za kimsingi zinaheshimiwa. Katika muktadha wa vita vinavyoendelea Ulaya na kwingineko, pamoja na mvutano unaoongezeka kati ya watendaji wakuu wa kimataifa, CEC na COMECE walihimiza Urais wa EU kuhakikisha juhudi endelevu za amani na utulivu. Walihimiza kuongeza mshikamano madhubuti kwa Ukraine na watu wake, na kuongeza juhudi za kidiplomasia kuelekea azimio la amani, haki na endelevu. Makanisa pia yalipata fursa ya kubadilishana na Balozi Willem van de Voorde baadhi ya vipengele nyeti zaidi vya Mkataba wa Umoja wa Ulaya wa Uhamiaji na Ukimbizi uliokubaliwa hivi karibuni.
CEC na COMECE zilikaribisha umakini uliotolewa na Urais wa Umoja wa Ulaya kwa ajili ya mabadiliko ya haki na mustakabali endelevu wa bara letu. Kulingana na makanisa ya Ulaya, lengo hili linapaswa kufikiwa bila kupuuza gharama yake ya kijamii wakati wa kutafuta maelewano ya kisiasa na kijamii. Kuhusu sekta ya kilimo, makanisa yalisisitiza haja ya kuunga mkono mazungumzo ambayo yanajumuisha uwakilishi mpana wa wakulima katika Umoja wa Ulaya. Wajumbe hao walithamini kipaumbele kilichotolewa na Urais wa Umoja wa Ulaya wa Ubelgiji kwa maendeleo zaidi ya Eneo la Elimu Ulaya, wakisisitiza jukumu la elimu isiyo rasmi na rasmi, pamoja na mtazamo kamili wa elimu kwa ajili ya maendeleo ya mafanikio ya mtu. Makanisa pia yalihimiza Urais kufanya mazungumzo na vijana kuwa sehemu ya kimuundo ya mchakato wa kidemokrasia wa Umoja wa Ulaya.
Mikutano na Marais wa Umoja wa Ulaya ni sehemu ya utamaduni wa muda mrefu unaoungwa mkono na Kifungu cha 17 cha Mkataba wa Utendaji wa Umoja wa Ulaya (TFEU), ambacho kinabainisha mazungumzo ya wazi na ya kawaida kati ya EU na Makanisa, vyama vya kidini au jumuiya. Na ujumbe wa CEC-COMECE uliundwa na:Padre Manuel Barrios Prieto, Katibu Mkuu wa COMECE, Mchungaji Dk. Peter Pavlovic, Katibu wa Utafiti wa CEC na Alessandro Calcagno, Katibu Mkuu Msaidizi wa COMECE
COMECE
Tume ya Mabaraza ya Maaskofu wa Umoja wa Ulaya(COMCE inaundwa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi zote za Wanachama wa Umoja wa Ulaya. Ilianzishwa mnamo 1980 kwa idhini ya Vatican kuwakilisha Mabaraza ya Maaskofu wa Umoja wa Ulaya ( EU) mbele ya taasisi za EU. COMECE hufanya mazungumzo na taasisi za Umoja wa Ulaya, ikitoa michango ambayo inakuza manufaa ya wote na mtazamo unaozingatia binadamu katika sera za Umoja wa Ulaya. COMECE inashirikiana mara kwa mara na Ofisi ya Tume ya Umoja wa Ulaya na Sekretarieti ya Vatican. Na Sekretarieti ya COMECE iko mjini Brussels, nchini Ubelgiji ambapo timu ya washauri hufuatilia, kuchambua na kuendeleza misimamo inayowasilisha mtazamo wa Kikatoliki kuhusu sera za Umoja wa Ulaya. Hati kuu za umahiri wa EU ambazo COMECE inafanya kazi ni zifuatazo:
• Haki na Haki za Msingi
• Masuala ya Kijamii na Kiuchumi
• Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya
• Uhuru wa Kimataifa wa Dini
• Uhamiaji na Ukimbizi
• Ikolojia, Nishati na Kilimo
• Maadili, Utafiti na Afya
• Tamaduni na Elimu
• Sera za Vijana
Muundo wa COMECE unajumuisha Mkutani Mkuu, Kamati ya Kudumu, Sekretarieti, Tume sita zinazoshugulika: (Masuala ya Kisheria, Masuala ya Kijamii, Mambo ya Nje, Uhamiaji na Ukimbizi, Maadili, Utamaduni na Elimu) na Ofisi ya Habari. Rais wa sasa ni wa Tuma hiyo ni Askofu Mariano Crociata, Askofu wa Latina nchini Italia na Katibu Mkuu wa sasa ni Padre Manuel Enrique Barrios Prieto.
CEC
Wakati huo huo Baraza la Makanisa ya Ulaya kwa sasa linajumuisha makanisa 114 kutoka maeneo yote ya Ulaya, yakitoka katika tamaduni za Kiorthodox, Kiprotestanti na Kianglikani. Mtandao wa Mabaraza ya Kitaifa ya Makanisa pia husaidia kuwaweka pamoja kwa kushikamana na masuala ya kitaifa na kikanda na Mashirika katika Ubia kuendeleza utaalamu wao katika maeneo kadhaa, ikiwa ni pamoja na diakonia, masuala ya uhamiaji na wakimbizi, na wanawake na vijana makanisani. Kama sehemu ya Juma la Maombi kwa ajili ya Umoja wa Kikristo, Afisa Programu wa CEC wa Taalimungu na Masomo Katerina Pekridou alitafakari kuhusu changamoto za kisasa za uekumene katika meza ya mduara iliyoandaliwa na Kikanisa cha Ulaya mnamo tarehe 18 Januari 2024 huko Brussels nchini Ubelgiji. Tukio hilo lilikusanya wawakilishi wa makanisa ya Ulaya. “Uekumeni ni harakati, lina misemo kadhaa, uzoefu, kiroho, mipango na programu.”
Pekridou alizungumza kuhusu majukwaa ya kiekumene yanayojulikana na changamoto zinazohusiana na tabia zao za kitaasisi. Alisisitiza umuhimu wa kuzingatia maneno tofauti ya mazungumzo ya kiekumene na kazi ya upatanisho wa Wakristo, pamoja na aina mbalimbali za vyombo vinavyofanya kazi kwa umoja wa Kikristo anapozungumza kuhusu uekumene. Kiutamaduni Juma la maombi huadhimishwa kuanzia tarehe 18-25 Januari, ya kila mwaka ambayo uhitimishwa katika sikukuu ya Mtakatifu Paulo. Katika ulimwengu wa kusini, ambapo Januari ni wakati wa mapumziko na makanisa mara nyingi hupata siku nyingine za kusherehekea, kwa mfano karibu na Pentekoste, ambayo pia ni tarehe ya mfano wa umoja.
Tuombe
Baba wa Mbinguni, tunakushukuru kwa zawadi ya Roho Mtakatifu, mpaji wa uzima, ambaye hutufanya kuwa wazi zaidi kwa kila mmoja, husuluhisha migogoro na huimarisha vifungo vyetu vya ushirika. Na ili tuweze kukua katika upendo wa pamoja na katika shauku ya kutangaza ujumbe wa Injili kwa uaminifu zaidi, ili ulimwengu ukutane katika umoja na kumkaribisha Mfalme wa Amani. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.