Tafuta

Maadhimisho ya Dominika V ya Neno la Mungu: Kauli Mbiu Kaeni Katika Neno langu. Yn 8:31 Maadhimisho ya Dominika V ya Neno la Mungu: Kauli Mbiu Kaeni Katika Neno langu. Yn 8:31  (Vatican Media)

Dominika ya V ya Neno la Mungu: Kaeni Katika Neno Langu, Yn 8:31

Dominika ya Neno la Mungu ni kwa ajili ya kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kulishuhudia Neno la Mungu, dira na mwongozo wa maisha. Maadhimisho haya ni matunda ya Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu na pia yana mwelekeo wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika: Uekumene wa damu, maisha ya kiroho, sala na huduma makini kwa maskini, kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya upendo wa Kristo Yesu inayomwilishwa katika maisha halisi.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Itakumbukwa kuwa dominika hii ilipewa jina la “Dominika ya Neno la Mungu” na Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake Binafsi “Motu Proprio” iliyopewa jina la Aperiut illis: “Aliwafunulia akili zao” ya 30/09/2019, katika kumbukumbu ya miaka 1600 ya kifo cha Mtakatifu Yeronimo Jalimu na Gwiji wa Maandiko Matakatifu. Lengo kuu ni kuliadhimisha, kulitafakari, kulieneza na kuliishi Neno la Mungu katika maisha ya kikristo, ikiwa ni pamoja na kusisitiza uhusiano uliopo kati ya Liturujia ya Neno na Liturujia ya Ekaristi Takatifu katika sadaka ya Misa Takatifu. Maneno ya mwanzo kabisa ya Aperiut illis yanasema; “Aliwafunulia akili zao ili waweze kuyaelewa Maandiko na kumtambua Yeye” (Luka 24:45).  Bwana wetu Yesu Kristo mfufuka, kabla ya kupaa kwake mbinguni aliwatokea wanafunzi wa Emaus waliokuwa wameshikwa na hofu na kukata tamaa, akawafunulia maana ya fumbo la Pasaka: yaani mateso, kifo na ufufuko wake ili kwalo awajalie watu wote wongofu na msamaha wa dhambi. Kabla ya kuwafumbua macho yao ili wamtambue kwa kuumega mkate (Sehemu ya pili ya Misa Takatifu, Liturujia ya Ekaristi Takatifu), kwanza aliwafafanulia, akiwafunulia na kuwaeleza habari zake jinsi zilivyoandika katika Maandiko Matakatifu, tangu Agano la Kale akianzia na Musa na Manabii wote, (Sehemu ya kwanza ya Misa Takatifu, Liturujia ya Neno). Kumbe bila kuyafahamu Maandiko Matakatifu, haiwezekani kulielewa fumbo la ukombozi wetu – mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo tunaloliadhimisha katika Sadaka ya Misa takatifu. Ndiyo maana Mt. Yeronimo aliweza kuandika: “Kutokujua Maandiko Matakatifu ni kutokumjua Kristo.” Tujitahidi basi kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu katika maisha yetu. Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2024 yananogeshwa na kauli mbiu “Kaeni katika Neno langu” Yn. 8:31.

Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu Kwa Mwaka 2024
Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu Kwa Mwaka 2024

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Yona (Yon. 3: 1-5, 10). Somo hili linatufunua ukuu wa huruma ya Mungu kwa wadhambi wanaotubu kama watu wa Ninawi walipohubiriwa na Yona. Itakumbukwa kuwa Nabii Yona alitumwa kwa Waninawi miaka ya 450 KK. Hiki ni kipindi baada ya Wayahudi kurudi kutoka uhamisho wa Babeli nao walijaa chuki, hasira na roho ya kisasi dhidi ya mataifa ya kigeni kwa mataso na madhila waliyoyapata wakiwa ugenini utumwani. Hivyo wakitamani kuona mkono wa Mungu ukiwaangamiza maadui zao, Yona akiwa ni miongoni mwa waliotamani kuona kisasi cha Bwana Mungu. Wakati akifikiri hayo ujumbe wa Mungu ukamjia aende Ninawi, taifa la kipagani, adui wa taifa lake akahubiri habari njema ya wokovu. Ili ngumu sana kwa Yona kuelewa huu wito. Hivyo ili hasira ya Mungu iwaangukie na kuwaangamiza watu wa Ninawi, Yona aliamua kutokwenda kuwahubiri habari za toba. Hivyo akapanda meli kuelekea Tarshishi ili kuukimbia na kujiepusha na uso wa Mungu. Katika harakati hizi Mungu alituma dhoruba kali ikaipiga meli hata ikaanza kuzama. Mabaharia wakaamua kutafuta ni kwa ajili ya nani madhila hayo yanawapata. Kura ikamuangukia Yona wakamtupa baharini nayo ikawa shwari. Yona alimezwa na kukaa ndani ya tumbo la Nyangumi kwa mda wa siku tatu na baadae akamtapikwa pwani. Ujumbe wa Mungu ukamjia Yona kwa mara ya pili. Ndilo somo la kwanza la dominika hii. Yona kwa shingo upande akauingia mji wa Ninawi na kutangaza hukumu juu yake akisema: Baada ya siku 40, Ninawi utaangamizwa. Yona alifikiri kuwa watu wa Ninawi ni wenye shingo ngumu, hawawezi kutubu. Hivyo adhabu na maangamizi, ilikuwa hakika kwake. Kinyume cha matarajio yake, watu wa Ninawi walimgeukia Mungu, wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia tangu aliye mdogo hadi aliye mkubwa na wanyama pia, wakafanya toba ya kweli. Mungu akawasamehe.

Kauli Mbiu: Kaeni katika Neno langu Yn 8:31
Kauli Mbiu: Kaeni katika Neno langu Yn 8:31

Yona akamlalamikia Mungu akisema; Nilijua mpango wako wa kuwakomboa watu wa Ninawi, ndiyo maana nikatoroka, kwa maana nalijua kuwa wewe ni Mungu mwenye huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya (Yona 4:2). Mungu akamkaripia Yona na kumfahamisha kuwa wana wa Ninawi nao wanastahili kusamehewa kwa kukiri na kutubu uovu wao. Kwa upande mwingine, Yona ni mfano wa watu wanaofuga chuki, hasira na kinyongo kwa maadui zao. Ni wale wanaoumia wanapoona wengine wanabarikiwa. Ni wale wanaolijihesabia haki na kujiona wa maana, wakiwadharau wengine wakiwaona ni wadhambi na walaanifu. Watu wa Ninawi walitubu, wakamwamini Mungu na kufanya toba ya kweli. Nasi kila mara tunapotenda dhambi hima tuikimbilie sakramenti ya kitubio tujipatanishe na Mungu, tuuvae unyenyekevu na utu wema ili tuweze kusaidiana sisi kwa sisi katika kuutafuta utakatifu. Kama wimbo wa mwanzo unavyotualika ukisema; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, mwimbieni Bwana, nchi yote. Heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake” (Zab. 96:1, 6). Naye mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyaongoze matendo yetu yafuate mapenzi yako, ili kwa jina la Mwanao mpenzi tustahili kutenda mema mengi.”

Kaeni katika Neno Langu Yn 8:31
Kaeni katika Neno Langu Yn 8:31

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 7:29-31). Somo hili linatuasa tujiandae, tuwe tayari mda wote kwa ujio wa pili wa Kristo siku ya kifo cha kila mmoja wetu. Chochote kile kinachoweza kuwa kikwazo kwa matayarisho kiachwe. Kwanza kabisa tuachane na tamaa potofu za kimwili. Sisi tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Mwili wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu. Tumekombolewa kwa damu ya Kristo. Kwa fumbo la pasaka, Kristo amempatia Mungu roho iliyookolewa na mwili uliotakaswa. Hivyo tunapaswa kumtolea Mungu miili yetu kama sadaka iliyo hai, takatifu na yenye kumpendeza. Hii ndiyo namna iliyo halisi ya kumwabudu Mungu (Rum 12:1). Pili tuachane na tamaa potofu za mali. Tumshukuru Mungu kwa zawadi ya vitu tulivyonavyo tukitambua kuwa sisi ni mawakili tu. Hivyo mali na utajiri tulizojaliwa na Mungu tuzitumie vyema kwa faida ya wote, hasa kwa kuwasaidia walio na uhitaji zaidi. Na tatu tuachane na tamaa potofu za heshima na vyeo kama anavyosema mtume Paulo kuwa wale watumiao ulimwengu wawe kama hawautumii, walio na mamlaka wawe watumishi wa wote.

Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu Kwa Mwaka 2024
Maadhimisho ya Dominika ya V ya Neno la Mungu Kwa Mwaka 2024

Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk. 1:14-20). Katika sehemu hii ya injili Yesu anatangaza kuwa ili tuweze kuwa karibu na ufalme wa Mungu yatupasa kufanya toba na kuianimi Injili. Mtume Yohane anasema kuwa tukisema hatuna dhambi twajidanganya na kweli haimo ndani mwetu. Lakini tukiziungama dhambi zetu, Mungu ni mwaminifu atatusamehe na kututakasa. Na tusipotubu hakika tutaangamia. Toba inatuweka huru kutoka katika kongwa la utumwa wa dhambi na minyororo ya shetani. Mwalimko mkuu ni wa toba na wongofu, kubadili mwelekeo wa maisha. Mwaliko huu ni wa hiari. Kila mmoja yuko huru kuupokea au la.  Kwa wanaoupokea msamaha uko wazi kwao na wanaoukataa moto wa milele ni haki yao. Baada ya kupokea msamaha, wajibu unaofuata ni kuiamini Injili, kujiweka chini ya utawala wa Mungu ili tupate kustahilishwa kuurithi uzima wa milele mbinguni. Kuingia katika ufalme wa mbinguni kunatudai kulipenda, kulisoma na kulitafakari Neno la Mungu lenye hazina na utajiri wa mambo yote yamhusuyo Mungu na ufalme wake kama anavyotuambia Mtakatifu Efraimu: “Bwana alitilia neno lake uzuri wa rangi mbalimbali, kusudi wale wanaolichunguza waweze kugundua ndani yake kile wanachokipendelea. Alificha hazina zote katika neno lake, kusudi kila mmoja wetu apate utajiri wake ndani ya lile analolitazama.” Basi nasi tulisome na kulitafakari daima Neno la Mungu ambalo ni taa ya maisha yetu ili tujifunze kwalo kuacha yaliyo mabaya na kuyatenda yaliyo mema kwa ajili ya ufalme wa mbinguni. Maana Bwana asema: Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima. Tumsifu Yesu Kristo!

Tafakari D3
16 January 2024, 14:27