Sudan Kusini:Askofu Mkuu wa Juba anawataka raia kuwa na matumaini kwa uchaguzi Desemba 2024
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Juba, nchini Sudan Kusini alitoa tafakari katika mwelekeo wa uchuguzi mkuu nchini mwao alioshirikisha wakazi, wake huku akiwaalika Wasudan Kusini kuwa na matumaini katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mnamo Desemba 2024. Askofu Mkuu Martin Mulla alisema “Ni nini kinachoweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia mwishoni mwa 2024? Sisi ni wanaume na wanawake ambao tunaleta matumaini kwa wengine; sisi ni watu wanaokaribisha changamoto, kama tulivyofanya tulipomkaribisha Papa Francisko nchini mwetu Januari 2023. Kisha tulikuwa na miezi miwili tu ya kujiandaa kwa ujio wake na tukio hilo lilikuwa zawadi kubwa kwetu sote.”
Kardinali Mulla alisema hayo katika wakati wa Misa ya Noeli tarehe 25 Desemba 2023 iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Teresa mjini Juba ambapo Kadinali Mulla alionesha imani kuwa Sudan Kusini kuwa inaweza kufanya uchaguzi huru na wa haki ifikapo mwisho wa 2024. “Kwa wengi walioshiriki ndiyo maana naunga mkono kuwa inaweza kuwa uchaguzi, nilisema kwamba katika kipindi cha miezi 11 au zaidi, mambo mengi yanaweza kutokea.” Kadinali huyo pia alithibitisha uungaji mkono kamili wa Kanisa mahali hapo kwa makubaliano ya amani yaliyohuishwa huku, akihimiza utekelezwaji wa masuala yaliyoachwa kutokana na migogoro inayoendelea kati ya makundi hayo mawili hasimu. Mkataba huo wa amani unaoitwa kuhuishwa ulitiwa saini tarehe 12 Septemba 2018 ili kumaliza vita vilivyoanza mwaka 2013 kati ya makundi hasimu yanayoongozwa na Salva Kiir, rais wa sasa, na Riek Machar, makamu wa kwanza wa rais wa nchi hiyo.
Sudan Kusini ilitakiwa kuhitimisha kipindi cha mpito kwa uchaguzi mwezi Februari 2023, lakini serikali ya mpito ilishindwa kutimiza masharti muhimu ya makubaliano hayo, ikiwa ni pamoja na kuandaa katiba na kuunganisha jeshi. Vyama katika makubaliano hayo kwa hakika vimeongeza muda wa serikali ya mpito kwa miaka mingine miwili, na kufanya uchaguzi mkuu kufikia Desemba 2024. Hata hivyo, waangalizi wengi wanaamini kuwa nchi hiyo kwa sasa haina uwezo wa kufanya uchaguzi unaoaminika kwani bado kuna kazi kubwa ya kujiandaa kwa uchaguzi huo. “Tuko kwenye mwisho wa utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyohuishwa, na sisi sote, kama watu wa kanisa, tunayaunga mkono, lakini kuna masuala muhimu ambayo tungependa kutekeleza kwa pamoja, Askofu mkuu wa Juba alisema. Baadhi ya kazi muhimu zinazohitajika kabla ya uchaguzi kufanyika ni pamoja na kufungua maeneo ya kisiasa na ya kiraia, kufadhili taasisi za uchaguzi, kuandaa katiba ya kudumu, kubainisha ustahiki wa wapigakura, mchakato wa kupiga kura, na kutumwa kwa vikosi vilivyo na mafunzo ya kutosha na vilivyo na vifaa.
Kabla ya mzozo huo kuzuka, watu milioni kumi nchini Sudan Kusini walihitaji msaada wa kibinadamu. Tangu uhuru wake mwaka 2011, nchi hiyo imekuwa eneo la migogoro ya silaha na migogoro ya kibinadamu. Tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 kumekuwa na vifo elfu 400 na mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao na hadi leo mivutano na migogoro baina ya jamii inaendelea.