Tafuta

Watu wakiwa wanachimba kaburi la maziko ya pamoja ya watu 200 huko Paleteau nchini Nigeria waliouwa kati ya tarehe 23 na 26 Desemba 2023. Watu wakiwa wanachimba kaburi la maziko ya pamoja ya watu 200 huko Paleteau nchini Nigeria waliouwa kati ya tarehe 23 na 26 Desemba 2023.  (AFP or licensors)

Nigeria,Askofu wa Sokoto auliza serikali:Je,ni akina nani hawa wauaji?

Mauaji wakati wa Noeli yanapita zaidi ya mapigano ya kiutamaduni ya vijijini au mashindano ya kidini,yanalenga kuivuruga Nigeria.Amesema hayo Askofu Matthew Hassan-Kukah wa Sokoto baada ya mauaji yaliyotekelezwa kati ya tarehe 23 na 26 Desemba 2023 mkoa wa Plateau.Karibu watu 200 waliuawa,500 walijeruhiwa huku familia 200 zililazimishwa kuacha nyumba zao na kutafuta makazi katika kambi za watu waliokimbia makazi.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Askofu Matthew Hassan-Kukah wa Sokoto mara baada ya mauaji yaliyotekelezwa kati ya 23 na 26 Desemba 2023 katika Jimbo la Plateau, anauliza swali kuwa:  “Je, tunawezaje kuendelea kuamini kwamba hakuna mpango wa muda mrefu wa kuchukua hatamu ya mamlaka katika jimbo la Nigeria?” Katika mashambulio yaliyoratibiwa dhidi ya takriban vijiji ishirini, karibu watu 200 waliuawa, 500 walijeruhiwa huku angalau familia 200 zililazimishwa kuacha nyumba zao na kutafuta makazi katika kambi za watu waliokimbia makazi. Habari zilizotolewa na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari, (FIDES) zinabainisha kuwa mashambulizi hayo yalihusishwa na wafugaji wa Fulani. Katika kile kinachojulikana kama Ukanda wa Kati, eneo ambalo kiutamaduni ni mpaka kati ya kaskazini, inayokaliwa kwa kiasi kikubwa na Waislamu, na kusini kuna Wakristo, huko nyuma kumekuwa na mapigano na mauaji kati ya Wafulani, ambao ni wafugaji wa Kiislamu wa kuhamahama na wakazi wenyeji ambao hujitolea kwa ajili ya kilimo na ni wakristo.

Ni hali iliyozidi mapigano ya kiutamaduni ya vijijini

Katika msururu wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya Nigeria, Askofu Kukah alielezea juu ya picha inayopita zaidi ya mapigano ya kiutamaduni ya vijijini au mashindano ya kidini. Kwa mujibu wa  Askofu wa Sokoto, anabainisha kuwa mauaji ya hivi karibuni  ni sehemu ya mpango wa kuyumbisha Shirikisho la Nigeria. “Mauaji haya ni utangulizi tu. Mauaji hayo si mapigano tena kati ya wachungaji na wakulima kuhusu malisho. Hapana, kuna zaidi na sisi kama taifa tutafanya vyema kushughulikia tishio hili kabla ya kuchelewa. Hakuna ubaya unaodumu milele. Ulimwengu umeshinda utumwa, ubaguzi wa rangi, unazi na aina za itikadi kali. Tungeweza kujifanya kuwa hatuko vitani, lakini kiukweli kuna vita vinavyoendelea dhidi ya serikali ya Nigeria na watu wake. Mungu apishe mbali, lakini inaweza kuanzishwa wakati wowote, mahali popote na kwa sababu yoyote ile.” Alikazia kusema Askofu Kukah.

Askofu anauliza Serikali ya Nigeria kwa matumaini ya kutaka majibu 

Kulingana na Askofu wa Sokoto ni kwamba “ili kukabiliana na hali hii ni muhimu kuondokana na mbinu ya kijeshi inayotegemea tu bunduki na risasi, lakini ni muhimu kuweka upya ulinzi wa  usalama wa taifa kwa msingi imara na wa kina, uchambuzi wa kiakili na kuchora ramani ya malengo ya nchi na hata matarajio, nafasi yake ya ndani, kikanda au kimataifa.” Kwa sababu hiyo Askofu,Kukah auliza baadhi ya maswali kwa wale wanaohusika na usalama wa serikali: “Tuna maswali yanayohitaji majibu:ni akina nani hawa wauaji? wanatoka wapi? Nani anawafadhili? Malalamiko yao ni yapi na dhidi ya nani? Wanataka nini? Wanafanya kazi kwa ajili ya nani? Haya yote yataisha lini? Kwa nini hawashindwi na hawaonekani? Nani anawapatia chanjo? Je, tunahukumiwa kuishi na haya yote na kukabidhi taifa hili lililovunjika kwa watoto wetu? Je, tunapaswa kutulizwa tu ili kufanya hili kuvumilika? Nani atatoa kasumba ya kupunguza maumivu yetu? Je, tunatembea kuelekea kujiangamiza?”

Askofu wa Jimbo la Sokoto auliza Serikali kuhusu mauaji ya watu 200 huko Plateau,Nigeria
08 January 2024, 15:02