SECAM NA CCEE KWA PAMOJA KATIKA TOLEO LA SEMINIA 24 NA 25 JANUARI 2024. SECAM NA CCEE KWA PAMOJA KATIKA TOLEO LA SEMINIA 24 NA 25 JANUARI 2024. 

SECAM,Nairobi:Januari 24-25,SECAM na CCEE watajadili Mwenendo wa Sinodi

Wawakilishi kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar(SECAM)na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya(CCEE)wanatazamiwa kujadili namna sinodi inavyounda Makanisa Barani Afrika na Ulaya.Ni katika semina itakayofanyika mjini Nirobi,Kenya kwa siku mbili ya 24 na 25 Januari 2024.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA), Padre  Anthony Makunde, ni kwamba wawakilishi wa Maaskofu kutoka mabara mawili  ya Ulaya na Afrika   ambayo yamekuwa na uhusiano wa muda mrefu tangu 2004, watakuwa na semina ya siku mbili katika mjini Nairobi, Kenya kwa kuongozwa na mada ya Sinodi: “Afrika na Ulaya wakitembea pamoja.” Semina hiyo itafanyika tarehe 24 na 25 Januari 2024  na linatarajiwa kuwa na maaskofu 20 kutoka Afrika na Ulaya ambapo itajikita katika nyanja mbalimbali za mada ikiwa ni pamoja na kulielewa Kanisa linalojikita ndani ya Sinodi katika nuru ya Katiba ya “Praedicate Evangelium,” kwa hisia ya bara ambapo  kikao cha kwanza cha Sinodi ya kisinodi na jinsi Kanisa linavyoweza kuwasikiliza vijana Barani Afrika na Ulaya katika nuru ya mchakato wa Sinodi.

Maaskofu watajadili kwa kuzingatia mazingira ya Afrika na Ulaya

Katiba ya Praedicate Evangelium (Hubiri Injili) ni Katiba ya Kitume ambayo ilitolewa na Baba Mtakatifu Francisko mnamo mwaka wa 2022, juu ya urekebishaji wa Curia Romana na huduma yake kwa Kanisa ulimwenguni. Hati hiyo inakazia kwamba kuhubiri Injili ndiyo kazi ambayo Bwana Yesu aliwakabidhi wanafunzi wake, na mamlaka yanajumuisha huduma kuu ambayo Kanisa linaweza kutoa kwa kila mtu binafsi na wanadamu wote katika ulimwengu mamboleo. Katika maeneo yote ya mada maaskofu wanapaswa kujadili katika semina hiyo huku wakizingatia mazingira ya Afrika na Ulaya.

Mshikamano na kukuza udugu

Tangu kuanza kwa uhusiano kati ya Maaskofu wa mabara mawili ya Ulaya na Afrika walikubali kuwa na mikutano yao kwa miaka mitatu. Semina ya kwanza ilifanyika Roma (ikiongozwa na mada: “Ushirika na mshikamano kati ya Afrika na Ulaya.” Semina ya mwisho  kuwa pamoja kabla ya janga la Uviko-19 ilifanyika huko Fatima nchini Ureno mnamo 2018 na iliaakisi maana ya utandawazi wa Kanisa na Tamaduni barani Ulaya na Afrika. Katika kikao kwa njia ya mtandao mnamo 2021, washiriki wa mabaraza ya maaskofu wa mabara  mawili walihimiza mshikamano na kukuza udugu, huku wakitoa wito kwa makanisa yote mahalia kufungua milango yao na kuwakaribisha watu wa Mungu kwa msingi wa majadiliano yao juu ya Waraka wa Papa Francisko wa Fratelli Tutti  yaani Wote ni ndugu ambao ulikuwa umechapishwa mnamo 2020.

Washiriki wa Semina hiyo

Baadhi ya wawezeshaji wanaotarajiwa katika semina ya siku mbili ni pamoja na Askofu Mkuu wa Nairobi, Philip Subira Anyolo; Rais wa SECAM, Kardinali Fridolin Ambongo Besungu wa Jimbo Kuu la Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC); Kardinali Jean -Claude Hollerich, Askofu Mkuu wa Luxembourg, Askofu Mkuu Gintaras Grušas wa Vilnius, Lithuania; Maaskofu Lucio Andrice Muandula wa Xai Xai, Msumbiji; Askofu Alexandre Joly wa Troyes, Ufaransa; na Askofu Bernardine Francis Mfumbusa wa Kondoa, Tanzania.

Semina ya SECAM na CCEE Nairobi Kenya
23 January 2024, 14:52