Tafuta

Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hawa mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine zaidi ya wana wa Israeli Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hawa mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine zaidi ya wana wa Israeli  

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Kristo Yesu Mwanga wa Mataifa

Mamajusi toka mashariki wamefika wakiwa na zawadi zao ambazo ni: dhahabu kujulisha kuwa huyu ni Mfalme, ubani kuwa huyu ni Kuhani na manemane kubashiri kifo. Mamajusi, kwa nyakati zile za kuzaliwa Yesu walikuwa ni watu wenye hekima na uwezo wa kutafsiri njozi ili kujua mambo yajayo na kusoma mapenzi ya Mungu katika matukio ya kawaida na yasiyo ya kawaida katika maisha. Kristo Yesu anajifunua kwa Mataifa kwa njia ya Mamajusi matendo makuu ya Mungu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Leo tunaadhimisha sherehe ya tokeo la Bwana, yaani Epifania. Neno Epifania lina asili yake katika lugha ya Kigiriki, maana yake ni kutokea, kujionyesha au kujifunua.  Mwanzoni Waisraeli walijiona kuwa wao ndiyo taifa pekee ambalo linapaswa kumngoja Bwana, kinyume chake Makabila mengine yalionekana kama watu wa mataifa na watu wasiomjua Mungu. Si hivyo tu, pia watu wasiotarajia chochote kutoka kwa Mungu.Tokeo la Bwana, yaani Kristo kujifunua kwa Mataifa yote ndiyo maana tutasikia katika Injili Mamajusi toka mashariki wamefika wakiwa na zawadi zao ambazo ni: dhahabu kujulisha kuwa huyu ni Mfalme, ubani kuwa huyu ni Kuhani na manemane kubashiri kifo. Mamajusi, kwa nyakati zile za kuzaliwa Yesu walikuwa ni watu wenye hekima na uwezo wa kutafsiri njozi ili kujua mambo yajayo na kusoma mapenzi ya Mungu katika matukio ya kawaida na yasiyo ya kawaida katika maisha. Mwinjili Mathayo anatuonesha kuwa hawa Mamajusi ni wawakilishi wa watu wa mataifa mengine zaidi ya wana wa Israeli waliopata kumwona Mtoto Yesu. Hivyo basi, leo katika dominika hii ya Epifania Nabii Isaya, Mtume Paulo pamoja na mwinjili Mathayo wanaonyesha waziwazi kabisa jinsi bwana alivyo jidhihirisha kwa watu ambao wao waliwaita “watu wa mataifa."

Mamajusi walikuwa ni wataalam wa nyota.
Mamajusi walikuwa ni wataalam wa nyota.

UFAFANUZI. Mpendwa msikilizaji na msomaji, Mamajusi ni watu gain? Hawa walikuwa wataalamu wa elimu ya nyota. Ni wanasayansi waliopenda kupekua mambo na kutafuta ukweli kupitia elimu ya nyota. Mamajusi walipoiona nyota ya pekee angani, walikumbuka utabiri wa Manabii Mika na Danieli usemao kwamba Masiha atakapozaliwa itatokea nyota ya pekee.  Tokeo la Bwana maana yake ni kujionyesha kwa Bwana, yaani Yesu Kristo, kwa mataifa, na tukumbuke kuwa katika mwaka wa liturujia mintarafu kipindi cha Noeli yaani sherehe za kuzaliwa Kristo humalizika na tukio la kutolewa Bwana hekaluni kisha tunaanza na kipindi cha kawaida cha mwaka wa Liturujia sehemu ya kwanza. Mamajusi ni mfano na shule endelevu kwetu wa Kristo wa nyakati hizi, wao walijisemea, tumeona nyota yake twende tukamwabudu. Hatari, uchovu na urefu wa njia havikuwakatisha tamaa, walidumu mpaka wakafika alikokuwa mtoto Yesu. Walipofika huko Yerusalemu walikwenda kwenye Ikulu ya Herode na kumuuliza, “yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake Mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.” Herode anaposikia habari za kuzaliwa kwa Masiha anafadhaika sana na kuhuzunika moyoni. Herode alikuwa kibaraka wa wakoloni wa Kiroma. Kwa hofu ya kunyang’anywa cheo chake aliwauwa watu wote aliowatilia mashaka, hata leo uchu wa madaraka katika kila kona ya dunia umeendelea kutamalaki, watu wengi wenye mwono huo wamewadhuru, binadamu wenzao hata kutoa uhai kisha kulinda au kutaka madaraka kwa nguvu na kwa manufaa yao, tunashuhudia vita na mapigano katika taasisi kubwa, Mataifa mbalimbali kisa nani ni mkubwa zaidi katika kutawala.

Mamajusi waliongozwa na nyota kumwabudu Yesu
Mamajusi waliongozwa na nyota kumwabudu Yesu

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anatabiri jinsi mataifa watakavyo ipokea ile nuru yaani Kristo Yesu, akisema ‘Namataifa wataijilia nuru yako …’   Pia Isaya anaendelea kutabiri akisema kutokana na ile nuru basi hakutakua na giza yaani dhambi zetu zinaondolewa. Tena katika somo la pili mtume Paulo ambaye anapewa heshima yakuitwa Baba wa mataifa anakazia na kusisitiza umuhimu wa usawa mbele ya Mwenyezi Mungu akisema ‘mataifa ni warithi wa pamoja nasi … maana yake Kristo alikuja kwaajili ya wote na si kwaajili ya Wayahudi pekee.  Hivyo basi, katika Sherehe ya tokeo la Bwana Kristo anazaliwa mioyoni mwa watu wa Mataifa nao kwa moyo mmoja wana mpokea kama mgeni wao wa heshima. Vivyo hivyo katika Injili Mamajusi wanakwenda Yerusalemu kumtafuta mtoto aliye zaliwa wakisema yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayaudi? Hii inatudhihirishia wazi kabisa kwamba Kristo hakuja kwa ajili ya Wayahudi tu bali kwa ajili ya watu wote, ndiyo maaana mamajusi kutoka mashariki ya mbali nao waridhihirishiwa uwepo wa masiha kwa njia ya nyota yenye mkia. Kwa kuonyesha kwamba wamtambua kristo ambaye amejidhihirisha kwao kama mfalme wakamtolea dhahabu, kama Mungu walimtolea ubani nakubabashiri ukombozi utakao kuja kwa njia ya kufa na kufufuka kwaka hawa kusita kumtolea manemane ili kubashiri kaburi.   Ndugu msikiizaji na msomaji wa Radio Vatican katika Injli tunasikia Herode anauliza swali Kristo azaliwa wapi? Ili swali ni vema kila mmoja wetu ajiulize na jibu lake kwa wote tuliojiuliza liwe hili ‘Kristo atazaliwa mioyoni mwetu kwani tukiruhusu kwa utashi wetu na uhuru kamili tukiongozwa na imani kwa Mungu, Kristo akikaa mioyoni mwetu tutamshinda yule mwovu yaani shetani ambaye kazi yake kubwa ni kuhakikisha Kristo hapati nafasi ya kuzaliwa mioyoni mwa watu. Kwa hiyo ndugu zangu katika Kristo tokeo la Bwana, litufanye tugandamane na Kristo ili azaliwe mioyoni mwetu.

Sherehe ya Epifania: Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa
Sherehe ya Epifania: Kristo Yesu ni Nuru ya Mataifa

KATIKA MAISHA. Sisi waamini tumejitoa vipi kwenda kumtafuta Bwana kama walivyofanya Mamajusi pamoja na vikwazo walivyopata toka kwa Mfalme Herode. Tumembebea na zawadi gani huyu Masiha? Tumechukua majungu, tamaa mbaya ufisadi, ukabila, fitina, na choyo kama zawadi kwa Bwana? Ni vizuri tupe Bwana zawadi za kufaa kama upendo, amani, utu wema na undugu kwa kila mtu. Sisi waamini ni wamoja kwa hiyo kwa pamoja tunaalikwa tushirikiane bila kubaguana wala kuonyeshana chuki iwe ni kwa sababu ya rangi, kabila, elimu, wingi wa mali zetu au cheo n.k. Ndugu zangu katika kristo daima tukumbuke kwamba Mungu wetu ni mmoja na anatupenda sote kwaule upendo mkuu alionao kwetu sisi kama baba hivyo ndugu zangu nivema na haki kabisa kuhudhihirisha huo upendo kkatika maisha yetu yakila siku hapa duniani.  Mamajusi walitumia elimu yao ya nyota kumtambua Kristo. Hayo ni matumizi mazuri ya vipaji tunavyopewa na Mungu hasa leo amabapo nachela kusema kuna maendeleo makubwa ya elimu na teknolojia mbalimbali ni kweli elimu imekuwa nuru ya kupunguza ujinga au au elimu tunayopataimegeuka kuwa ujinga ulioboreshwa na kutupeleka gizani zaidi? Je! nasi tunatumiaje vipaji vyetu. Kila mtu anacho kipaji alichojaliwa na Mungu. Je! Inakitumia kumfanya Kristo ajulikane kwa watu? au unatumia kipaji chako kumfanya Kristo asijulikane? Kila mtu anayo nafasi katika mazingira yake kumfanya Kristo aliyejifunua kwetu azidi kujulikana. Kristo ni mwanga, tulikuwa gizani naye ametuleta katika mwanga. (Isa 9:2), “Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu, wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti nuru imewaangazia.”

Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu
Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu

Mamajusi wanatuonesha jinsi tunavyopaswa kutenda. Zipo nyakati ambazo hatuna uhakika kuwaMungu anataka nini kwetu. Zipo hali fulani ambapo hatuoni vizuri njia ambazo Mungu anataka tushike, hapa lazima tutafute. Twaweza kusoma katika biblia ili kuona ikiwa Yesu amewahi kuwa katika hali ya namna hiyo. Twaweza kuomba ushauri kutoka kwa viongozi wetu wa dini. Inatubidi kusali pia ili tuweze kufanya maamuzi mema. Mfalme huyu anatumia nafasi yake vibaya. Aliwauwa watoto ili kulinda cheo chake. Daima tukumbuke kuwa uongozi unatoka kwa Mungu. Mungu anatuongoza kupitia watu wake. Watu wanapomchagua kiongozi, Mungu ndiye anayechagua kupitia watu hao. (Sauti ya watu ni sauti ya Mungu.) Je! Sisi hatujawahi kuhatarisha, kutishia, au hata kutoa uhai wa mtu ili kulinda nafasi zetu? Hatujawahi kuwatakia wengine mabaya ili washindwe na sisi tuchukue nafasi zao? Hii ni changamoto kwetu sote, kila mmoja ajifikirie katka nafasi yake na ajiulize ni mara ngapi amewahi kusababisha madhara kwa wengine kutokana na nafasi aliyonayo Hitimisho: Wapendwa katika Kristo, Mungu amejifunua kwetu, amekuja duniani kutukomboa. Kwa kukubali kuchukua mwili na kuwa mwanadamu kama sisi amekuwa jinsi sisi tulivyo, ili na sisi tuwe kama yeye alivyo. Kuwa kama alivyo nikuushiriki utukufu wa Baba yake mbinguni. Katika kuja kwake wapo walio mkataa na walio mpokea. Sisi tuige mfano wa wale waliompokea. Pia tuwe mwanga kwa wale ambao bado hawajampokea, waweze kufanya hivyo, ili sote tupate kuuridhi ufalme wa Mungu uliokwishaandaliwa kwa ajili yetu sote. 

Sherehe ya Tokeo la Bwana
04 January 2024, 14:57