Tafuta

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote.  (Vatican Media)

Sherehe ya Ubatizo wa Bwana: Umuhimu wa Sakramenti ya Ubatizo: Mlango wa Imani

Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo; inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote; tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Yesu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa Sakramenti zingine zote, Ubatizo ni Sakramenti inayotuingiza katika ukristo, ni Sakramenti inayotuondolea dhambi ya asili na adhabu zake zote. Ni kwa njia ya ubatizo tunazaliwa upya, tunakuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Ubatizo unatupa uwezo wa kufa kwetu katika kutenda dhambi na kuzaliwa tena katika maisha mapya. Kwa ubatizo tunashirikishwa Fumbo la Pasaka, fumbo la ukombozi wetu. Ubatizo hutuwezesha kuingia kwa namna ya pekee katika ushirika wa Utatu Mtakatifu, kwani hutufanya kuwa watoto wa Baba, warithi pamoja na Kristo, na kuwa hekalu la Roho mtakatifu (KKK 1263). Ubatizo unatushirikisha ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Hii ndiyo maana ya “alama ya kiroho isiyofutika” tunayopata katika sakramenti hii. Ndugu mpendwa katika Kristo, leo badala ya kuadhimisha Dominika ya kwanza ya mwaka, kanisa linaadhimisha sikukuu ya ubatizo wa bwana. Hivyo ni sikukuu ya kukumbuka ubatizo wetu. Tunapoadhimisha sikukuu ya Ubatizo wa Bwana. ni nafasi ya kumshukuru Mungu kwa neema mbalimbali anazotujalia kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.Pia ni nafasi ya kutafiti mioyo yetu namna gani tunalinda na kudumisha neema za ubatizo wetu katika maisha yetu ya Ukristo. Je, unakumbuka siku ya ubatizo wako? Je unakumbuka siku, tarehe na mwaka uliopata sakramenti hiyo?   Kama unakumbuka, hongera sana na Mungu akusaidie uishi vema neema za ubatizo wako. Kama hukumbuki, pole sana ila jitahidi kukumbuka ili uweze kusherehekea siku hiyo muhimu sana katika maisha yako. Si ajabu hata kuna watu hawakumbuki siku za kuzaliwa kwao. Tarehe hizi za ubatizo, ndoa, upadrisho, kipaimara na komunyo ya kwanza ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo. Wengi tunakumbuka siku tuliofanyiwa mabaya, hata wengine huwa wanaandika kwenye daftari siku waliofanyiwa mabaya. Nawakaribisheni kukumbuka yaliyo mema ila mabaya tusamehe. Leo ni kumbukizi ya kubatizwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo!

Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha
Ubatizo ni mwanzo wa safari ya utakatifu wa maisha

UFAFANUZI: Baada ya dhambi ya wazazi wetu Adam na Eva, wanadamu walipoteza neema ya utakaso, na hivyo wakajitenga na Mungu Baba. Dhambi hiyo ya kwanza huitwa dhambi ya aisli. Hata hivyo, Mungu kwa huruma yake alimtuma mwana wake wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo ili awakomboe wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi na adhabu ya milele, na kurudisha tena urafiki wetu na Mungu uliyovunjwa kwa dhambi ya asili. Yesu alifanya hivyo ili kutupatia tena neema ya utakaso iliyo uzima wa kimungu rohoni mwetu. Tukitaka kupokea neema hiyo ya utakaso hatuna budi kuzaliwa mara ya pili kwa kupokea sakramenti ya ubatizo, kwa njia ya maji na Roho M. Rej Yn 3:5. Hivyo ubatizo hutuondolea dhambi ya asili na dhambi nyingine kama zipo na adhabu ya dhambi. Ubatizo hutufanya kuwa watoto wa Mungu na wa kanisa lake, na kuwa washiriki katika utume wa kanisa. Tunapoadhimisha sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana naomba sana tusichanganye kabisa Ubatizo wa Bwana wetu Yesu Kristo na Ubatizo wetu, iwe tulibatizwa tukiwa watoto wadogo au watu wazima. Kwanini sasa Yesu alibatizwa? Yesu alibatizwa kwa sababu ya malengo makuu matatu: Yesu alibatizwa kwa sababu alitaka kuonesha kuwa anashikamana na walimwengu. Ubatizo wake haukuwa wa maondoleo ya dhambi ulikuwa Ubatizo wa toba. Walimwengu ndiyo waliokuwa wanahitaji kwasababu ya kuwa wadhambi. Mfano, unapoenda kwenye msiba usiokuhusu, hufiki pale na kuanza kukata soga tu, bali unakuwa na huzuni kama waombolezaji wengine unaowakuta pale. Yesu alibatizwa ili kutoa fundisho kwetu juu ya toba. Kwani sisi tulio wadhambi ndiyo tunaohitaji. Mfano, mama anapotaka kumfundisha mtoto kula chakula na yeye anakula hata kama hahitaji. Kwa hiyo anakula ili kutoa mfano kwa wanaohitaji kula hicho chakula. Ndiyo ubatizo wa Yesu ulivyokuwa, alibatizwa ili kutuonyesha sisi tunachotakiwa kukifanya. Yesu alibatizwa kwa sababu alitaka kuyatakatifuza maji ya Ubatizo na kuweka Sakramenti ya Ubatizo. Katika somo letu la kwanza, Nabii Isaya anaorodhesha kazi za mtumishi wa Bwana. Mtumishi huyo mteule, aliyetiwa Roho Mtakatifu, anawaalika watu wote waje wapate huduma msingi na lazima katika maisha, kama maji, chakula, malazi, kuja kufurahi wakihakikishiwa gharma zote, na kukaa kwa furaha na Bwana wao zaidi Bwana atayafungua macho ya vipofu, atawatoa wafungwa gerezani na wale walio gizani wataona nuru. Atafanya kazi hiyo bila kukata tamaa mpaka atakapoweka hukumu ya kweli duniani.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka

Katika somo la Injili tumesikia Yesu akiwa na malengo haya 3 alivyobatizwa na utambulisho wa Mungu kuwa Yesu ndiye mwanaye mpendwa aliyependezwa naye. Yesu alikwenda mahali alipofanya kazi Yohane ili naye akabatizwe.Mwito aliyoutoa Yohane kwa taifa zima la Israeli kuwa litubu na  kupokea Ubatizo wa toba unakubaliwa pia na Yesu,kwa kuwa  alijitambua  kuwa sehemu ya taifa la Israeli.Ingawa watu wengine walikuwa na maswali mengi juu ya aliyekuwa anawabatiza kama ndiye Kristo  waliyeahidiwa,hivyo ndiye waliyekuwa wanamsubiri au siyo.Yohane anawaambia kuwa yeye ni mtangulizi,ni mjumbe tu mwenye uwezo wa kubatiza kwa maji. Mfalme mwenyewe anakuja, hivyo wamwamini kwa kuwa huyo ajaye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto. Ndipo walipobatizwa na Yesu pamoja nao. Mara baada ya Yesu kubatizwa,akiwa anaomba mbingu zilifunguka.Nabii Isaya alimwomba Mungu azindue kipindi kipya katika historia ya watu wake.”Laiti ungepasua mbingu na kushuka ili milima iteteme  mbele yako” (Is 64:1).Aliomba Mungu azifungue mbingu na ashuke chini kwa watu wake.Wakati wa Ubatizo wa Yesu ombi hilo lilisikilizwa.Mbingu zilifunguka,Mungu katika nafsi ya mwanawe alifika kwa watu wake.Kizuizi kilichowatenga binadamu na Mungu kilibomolewa.Yesu sasa ni mkono wa Mungu unaomshika binadamu na kumwinua ili amfikie Mungu. Tunalezwa kuwa Roho alishuka juu yake. Katika Agano la Kale tunaona kuwa Roho alishuka juu ya waisraeli (Is 63:11,14; Kut 19:11). Pia wajumbe mahususi wa Mungu walishukiwa na Roho wa Mungu, nao ni Musa pamoja na wazee (Nam 11:16-30), Waamuzi (Amu 6:34), Mfalme Daudi (1Sam 16:13) na Manabii (Ez 11:5). Yesu anashukiwa na Roho wa Mungu, hivyo anasimama sasa badala ya viongozi waliomtangulia. Kwa tukio hilo utabiri wa Nabii Isaya 11:1.Hata wewe ulipobatizwa, mbingu ilifunguka. Mtandao huu au mawasiliano haya yalifungwa pale ambapo dhambi ilipoingia duniani. Tunapotenda dhambi tunafunga mawasiliano. Yesu amekuja ili kutufungulia mbingu ili tuweze kuwasiliana na Mungu. Kwa njia ya Ubatizo, waamini wanafanywa kuwa viumbe vipya na kumvaa Kristo, wanafanywa kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa lake na wanawezeshwa kupokea sakramenti zingine.

Ubatizo ni alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu
Ubatizo ni alama ya kufa na kufufuka na Kristo Yesu

KATIKA MAISHA: Ni katika tukio hili Sakramenti ya Ubatizo imewekwa kuwa mlango wa imani ya kuingilia mbinguni. Rejea mazungumzo ya Yesu na Nikodemo. (Yoh 3:3). Ili Kanisa libaki kuwa taasisi ya wokovu kwa vizazi vyote na kwa kuwa Yesu alishaweka Sakramenti ya Ubatizo, alitoa amri kwa mitume wake kuwa, enendeni duniani kote mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu na kuwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu” (Mt 28:19). Sakramenti ya Ubatizo inatufanya tuzaliwe upya kwa mara ya pili kwa njia ya maji na Roho Mtakatifu. Kuvua utu wa kale, kumvaa Kristo na kujipamba kwa fadhila na utakatifu. Mara zote ubatizo hufungamana na imani. Maandiko Matakatifu yanatuambia kuwa toba na kumwamini Bwana Yesu humpeleka mtu kwenye Ubatizo uletao ondoleo la dhambi (Mdo. 2:26-28). Ndiyo maana mtume petro katika somo letu la pili anasema kuwa “katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na Yeye” (Mdo. 10:35). Kumcha mungu ni kuenenda katika mafundisho yake kwa imani na matendo, kwani imani bila matendo imekufa (Yak. 2:17), hivi tunapaswa kuishi kadiri ya imani yetu tuliyopokea katika ubatizo. Basi tunapoadhimisha Sikukuu hii ya Ubatizo wa Bwana kama familia ya Mungu, Sikukuu hii itukumbushe kuuishi vema Ubatizo wetu. Tusiusaliti. Ahadi zetu za Ubatizo zitukumbushe wajibu tulionao mbele ya Mungu wa kumsikiliza Yesu, kumpenda jirani na kulitumikia Kanisa lake na familia zetu. Leo kila mmoja wetu ajichunguze jinsi anavyouishi ukristo wake. Tunaweza kusema Mungu bado anapendezwa nasi? Hajachoshwa na kuchukizwa na maovu yetu? Licha ya dhambi zetu Mungu anatupenda daima. Mbingu ilishafunguliwa kwa ajili yetu sisi ili tuweze kumfikia Baba.Tusijifungie mbingu sisi wenyewe kwa dhambi zetu. Tupiganie kumpendeza Mungu daima na si vinginevyo. Tuchukue hatua tubadilike tumrudie yeye ili aweze kutujalia neema zake katika maisha yetu. Tunapoadhimisha ubatizo wa Yesu na sisi tukumbuke na ubatizo wetu sisi wenyewe. Je, ile nguo nyeupe tuliyopewa imebadilika rangi, yaani tumeichafua? Tuliambiwa nguo hiyo iwe ishara ya cheo chetu. Kumbe kuitwa Mkristo ni cheo. Je, tumeshuka cheo au bado ni wakristo hai. Ile furaha na neema ya ubatizo ipo au imetoweka? Je, ule Mshumaa tuliowasha unawaka au tupo gizani? Kwa hiyo tunapoadhimisha ubatizo wa Bwana na sisi tuna maswali mengi pia ya kujiuliza.

Ubatizo wa Bwana 2024
05 January 2024, 14:26