Sr. Maria Antonia Daniel Halot, aliyefariki dunia tarehe 4 Januari 2024 kwa ugonjwa wa Shinikizo la Damu. Sr. Maria Antonia Daniel Halot, aliyefariki dunia tarehe 4 Januari 2024 kwa ugonjwa wa Shinikizo la Damu.  

Sr. Maria Antonia Daniel Halot Aliyefariki Hivi Karibuni Azikwa Nchini Italia

Jumuiya ya watanzania, Jumamosi tarehe 20 Januari 2024 walikusanyika kwenye Kikanisa cha Nyumba ya Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana “Suore Francescane del Signore” kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani Marehemu Sr. Maria Antonia Daniel Halot, aliyefariki dunia tarehe 4 Januari 2024 kwa ugonjwa wa Shinikizo la Damu. Baada ya Ibada hii ya Misa Takatifu, Maiti ya Sr. Maria Antonia Daniel Halot ilisafirishwa hadi Caltanisetta kwa mazishi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.

Jumuiya ya watanzania wanaoishi nchini Italia pamoja na watu wenye mapenzi mema, Jumamosi tarehe 20 Januari 2024 walikusanyika kwenye Kikanisa cha Nyumba ya Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana “Suore Francescane del Signore” kumsindikiza katika safari yake ya mwisho hapa duniani Marehemu Sr. Maria Antonia Daniel Halot, aliyefariki dunia tarehe 4 Januari 2024 kwa ugonjwa wa Shinikizo la Damu. Baada ya Ibada hii ya Misa Takatifu, Maiti ya Sr. Maria Antonia Daniel Halot ilisafirishwa hadi Caltanisetta, kwenye Madhabahu ya “Signore della Città kwa sala na hatimaye, kuzikwa tarehe 22 Januari 2024 kwenye Makaburi ya Caltanisetta, Kusini mwa Italia. Kutokana na sababu mbalimbali wazazi wa Marehemu Sr. Maria Antonia Daniel Halot, hawakuweza kuhudhuria lakini Sr. Catharina Ilonga wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu ambaye ameiwakilisha familia. Nilipata bahati ya kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na hatimaye, kutoa mahubiri. Katika tafakari hiyo niligusia mambo makuu matatu: Fumbo la kifo katika maisha ya mwanadamu na matumaini katika Ufufuko wa wafu; Ushuhuda wa maisha na utume wa kimisionari kwa wale wamisionari waliokatiwa tiketi ya kwenda tu na hatimaye ni fumbo la maisha ya kijumuiya, mahali pa kujifunza kusikiliza kwa makini na kusikiliza kwa moyo! Nilikazia sanaa na ustadi wa kumngojea Bwana katika upole, ujasiri bila ushabiki wala makelele. Huu ni wakati tete sana katika maisha unaosimikwa katika ukimya uliosheheni matumaini. Hivi ndivyo tunavyopaswa kulisubiria Fumbo la kifo katika maisha. Lakini kabla ya kufikia hatima ya maisha ya mwanadamu, bado kuna Misalaba mbalimbali ya maisha, kumbe, kama waamini tunapaswa kujifunza sanaa na baraka ya kuweza kulisubiria Fumbo la kifo katika maisha.

Marehemu Sr. Maria Antonia Fabiola alikuwa ni mtu wa sala na mshauri makini
Marehemu Sr. Maria Antonia Fabiola alikuwa ni mtu wa sala na mshauri makini

Katika magumu na changamoto za maisha ni vigumu kwa mwanadamu kuwa na subira na kubaki mtulivu. Mara nyingi katika hali na mazingira kama haya, ni rahisi sana mtu kujikatia tamaa na matumaini kuanza kuyeyuka kama ndoto ya mchana! Kumbukumbu nzuri za zamani haziwezi kutoa faraja kwa sababu ya uchungu na mateso, hali inayoweza kukata mawasiliano hata katika maisha ya sala, lakini Mwenyezi Mungu daima yuko kati pamoja na waja wake. Wakati uchungu na magumu ya maisha yanafikia kilele chake, tumaini huchanua tena ghafla. Tujifunze kurejesha matumaini wakati wa uchungu na maumivu makali na kuanza safari ya Kipasaka, tayari kuuendea mwanga wa Kristo Mfufuka, ili aweze kupyaisha tena tumaini letu. Ikiwa tunaelemewa sana na Fumbo la Kifo, katika Kristo Yesu kuna tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Kama kuna kitu ambacho tuna uhakika nacho ni kwamba, tutakufa, lakini kwa njia ya zawadi ya Fumbo la Upendo wa Kristo Yesu na kwa kushinda kwake kutoka kwa wafu, anatukomboa kutoka katika kifo na kutushirikisha kwenye maisha mapya ya uzima wa milele. Tunapaswa kujifunza kuishi na mioyo inayowaka, miguu inayotembea kwa sababu maisha na utume wa kimisionari ni maisha na safari ya imani kama ilivyokuwa kwa Sr. Maria Antonia Daniel Halot, alipoanza kwa mara ya kwanza safari ya kimisionari nchini Italia, tarehe 29 Juni 2015. Kwa bahati mbaya hii imekuwa ni safari isiyokuwa na tiketi ya kurejea tena nchini Tanzania kati pamoja na ndugu, jamaa na watu wa Mungu katika ujumla wake.

Sr. Maria Antonia Fabiola Daniel Halot ni kutoka Jimbo Katoliki la Mbulu
Sr. Maria Antonia Fabiola Daniel Halot ni kutoka Jimbo Katoliki la Mbulu

Hivi karibuni Familia Ya Mungu nchini Tanzania imeadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara kwa kuongozwa na kauli mbiu “Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili.” Bagamoyo ukawa ni mlango wa imani. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara lilihimiza roho na sadaka ya umisionari na kwamba, sasa ni zamu ya Wakristo Barani Afrika kuwa wamisionari kwa kuwasaidia wengine kukua kiroho, kuamsha imani, kutangaza na kushuhudia Injili. Leo hii eneo la Parokia ya Bagamoyo lina kumbukumbu isiyofutika ya makaburi ya wamisionari wa kwanza waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Hata kwa wamisionari kutoka Tanzania, wameanza kuacha alama ya sadaka ya kimisionari ughaibuni. Hapa nchini Italia, Sr. Maria Antonia Daniel Halot anakuwa ni Mtawa wa pili kufia na kuzikwa Italia, kwa miaka ya hivi karibuni baada ya Sr. Mariana Nyakunga Mdemu aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba 2019 mjini Roma na kuzikwa tarehe 18 Oktoba 2019 huko Sicilia, Kusini mwa Italia. Tunaye pia Padre Agapito Mhando! Inasikitisha sana kwa Sr. Maria Antonia Daniel Halot aliyeweka nadhiri zake za daima, tarehe 15 Oktoba 2023, kumbukizi ya siku ya kuanzishwa kwa Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana “Suore Francescane del Signore” kunako mwaka 1885. Kwa hakika alikuwa ni mtu wa sala, mshauri wa ajabu, mvumilivu na mtu aliyeongozwa na Neno la Mungu kama dira na taa ya maisa yake. Kama ilivyokuwa kwa wamisionari waliofika Tanzania miaka 150 iliyopita na kusadaka maisha yao, vivyo hivyo sasa ni zamu ya watu wa Mungu kutoka Afrika kujisadaka katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo.

Hii ndiyo zawadi na sadaka ya kimisionari: maisha kwa ajili ya Injili.
Hii ndiyo zawadi na sadaka ya kimisionari: maisha kwa ajili ya Injili.

Kwa njia ya Mashauri ya Kiinjili, watawa wanachangamotishwa na Mama Kanisa kushuhudia unabii wao katika maisha na utume wa Kanisa; mfano na kielelezo cha upatanisho, haki na amani na kwamba, inawezekana watu kutoka katika makabila, lugha na mataifa mbalimbali kuishi kwa umoja, amani na upendo unaofumbatwa na Kristo Yesu kwa Kanisa lake. Muungano huu wa maisha ya upendo na udugu wa kibinadamu unaimarishwa kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya karama na mapaji mbalimbali, watawa wanaweza kuendelea kulipamba Kanisa, kwa kuwa waaminifu kadiri ya karama za waanzilishi wa mashirika yao ya kitawa na kazi za kitume. Watawa wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni kielelezo cha huduma makini inayomwlishwa katika maisha ya kimissionari, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, hususan miongoni mwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lakini ikumbukwe kwamba, maisha ya jumuiya ni fumbo linalopaswa kumwilishwa kila siku! Hapa ni mahali pa kujifunza sanaa ya kusikiliza kwa makini na kuzungumza kutoka katika sakafu ya moyo wa mtu! Jumuiya ni mahali pa kujifunza kutembea kwa umoja katika furaha, majonzi na magumu ya maisha, ili kupunguza na kama si kuepuka kabisa vifo vya msongo wa mawazo! Sr. Maria Antonia Daniel Halot umetuachia somo gumu la kujifunza sanaa ya kusikiliza kwa moyo!

Wito wa kujifunza sanaa ya kusikiliza kwa moyo!
Wito wa kujifunza sanaa ya kusikiliza kwa moyo!

Kwa ufupi historia ya maisha na utume wake inasomwa na Sr Mary Grace Niyigena wa Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana: Sr. Maria Antonia Daniel Halot alizaliwa tarehe 20 Desemba 1985 katika Kijiji cha Endamana kata ya Bashinet, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, nchini Tanzania. Alibatizwa tarehe 25 Desemba 1998 na kupewa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu pamoja na Kipaimara kwenye Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Parokia ya Bashinet. Alianza shule ya msingi kunako mwaka 1995 na kuhitimu masomo yake ya msingi mwaka 2001. Mwaka 2005 alijiunga na elimu ya sekondari ya Dongobeshi. Wakati huo huo, alikuwa ni mwanachama wa Legio Maria na Chama cha Wanafunzi Wakatoliki Tanzania, TYC na alibahatika kuwa ni kiongozi wa wanafunzi Wakatoliki wakati wa ujana. Kunako mwaka 2009 alijiunga na Shirika la Masista Wafranciskani wa Bwana “Suore Francescane del Signore.” Mwaka 2012 alianza malezi ya unovisi na hatimaye, akaweka nadhiri zake za kwanza tarehe 11 Januari 2014. Tarehe 29 Juni 2015 alitumwa kwenda Italia kama mwalimu na mlezi wa watoto katika shule ya awali. Na Mwaka 2023 akaanza masomo Chuo Kikuu cha LUMSA kilichoko mjini Roma. Tarehe 15 Oktoba 2023 akafunga nadhiri za daima. Na ilipogota tarehe 4 Januari 2024 akafariki dunia kwa ugonjwa wa shinikizo la damu. RIP.

Marehemu Sr. Antonia

 

22 January 2024, 16:16