Tafakari Dominika ya Tano Mwaka B wa Kanisa: Fumbo la Mateso Katika Maisha ya Mkristo!
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 5 ya Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatupa nafasi ya kutafakari thamani ya Mateso na magonjwa katika maisha yetu. Ujumbe ni huu, tukiyapokea kwa imani, nguvu, hekima na upendo wa Mungu vinadhihirika ndani mwake kwani ni kwayo tunakuwa karibu naye kwa kuwa tukiwa katika udhaifu tunaongeza juhudi za kusali kama wimbo wa mwanzo unavyotualika ukisema; “Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba; kwa maana ndiye Mungu wetu” (Zab. 95:6-7). Zaidi sana mgonjwa na mateso, ya wengine yanatupa nafasi ya kuwahudumia kwa upendo wa Kristo ndiyo maana mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Bwana, tunakuomba utulinde sisi watoto wako kwa pendo lisilo na mwisho. Na kwa kuwa twategemea tu neema yako ya mbinguni utuhifadhi daima kwa ulinzi wako”. Somo la kwanza ni la kitabu cha Ayubu (Ayubu 7: 1-4, 6-7). Maandiko matakatifu yanasimulia kuwa Ayubu alikuwa mtu mwema, mcha Mungu na mwaminifu, tajiri wa mifugo, alijaliwa zawadi ya watoto, hivyo alionekana kuwa amejaliwa wingi wa neema na baraka za Mungu kwa wema wake. Lakini mateso, magonjwa na mahangaiko yalipomkumba, Ayubu alipoteza mali zake zote, akafiwa na watoto wake, na yeye kupata ugonjwa mbaya wa ngozi ulioambatana na madonda na maumivu makali. Katika hali hii machoni pa watu akiwemo mke wake na rafiki zake, alionekana kuwa ametenda dhambi na kumwasi Mungu hivyo anapokea adhabu kutoka kwake. Ayubu alijitetea kuwa hajafanya uovu wowote ambao ungemstahilisha hiyo adhabu na ya kwamba yeye anaamini ni mpango wa Mungu katika maisha yake. Akiwa katika mateso makali hayo, Ayubu alikiri kwamba anampenda Mungu na Mungu anampenda. Hivyo aliendelea kumtumainia Mungu, naye akaona uaminifu wake, akamponya na kumbariki zaidi na zaidi.
Shetani alimshtaki Ayubu kwa Mungu kuwa anamwamini Yeye kwa sababu amempa ulinzi na mali nyingi. Naye Mungu alimpa shetani ruhusa amjaribu Ayubu ili kumthibitishia kuwa uadilifu wake hautegemei neema na baraka za mali alizonazo. Kumbe japo mateso na magonjwa ni matunda ya dhambi; lakini si kila mgonjwa ni mdhambi. Ndiyo maana Mitume walipomwuliza Yesu, ni nani aliyetenda dhambi hata mtu huyu akawa kipofu, Yesu alijibu: “Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye wala za wazazi wake. Alizaliwa kipofu ili nguvu za Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake (Yn 9:1ff). Kumbe Ayubu anatufundisha kumtumaini Mungu wakati wote na katika hali zote. Majaribu, mateso na mambo mabaya yanayompata mtu si lazima yawe matokeo ya dhambi zake. Mungu anaweza kuyaruhusu yampate ili kuthibitisha imani na uaminifu wake kwake. Wakati mwingine shetani huushambulia uadilifu wa mtu mwema ili amkufuru Mungu. Kumbe katika hali ya magonjwa na mateso yatubidi tumkimbilie Mungu, tukate rufaa kwake yeye mwenye uwezo wa yote atatuokoa. Ndivyo inavyotukumbusha zaburi ya wimbo wa katikati ikisema: “Bwana ndiye aijengaye Yerusalemu, huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, na kuziganga jeraha zao. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, akili zake hazina mpaka. Bwana huwategemeza wenye upole, huwaangusha chini wenye jeuri (Zab. 146:1-6).
Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 9:16-19, 22-23). Katika somo hili tunapata wasifu wa dini ya kweli na wa mhubiri wa kweli. Kuhubiri ni wito kutoka kwa Mungu na si matakwa na hiari ya mtu binafsi. Mhubiri anapokea kutoka kwa Mungu wajibu anaopaswa kuutekeleza kwa neema za Mungu. Hivyo hapaswi kujivuna wala kuhubiri anachotaka. Tena anapaswa kutambua kuwa asipoihubiri Injili atapata taabu kama anavyosema Mtume Paulo; “Ole wangu nisipoihubiri Injili”. Mhubiri anapaswa kuwa yote kwa ajili ya wote bila ubaguzi ili watu wote wapate kumjua Kristo. Katika somo hili mtume Paulo anatukumbusha wajibu wa kila mbatizwa wa kuihubiri Injili. Hii ni kwa sababu kila aliyebatizwa, ameshirikishwa ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo. Kumbe kila mbatizwa amepokea wajibu wa kuitangaza injili, kwa maneno na matendo yake. Katika kutimiza wajibu huu hatupaswi kujisifu wala kujivuna kwa lolote bali tufanye yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Tukumbuke daima kuwa sala zetu, mahangaiko yetu, mateso yetu na mema yote tunayoyafanya yana matokeo yake katika fumbo la mwili wa Kristo na daima hutoa matunda mema kwa sifa na utukufu wa Mungu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk 1:29-39). Katika sehemu hii ya Injili tunakutana na Yesu akihubiri juu ya Ufalme wa Mungu huku akiponya wagonjwa na kuwatakasa walio na pepo. Yesu kuwaponya wagonjwa ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa watu wake inayojidhihirisha kwa njia ya Yesu Kristo. Hiki ndicho walichoagua manabii wakisema: “Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, anayachukua magonjwa yetu (Isa 53:4). Mtakatifu Papa Yohane II akiwa Mwanza Tanzania katika Kanisa Kuu la Epifania 03/09/1990 akiwapa faraja wagonjwa alisema hivi; “Yesu bado yu karibu sana na wagonjwa! Yuko karibu na kila mmoja katika mateso. Yuko karibu na aliye katika upweke akiogopa na kuhisi kuwa hakuna yeyote anayeuelewa uchungu wake. Yuko karibu na wenye magonjwa yasiyotibika na wale wanaokufa. Yesu yuko pamoja nanyi kwa kuwa yeye aliye Mungu alipata mateso. Kwenye Bustani ya Gethsemane alihuzunika na kusononeka wakati akiikabili sadaka kuu. Mikono na ubavu wake bado vina alama za mateso na kifo chake. Hivyo msiogope kumruhusu Yesu kuyatumia magonjwa yenu kama neema maalum ya kuwasogeza karibu zaidi kwake. Kupitia udhaifu wenu, atawasaidia kukua katika hekima, busara na ufahamu wa kiroho. Zaidi ya yote kuweni na imani kwamba kwa muungano wenu na Kristo, mateso yenu yatazaa matunda mema ya kiroho kwa faida ya Kanisa na ulimwengu.”
Maneno haya ya Mtakatifu Yohane Paulo II yanatukumbusha kuwa kwa ubatizo tuliunganishwa na Yesu katika Fumbo la kifo chake na kufufuka kwake kwa ajili ya maisha mapya (Rum. 6:5), na tuliletwa ulimwenguni kwa ushuhuda na ushindi wake dhidi ya dhambi na kifo. Hivyo Yesu anatutaka tuimarishe muungano wetu katika imani na kuzidi kufanana naye (Rum 8:29). Katika magonjwa yetu anataka kutuonyesha katika miili yetu nguvu ya ushindi wa neema yake. Kama Yeye alivyoutwaa udhaifu wetu na kuyachukua magonjwa yetu. Nasi tunaalikwa kuutwaa udhaifu wa wengine kwa kuwasaidia wanaoteseka kwa matatizo mbalimbali. Namna hiyo tunapa nafasi ya kuziishi fadhila mbalimbali za kikristo kama vile kuwa na huruma kwa wanaoteseka, ukarimu na majitoleo kwa wahitaji, ujasiri katika shida, mashaka na taabu, nguvu palipo na udhaifu, upendo palipo na chuki, faraja palipo na huzuni. Tuombe basi neema na baraka za Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili tuyapokee mateso na mahangaiko yetu na ya wengine pasipo kunung’unika ili yaweze kutukomaza kiimani na kutuweka karibu zaidi na Mungu na hivyo tuweze kustahilishwa kuingia katika ufalme wake mbinguni. Ndiyo maana mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, umeumba vitu hivi ili vitusaidie hasa katika unyonge wetu. Tunakuomba utujalie viwe pia sakramenti ya kutuletea uzima wa milele”. Ndivyo anavyotuahidi Kristo katika antifona ya wimbo wa komunyo akisema; “Heri wenye huzuni; maana hao watafarijika, Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa” (Mt. 5:4-6). Hii inatudai tuishi tukiwa tumeunga na Kristo kama Mama kanisa anavyotuombea katika sala baada ya komunyo akisema: “Ee Mungu, umependa tushiriki mkate mmoja na kikombe kimoja. Tunakuomba utujalie kuishi tumeungana na Kristo, tupate kuzaa matunda kwa furaha kwa manufaa ya wokovu wa ulimwengu.” Basi ili tuunganike zaidi na Kristo tuwatembelee, tuwafariji na kuwasaidia kimwili na kiroho wagonjwa na wenye shinda mbalimbali kwa kusali pamoja nao, kuwasaidia waweze kupokea sakramenti ya Kitubio, Ekaristi Takatifu na Mpako wa wagonjwa na kuwaandaa kupokea mapenzi ya Mungu katika hali iliyo njema pale Mungu anapoamua kuwaita kuwashirikisha uzima mpya na wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!