Tafuta

Tafakari ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwa maskini na wahitaji zaidi. Tafakari ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa: Imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma na mapendo kwa maskini na wahitaji zaidi.  (AFP or licensors)

Tafakari Dominika IV ya Kipindi Cha Mwaka B wa Kanisa: Imani Katika Matendo ya Upendo

Masomo ya dominika hii yanatupa nafasi ya kutafakari namna gani matendo yetu yanavyopaswa kuakisi imani yetu. Na njia ni hii, kuiishi vyema amri kuu ya mapendo ndiyo maana mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, utujalie kukuheshimu kwa moyo wetu, na kuwapenda watu wote kwa mapendo ya kweli”. Katika kuiishi Amari ya mapendo tunapaswa kufuata maongozi ya Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wake! Upendo!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 4 ya Mwaka B wa Kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii yanatupa nafasi ya kutafakari namna gani matendo yetu yanavyopaswa kuakisi imani yetu. Na njia ni hii, kuiishi vyema amri kuu ya mapendo ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, utujalie kukuheshimu kwa moyo wetu, na kuwapenda watu wote kwa mapendo ya kweli”. Katika kuiishi Amri ya mapendo tunapaswa kufuata maongozi ya Mungu kwa ajili ya sifa na utukufu wake kama wimbo wa mwanzo unavyoimba ukisema; “Ee Bwana Mungu wetu, utuokoe, utukusanye kwa kututoa katika mataifa, tulishukuru jina lako takatifu, tuzifanyie shangwe sifa zako” (Zab. 106:47). Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kumbukumbu la Torati (Kumb 18:15-20). Katika somo hili, Mungu kwa njia ya Musa anaahidi kuwapa Waisraeli Nabii mwingine atakayewaongoza. Ahadi hii inatolewa kipindi ambapo Musa alikaribia kufa baada ya safari ya miaka 40 jangwani kuelekea nchi ya ahadi naye asingeweza kuingia katika nchi hiyo. Hivyo, ujumbe huu ulikuwa ni kuwafariji na kuwatia moyo wasijekata tamaa kwa kifo chake. Kwani Mungu atawapa kiongozi mwingine kama yeye Musa naye atanena maneno ya Mungu na sio maneno yake na watu watapaswa kumsikiliza. Ndiyo maana zaburi ya wimbo wa katikati inasisitiza kuisikiliza sauti ya Mungu ikikumbusha yaliyomsibu Musa asiingie nchi ya ahadi ikisema; “Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu, kama vile huko Meriba, hapo waliponijaribu baba zenu, wakanipima, wakayaona matendo yangu. Njoni, tumwimbie Bwana, tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumfanyie shangwe kwa zaburi. Njoni, tuabudu, tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba. Kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi tu watu wa malisho yake, na kondoo za mkono wake” (Zab. 94:1-2, 6-9).

Mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wanaotengwa na jamii
Mashuhuda wa Injili ya upendo kwa maskini na wanaotengwa na jamii

Ahadi hii ya Mungu ilikumbukwa daima na Wayahudi. Ndiyo maana alipotokea Yohani Mbatizaji, walimuuliza: “Je, wewe ndiye Nabii yule ajaye?” (Yn. 1:22). Kristo Yesu ni yule Nabii ambaye Mungu kwa kinywa cha Musa aliwaahidi watu wake. Ndiyo maana mtume Petro katika mahubiri yake kwa Wayahudi baada ya kumponya mlemavu mbele ya lango la Hekalu alisema: Kwa maana Musa alisema; “Bwana Mungu wenu atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu, itawapasa kumtii huyo kwa kila jambo atakalowaambia. Mtu yeyote ambaye hatamsikiliza huyo nabii, atakataliwa mbali kabisa na watu wake. Yesu ndiye Nabii na Masiha ambaye Musa alitabiri habari zake” (Mdo 3:22-23). Naye Stefano katika hotuba yake kwa Wayahudi kabla hawajamuua kwa kumpiga mawe alisema: Huyu ndiye yule ambaye Musa aliyewaambia Waisraeli: “Mungu atawainulia nabii kutoka miongoni mwa ndugu zenu” (Mdo 7:37). Basi nasi tunapaswa kuyasikiliza daima maneno ya Kristo Yesu Bwana wetu akituongoza daima kutenda matendo mema yatakayotustahilisha kuingia mbinguni, nchi yetu ya ahadi. Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 7:32-35). Katika somo hili Mtume Paulo anaeleza bayana kuwa katika Kanisa kuna aina mbili za namna ya maisha nazo ni maisha ya ndoa na maisha ya useja. Hivyo anatoa ufafanuzi wa namna ya kuishi maisha ya ndoa na useja kitakatifu. Kwanza kila mtu anatakiwa kumtumikia Mungu kadiri ya maisha aliyochagua. Mseja matendo yake yanatakiwa kumdhihirisha kuwa yeye ni mseja na ameyatoa maisha yake kwa ajili ya Mungu tu. Mtu wa ndoa naye anapaswa kushughulika na mambo yahusuyo ndoa na ampendeza Mungu katika mambo yahusuyo ndoa. Paulo anatoa angalizo juu ya uchaguzi wetu wa maisha, kuwa kila mtu achague vema mtindo wa maisha anayopenda na kuyaweza kuyaishi. Hivyo anatoa ushauri kwa kila mtu kujipima vema kabla ya kuchagua na kuingia katika mtindo wa maisha anayoyachagua yawe ya ndoa au ya useja. Kila mtu anatakiwa kuchagua mtindo ambao ataweza kuuishi vyema akimpendeza Mungu. Kumbe katika uchaguzi wa maisha tusifuate mkumbo bali tuchague vyema ili tusiishi kwa ubabaishaji na huzuni na mfadhaiko maisha yote.

Kristo Yesu anaendelea kuita watangazaji na mashuhuda wa Injili
Kristo Yesu anaendelea kuita watangazaji na mashuhuda wa Injili

Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk 1:21-28). Katika sehemu hii ya Injili, mwinjili Marko anatueleza jinsi Yesu Kristo, baada ya kuwaita Mitume wake wanne: Simon, Andrea, Yakobo na Yohane, alivyoanza utume wake huko Kapernaumu akidhihirisha ukuu wake kama Masiha aliyeahidiwa katika Agano la kale kwa kufundisha, kuponya wagonjwa, na kufukuza pepo wachafu. Maandiko Matakatifu katika Agano la Kale, yalieleza kuwa maradhi na kupagawa na pepo wabaya ni mapato ya dhambi chini ya utawala wa shetani. Kwa maana “Mungu hakuifanyiza mauti, wala haimpendezi kuona watu wakipotea…ila ulimwengu uliingiliwa na mauti kwa husuda yake shetani, nao walio wa upande wake hupata kuionja” (Hek 1:13, 2:24). Hivyo Yesu kufanya miujiza ya kuponya maradhi, ni uthibitisho kwamba yeye ni Masiha aliyefika kuvunja utawala wa shetani na dhambi. Kwa ubatizo tumetengwa na shetani na kuungana na Kristo. Sisi tuliobatizwa na kumvaa Kristo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya nguvu tulizojaliwa za kupambana na mwovu shetani. Imani yetu kwa Kristo inatosha kabisa kupambana na pepo wabaya. Kumbe hatuna sababu ya kuogopa. Maana Kristo akiwa upande wetu hakuna wa kututisha maana hata pepo wachafu wanamtambua kuwa yeye ni Mtakatifu wa Mungu na mbele zake wote wananyamazishwa (Mk 1:25). Basi na tuidhihirishe imani yetu kwa maneno na matendo yetu kwa ajili ya uzima wa milele kama anavyotuombea mama kanisa katika sala baada ya Komunio akisema; “Ee Bwana, sisi tuliokula sadaka ya ukombozi wetu, tunakuomba utuzidishie daima imani ya kweli kwa chakula hicho kiletacho uzima wa milele”. Tuwe kweli na Imani dhabiti ili kwa maneno na matendo yetu tumshuhudie Kristo katika maisha yetu ili kwayo watu wengine waweze kumtambua na kumfuata nao wapate uzima wa milele tukafurahi pamoja milele yote mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo. 

Tafakari D4

 

25 January 2024, 15:39