Wamisionari wa Damu Azizi Yesu Wapata Mapadre 11 na Shemasi 1!
Na Ndahani Lugunya, - Dodoma.
Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kuhusu wito na maisha ya Daraja Takatifu ya Upadre anapenda kukazia sana kuhusu: Umuhimu wa huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu kuwa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa sababu Kristo Yesu ndiye chemchemi ya upendo kwa waja wake. Wakleri wanakumbushwa kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu, wao kimsingi ni: waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja Takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Kwa namna ya pekee, ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani: Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Sakramenti ya Upatanisho, inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhudana vyombo vya huruma ya Mungu, inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao! Huu ndio urithi unaojikita katika Mafundisho tanzu ya Mama Kanisa. Ni ukweli ambao wakleri wanapaswa kuumwilisha katika maisha na utume wao, kwa njia ya Roho Mtakatifu. Padre daima anapaswa kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Ibada kwa Bikira Maria inawawezesha wakleri kujifunza kutoka katika shule ya Bikira Maria, ili kweli waweze kuwa wafuasi na mitume hodari wa Kristo Yesu kwa kusikiliza na kutenda kama alivyokuwa Bikira Maria. Daima amekumbusha kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa, ni watu wanaopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa.
Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Askofu mkuu Beatus Michael Kinyaiya, OFMCap. Wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania, amewataka Mapadre na Mashemasi wapya kuwa ni watunzaji wa imani ya Kanisa, kanuni maadili na utu wema; wawe ni vyombo na mashuhuda wa furaha, matumaini na mapendo! Wajitahidi kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa moyo wa uchaji na Ibada na kwamba Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, waamini wote wanapaswa kuishi maisha adili na matakatifu. Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi Kanda ya Tanzania inaendelea kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwajalia Mapadre 11 na Shemasi mmoja. Nalo Shirika la Madonda Matano ya Yesu lina mshukuru Mungu kwa kuwawezesgha kupata mashemasi wa tatu kwa mkupuo, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Damu Azizi ya Yesu, Kisasa, Jimbo kuu la Dodoma. Askofu mkuu Beatus Michael Kinyaiya, OFMCap. Amewataka Mapadre wapya na Mashemasi wapya kutangaza, kushuhudia na kuishi kikamilifu kile wanachofundisha na kuamini. Leo hii kuna makundi mbalimbali yenye misimamo mikali ya kidini na kiimani. Kundi la kwanza ni wale wasioguswa na ukosefu wa haki jamii ndanya jamii. Kundi la pili ni wale wanaotaka Mapadre wawahalalishie matendo maovu kijamii, kwa mfano mahusiano ya kimapenzi kwa watu wa jinsia moja. Baadhi ya watu ndani ya jamii watawataka Mapadre kujifungamanisha sana na jamii. Watu mbalimbali wenye mahitaji mbalimbali watawaendea, huku wakitafuta majibu ya maswali na changamoto zao.
Watambue kwamba, wameitwa na kutumwa kuwahudumia watu wa Mungu ili waweze kuzaliwa upya katika mwanga wa Ufalme wa Mungu; huku wao wakiwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha, amani, matumaini na mapendo na kwamba, haya ni mambo wanayopaswa kuyapatia kipaumbele cha kwanza kabisa katika maisha na utume wao, huku wakiwa ni mfano mzuri kwa jirani zao kwa njia ya: maisha ya sala, maadili mema na uchapaji kazi bora. Mapadre wapya wasimame kidete kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Watambue kwamba vijana wa kizazi kipya wanahangaika kutafuta utambulisho katika ulimwengu mamboleo, kumbe wawe ni msaada wao, wawakusanye na kuwasaidia vijana katika safari ya maisha yao. Askofu mkuu Beatus Michael Kinyaiya, OFMCap., akiwageukia Mashemasi wapya, amewataka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya upendo wa Mungu, unaojidhihirisha katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, linalopaswa kuadhimishwa kwa imani na uchaji mkubwa na kwamba, watu wote wa Mungu wanahimizwa kuziishi kikamilifu Amri na Maagizo ya Mungu, kila mtu akitambua cheo, dhamana na utume wake ndani ya Kanisa, ili kutimiza vyema wajibu wao. Amehitimisha mahubiri yake kwa kuwaalika watu wa Mungu kuombea miito mitakatifu ndani ya Kanisa, ili vijana wengi wapende kuwa ni Mapadre na Watawa na kamwe wazazi wasiwe ni vikwazo kwa watoto wao na badala yake, wawaruhusu na kuwahimiza kufanya kazi katika Shamba la Bwana. Mashemasi kumi na moja waliopewa Daraja Takatifu ya Upadre kutoka Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, C.PP.S., ni: Padre Appolonius Byarugaba, Pd. Livinus Benedikto; Pd. Bonaventura Maro, Pd. James Titus Makinda, Pd. Aidani Alphonce Mtui. Wengine ni Pd. Abibon Rukiza, Pd. Abelhard Dimosso, Pd Gregory Ndeshilo, Pd. Revocatus Gimbuya, Pd. Joseph Richard pamoja na Padre Ernest Shirima. Majandokasisi waliopewa Daraja Takatifu ya Ushemasi kutoka Shirika la Madonda Matano ya Kristo Yesu ni: Shemasi Onesmo Paulo Ngo’o, Shemasi Alex Lukwawila, Shemasi Khoabane Lelimo pamoja na Shemasi Wilbrant Urio, C.PP.S., wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu.