Dominika ya Sita Ya Mwaka B wa Kanisa: Siku ya 32 ya Wagonjwa Ulimwenguni 2024
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
Mpendwa msikilizaji na msomaji Dominika hii ya 6 ya Mwaka B tunakamilisha sehemu ya kwanza ya kipindi cha mwaka tukielekea kipindi cha Kwaresima na hatimaye Kipindi cha Pasaka. Katika dominika hii tunamwona Yesu tabibu akiponya magonjwa ya mwili na roho, na pia kurejesha amani na thamani ya utu mtu, heshima na haki zake msingi, kwani ukoma ulikuwa ugonjwa mbaya sana ambaye alibainika amepata ugonjwa huu alitengwa na jamii, hivyo Yesu anapokea ombi na kumtakasa aliyetambua ukuu wa Masiha huyu wa Nazareti. Leo Mama Kanisa anaadhimisha Siku ya 32 ya Wagonjwa Ulimwenguni inayonogeshwa na kauli mbiu: “Si vuzri kwamba mwanadamu awe peke yake.“ Uponyaji wa Wagonjwa Katika Kuponya Mahusiano.“ Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kushinda upweke katika maisha; thamani, utu na heshima ya mwanadamu; anakazia ukaribu wa huruma na upendo kwa kujikita katika huruma na upendo wa Kristo Yesu na kwamba, wagonjwa wako katika kiini cha maisha na utume wa Kanisa. UFAFANUZI: Dominika iliyopita tuliangazia maana na thamani ya mateso yetu, tukaona umuhimu wa majaribu katika kukuza imani na jinsi mateso hayo yanavyotusogeza karibu na Mungu. Katika somo I (Law 13:1-2, 44-46) na Injili (Mk 1:40-45) unazungumziwa ugonjwa wa ukoma. Ugonjwa huu ulikuwa tatizo kubwa kwa wayahudi hivi kwamba ukikupata utaonekana mtenda dhambi nambari moja duniani uliyelaaniwa na Mungu, hivi utavaa kengele, kaniki na kutengwa, “mwenye ukoma nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu na atapiga kelele, ni najisi ni najisi. atakaa peke yake, makazi yake yatakuwa nje ya malago.”
Kadiri ya somo la Kwanza, Makuhani ndio walithibitisha kuwa huyu ana ukoma atengwe au amepona arudi hivi Yesu alitaka mgonjwa huyu aruhusiwe kujiunga tena na jamii yake... Alitaka pia mamlaka na wakuu watambue kuwa Nabii Mkuu ametokea katika Israel na utabiri wa manabii umetimia kwamba Masiha atakapofika vipofu wataona tena, viziwi watasikia, bubu watasema, viwete watatembea, wafu watafufuliwa, wenye ukoma watatakaswa na masikini kuhubiriwa Habari Njema (Mt 11:5). Yesu anakutana na mgonjwa anamuhurumia, ananyosha mkono wake, anamgusa na kumponya. Tendo hili lina maana kubwa, limebeba moyo wa upendo na kujali, Kristo hamnyanyapai mgonjwa, hageuzi uso wake mbele ya huyu aliyetengwa na wote bali anamsaidia kwa kiwango kikubwa kabisa. Hapa tugusike wote, tukutane na wenzetu wenye shida, tusiogope kunyoosha mikono yetu ya msaada kwa kadiri tunavyoweza. Yesu anatufundisha namna ya kuishi na wenye shida ili nao waonje joto na thamani ya upendo. Hata hivyo yule mkoma hakai kimya, anatangaza habari hiyo kwa kila mtu hivi kwamba Yesu analazimika kujitenga na watu. Mwanzoni mgonjwa huyu alitengwa sasa amepona yupo tena kwenye jamii lakini Kristo anachukua nafasi yake akijitenga na jamii, maana yake Kristo anawatoa watu kwenye dhiki na kuchukua nafasi zao, “hakika ameyachukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu, atawafanya wengi kuwa wenye haki, naye atayachukua maovu yao” (Isa 53:3, 11b).
Huyu mkoma alipata furaha kisha kuponywa. Nasi tumeponywa ukoma wetu kila mmoja kwa kadiri yake. Bwana Yesu ametugusa katika nafasi mbalimbali za maisha kwa mikono yake, ametuhurumia na ametutakasa. Ameponya ukoma wa ugomvi na mtu niliyekuwa nampenda sasa tunaishi kwa amani. Ameponya ukoma wa majivuno sasa nina unyenyekevu. Nilikuwa na ukoma wa umasikini lakini Mungu amenijalia ninaweza walau kupata chakula asubuhi, mchana na jioni, ninaweza kubadili nguo ninapooga na kusafiri nikipata dharula. Nilikuwa na ukoma wa ulevi, lakini Kristo amenitakasa na sasa nakunywa kwa kiasi nikimfikiria pia mwenzangu wa ndoa na watoto wetu kwa mahitaji yao. Nilikuwa na ukoma wa kujisahau wajibu zangu lakini Kristo amenigusa nimepona, sasa ninawajibika ipasavyo katika ofisi yangu, biashara, shambani na popote ninapohitajika. Nilikuwa na ukoma wa kijicho na wivu, Kristo ameniponya na sasa nafurahia maendeleo ya jirani yangu, ninaongea vizuri juu yake, simnyanyapai katika madhaifu yake na ninaishi naye vizuri, nina amani na watu wote “Nimrudishie Bwana nini kwa ukarimu wake wote alionitendea, nitakipokea kikombe cha wokovu, na kulitangaza Jina la Bwana.” (Zab 116:12-13) Ee Mungu ninakushukuru! Tunayo mengi nafsini mwetu yanayohitaji utakaso. Tuanguke miguuni pa Kristo alivyofanya yule mkoma tukisema “Bwana, ukitaka waweza kunitakasa”. Dunia ni nzito inanielemea, nimekandamizwa na mengi, moyo wangu ni mzito, mengi yananibabaisha, wenzangu hawanielewi, nimefiwa, naumwa, sina amani, sina fedha, hakuna anayejali, “Bwana ukitaka waweza kunitakasa na haya yote!”... Yesu ni mwema, jibu lake moja tu “Nataka takasika” mkristo tabasamu!
Tunapopokea neema ya kitubio na msamaha wa Mungu, tunapofinyangwa na kufanywa wapya rohoni, tunapojaliwa mahitaji na kukaa vizuri na wenzetu, ni lazima tuuone ukuu wa Mungu na kukiri utukufu wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema “furaha ya Injili inaenea, kujaa mioyoni na kuonekana katika maisha ya wote wanaokutana na Yesu na kupokea ofa ya ukombozi. Kwa neema yake wanafanywa huru na dhambi, wanaondolewa huzuni zao na kumaliziwa kabisa upweke wao. Ndani ya Yesu furaha yetu haiishi bali inafanywa mpya wakati wote.” kwa sababu ya neema hiyo inayoonekana kwetu leo tunasali tukimshukuru Mungu Baba yetu. Utukufu wa Mungu na ukuu wake havielezeki, huruma zake hazichunguziki na mamlaka yake hayana kipimo. tutumie karama zetu vizuri kwa sifa na utukufu wa Mungu vile tunavyoaswa na Mt Paulo katika somo II (1Kor 10:31- Kwake yote yanawezekana, sifa, utukufu na heshima apewe Yeye milele na milele. Huruma ya Mungu i juu ya wote wamchao, wamwendeao kwa mioyo mitulivu na unyenyekevu wakisema “Bwana unihurumie mimi mwenye dhambi”. Tufungue mioyo ili nguvu ya uponyaji ipenye rohoni mwetu na kutujaza mema ya kimbingu, tulishike neno la Mt. Paulo anakazia anaposema “mlapo au mnywapo au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” (1Kor 10:31), Amina!