Jugo Media Kumbukizi ya Miaka 5: Uzinduzi Wa Ofisi ya Uzalishaji wa Vipindi
Na Yuventa Mahela, Dar es Salaam na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake kwa njia ya Kristo Yesu. Ikumbukwe kwamba, mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake.
Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Uandishi wa habari za Kanisa ni taaluma yenye usumbufu mwingi. Lakini hii ni sanaa ya kutafuta na kusimulia matukio mbalimbali ya maisha na utume wa Kanisa. Hii pia ni njia ya kumpenda mwanadamu, kwa unyenyekevu pamoja na majitoleo makuu. Hii ni kazi yenye magumu yake, lakini jambo la msingi ni kwamba, hii ni kazi nzuri inayotia moyo wa kumpenda binadamu na kuendelea kujifunza kwa unyenyekevu. Hii ni changamoto kwa wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kuzama zaidi katika asili na roho ya matukio; kwa kusimamia ukweli wa maisha na utume wa Kanisa, kwa kuzingatia madhumuni yake ya maisha ya kiroho, maadili na utu wema, badala ya kung’ang’ania na kujikita tu katika kashfa zinazolichafua Kanisa! Wadau wa tasnia ya mawasiliano ya Kanisa wajifunze kuwa na “aibu ya kukaa kimya.”
Baba Mtakatifu Francisko anawapongeza waandishi wa habari za Kanisa kwa kazi kubwa wanazozifanya katika kutafuta na kuandika ukweli. Anawataka wazingatie ulinganyifu wa habari na tafakari; kuzungumza na kwa kusikiliza; kwa kuwa na utambuzi mpana pamoja na upendo. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, vyombo vingi vya mawasiliano ya jamii vinalenga kuandika habari za kupotosha mambo ya kidini na kukuza maelekeo ya kiitikadi na kisiasa kwa kutoa habari nyepesi nyepesi. Baba Mtakatifu anawataka wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii kutangaza na kushuhudia ukweli, bila kupiga makelele yasiyokuwa na mafao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa: Kanisa lina dhamana ya kujikita katika mchakato wa mawasiliano yaliyo bora zaidi kwa njia ya ushuhuda kabla ya hata ya kusema maneno. Ni katika muktadha huu wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji mtu mzima: kiroho na kimwili, Jugo Media, “Justina na Gores” chombo cha uinjilishaji kwa njia ya mitandao ya kijamii, kinafanya kumbukizi ya Miaka mitano tangu kilipoanzishwa na Ibrahim Gores, tarehe 19 Februari 2019. Hiki ni chombo ambacho kinaendelea kujikita katika utangazaji na ushuhuda wa Habari Njema ya Wokovu, mchakato unaofumbata uinjilishaji na utamadunisho, lengo kuu likiwa ni kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili kupitia mitandao ya kijamii au kwa maneno mafupi, hii ni Injili kiganjani mwako.
Hivyo basi, tarehe 19 Februari 2024, Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA., wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka Mitano tangu kuanzishwa Jugo Media alibariki na hatimaye, kuzindua Ofisi ya Uzalishaji wa Vipindi “Jugo Media Production Center” huko Msimbazi Center. Ofisi hii ina Studio ya kurekodi kwaya na waimbaji binafsi; Urushwaji wa Ibada mbalimbali mtandaoni pamoja na uzalishaji wa albamu na picha za matukio kama: Ubatizo, Kipaimara, Upadrisho na Nadhiri. Ofisi hii pia inajishughulisha na utunzaji wa matukio ya kijamii kama vile: Ndoa, Send off, mahafali ya shule pamoja na mazishi. Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, OSA., amewapongeza sana Jugo Media kwa kuzindua Ofisi ya Uzalishaji wa Vipindi, kwa kuendelea kujipambanua katika uwajibikaji mkubwa unaosimikwa katika unyenyekevu na utayari; mambo ambayo yanaweza kuwafikisha mbali katika muktadha wa uinjilishaji, kiburi na majivuno ni kaburi katika maisha na utume wowote ule.
Kwa upande wake, Askofu Msaidizi Henry Mchamungu Kyara wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam amewatia shime wana Jugo wote, akiwataka kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu pasi na hofu; matatizo na changamoto za maisha na utume wao zisiwe ni vikwazo bali fursa ya kusonga mbele. Wakumbuke kwamba, “hata Mkuyu ulianza kama mchicha”, vyombo vikubwa vinavyosikika sehemu mbalimbali za dunia vilianza kidogo kidogo na hatimaye, kuweza kufikia hatua kubwa zaidi. Amewataka waendelee kumtumainia Mungu naye atawabariki. Kwa upande wake, Ibrahim Gores, Mkurugenzi Mtendaji wa Jugo Media amesema kwamba, Jugo Media ni matunda ya: Kwaya ya Familia Takatifu, Parokia ya Mtakatifu Yosefu, Jimbo kuu la Dar es Salaam na daima wameendelea kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kupitia kwa uongozi wa Parokia na sasa Jugo Media inalelewa na kusimamiwa na Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Viongozi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam wameahidi kutoa ushirikiano zaidi na Jugo Media ili iweze kutoa huduma bora zaidi. Watu wengi wa Mungu Jimbo kuu la Dar Es Salaam wanaguswa sana na weledi na utayari; sadaka na majitoleo yao na kwamba, utekelezaji wa dhamana na majumu yao ni sadaka kubwa. Katika hafla hii, Peter Kisoki, Mwakilishi wa Jugo Media Jimbo Katoliki la Morogoro ametunukia nishani ya kuwa ni Mwana utume bora katika kipindi cha mwaka 2023-2024. Hafla hii imehudhuria na viongozi wakuu wa vyama vya Kitume, Jimbo kuu la Dar Es Salaam, waamini, marafiki pamoja na wadau mbalimbali wa Jugo Media.