Nigeria,Maaskofu:Mageuzi ya kiuchumi yamesababisha umaskini uliokithiri
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kutokana na mageuzi ya serikali, mamilioni ya Wanigeria wamegubikwa kuwa maisha ya umaskini uliokithiri, mateso ya ajabu na ugumu wa maisha ambao haujawahi kutokea katika historia ya taifa letu. Ndivyo alisema Askofu Mkuu Lucius Iwejuru Ugorji, wa Jimbo Kuu la Owerri na rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria (CBCN), akikosoa mageuzi ya kiuchumi yaliyozinduliwa na serikali ya Rais Bola Tinubu katika hotuba yake ya ufunguzi katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa kila mwaka wa Baraza la Maaskofu Nigeria (CBCN).
Kupanda kwa bei ya mafuta mara tatu
Raia wa Nigeria wanakabiliwa na kupanda kwa bei ya mafuta mara tatu na kupanda kwa gharama za chakula baada ya Rais Tinubu, akiwa madarakani tarehe 29 Mei 2023, kubatilisha ruzuku ya mafuta na kuelekeza sarafu ya taifa ya naira katika masoko ya bidhaa kwa viwango vya ubadilishaji wa kimataifa. Hii ina maana kwamba thamani ya naira dhidi ya sarafu nyingine haiamuliwi tena na benki kuu ya Nigeria bali na masoko ya fedha za kigeni. Kulingana na uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi (Nigeria inazalisha mafuta ghafi lakini lazima kutoka nje ya nchi kwa sababu uwezo wake wa kusafisha hautoshi kukidhi soko la ndani) na chakula, Nigeria imeshuhudia mfumuko wa bei ukipanda kwa kasi, jambo ambalo limeathiri zaidi sehemu maskini zaidi za wakazi.
Watu wamesalia kuomba omba
Rais Tinubu anasema kwamba athari mbaya za mageuzi hayo zitakuwa za muda mfupi, kwa sababu katika muda mrefu mageuzi yatakuwa na athari chanya kwa kuvutia uwekezaji wa kigeni katika uchumi wa taifa. Wakati huo huo, hata hivyo, idadi ya watu inateseka. “Katika kujaribu kuishi, idadi inayoongezeka ya watu maskini wanakimbilia kuomba omba. Pamoja na zaidi ya Wanigeria milioni 80 wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wa chini ya dola mbili kwa siku, nchi yetu, kulingana na takwimu za hivi karibuni kutoka Benki ya Dunia, ni ya pili kwa watu maskini zaidi duniani baada ya India” alisema Askofu mkuu Ugorji.
Matatizo mengi yanatokana na mageuzi ya kiuchumi
Na kuongeza kusema kuwa “Wanaigeria wengi maskini wanaendelea kuteseka na kufa kutokana na matatizo yanayosababishwa na mageuzi ya kiuchumi ya serikali, rais ameendelea kuwahimiza watu kujitolea zaidi na zaidi kwa kujua kwamba siku bora zaidi zinakuja.” Rais wa Baraza la Maaskofu kisha akazungumzia suala la ukosefu wa usalama, akisisitiza kwamba licha ya fedha zinazotolewa kila mwezi kwa ajili ya vikosi vya usalama, kumekuwa na ongezeko la utekaji nyara kwa ajili ya fidia na mauaji nchini kote.