Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka: Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake. Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Pasaka: Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake.  

Tafakari Dominika ya Pili ya Kwaresima Mwaka B: Kuimarika Kwa Imani na Matumaini

Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake. Akawaonesha kwamba, hatima ya maisha ya mwanadamu ni kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hii ni changamoto ya kuendelea kujizatiti kikamilifu katika kuuponya Ulimwengu kutokana na uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kuendelea kuujenga Ufalme wa Mungu. Ni ufunuo wa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya pili ya kwaresma mwaka B wa kilitrujia, siku ya kumi na mbili ya majiundo ya kiroho. Ni dominika ya kugeuka sura kwa Yesu na kung’ara kwake kwa utukufu, ishara wazi ya kuwa baada ya dhiki ni faraja, baada ya mateso na kifo kuna ufufuko. Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake. Akawaonesha kwamba, hatima ya maisha ya mwanadamu ni kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hii ni changamoto ya kuendelea kujizatiti kikamilifu katika kuuponya Ulimwengu kutokana na uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kuendelea kuujenga Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Yeye ni Bwana wa historia na viumbe vyote na hatima ya yote haya ni ufalme wa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu Kristo Yesu ni Mwana Mpendwa wa Mungu, waamini wanaalikwa kumsikiliza kwa dhati kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Katika muktadha huo, Mungu anamtambulisha kwa ulimwengu akisema; “Huyu ni mwanangu mteule wangu, msikieni yeye”. Kumsikiliza Yesu na kuyaishi anayotufundisha kunatustahilisha kuuona utukufu wa Mungu. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo (Koleta) anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu, umetuamuru tumsikie Mwanao wa pekee. Upende kutulisha Neno lako ndani yetu. Nasi tukiisha takata, tufurahi kuuona utukufu wako”.  Wimbo wa mwanzo unasisitiza juu ya hamu hii ya kuuona utukufu wa Mungu ukisema; “Moyo wangu umekuambia, Bwana, uso wako nitautafuta. Usinifiche uso wako” (Zab. 27:8-9). Hamu hii ya kuuona utukufu wa Mungu inaifanya imani yetu kwake kukua, kukomaa na kuimarika. Maana imani ni “kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyooneka” (Heb 11,1). Imani hii ni zawadi kutoka kwa Mungu na ni fadhila ya kimungu. Lakini inahitaji utashi wa mwanadamu katika kuipokea, kuikuza, kuiishi na kuirithisha kwa wengine.

Kristo Yesu ndiye Sadaka ya Agano Jipya na la Milele
Kristo Yesu ndiye Sadaka ya Agano Jipya na la Milele

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Mwanzo (Mwa. 22:1-2, 9a, 10-13, 15-18). Katika somo hili Mungu anamjaribu Ibrahimu kwa kumtaka amtoe mwanae wa pekee Isaka kama sadaka ya kuteketezwa. Ibrahimu kwa imani, alisikiliza na kuitii sauti na maagizo ya Mungu akaenda kumtoa mwanae sadaka ya kuteketezwa mbele zake. Mungu kwa kuona Imani ya Ibrahimu anampatia kondoo dume iwe mbadala wa sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanae Isaka. Huu ni utabiri wa Upendo wa Mungu kwa wanadamu wa kumtoa mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo awe fidia ya dhambi zetu. Ibrahimu, kwa imani alitii sauti na maagizo ya Mungu, akapata sifa ya kuwa baba wa imani na kielelezo cha imani kwa Mungu. Yeye alipoanza safari yake ya imani kwa kupokea mwito wa Mungu, aliyasimika maisha yake yote katika imani hiyo. Aliiruhusu na kuifanya imani kuwa jibu la yote katika maisha yake. Ni katika hii imani, Mungu akatoa ahadi hii kwake; “katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako, na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibariki; kwa sababu umetii sauti yangu”. Ni katika muktadha huu, Mzaburi alipotafakari thamani ya imani kwa Mungu na ahadi zake aliimba wimbo huu wa katikati akisema; “Nitaenenda mbele za Bwana, katika nchi za walio hai. Naliamini, kwa maana nitasema, mimi naliteswa sana. Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, mwana na mjakazi wako, umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kushukuru; na kulitangaza jina la Bwana. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, naam, mbele ya watu wake wote. Katika nyua za nyumba ya Bwana, ndani yako, Ee Yerusalemu” (Zab. 116: 9-10, 15-19).

Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima
Kung'ara kwa Kristo Yesu ni kielelezo cha utukufu na ukuu wake wa daima

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 8:31b-34). Katika somo hili, Mtume Paulo anatukumbusha kuwa Kristo aliyetolewa sadaka na Baba ili atukomboe, ndiye anayetuombea na ndiye atakayetuhukumu siku ya mwisho. Lakini hatupaswi kuwa na mashaka na huzuni kuhusu hukumu ya mwisho kwa maana lazima tutaibuka washindi tu, kwa nguvu ya imani. Maana imani ndiyo inamfanya Mungu kuwa upande wetu. Na Mungu akiwa upande wetu hakuna wa kushindana nasi. Nasi tuna uhakika huo, maana kwa Ubatizo Mungu amekuwa upande wetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk. 9:2-9). Sehemu hii ya Injili inasimulia tukio la Yesu kugeuka sura, siku sita baada ya ungamo la Petro kuwa Yesu ni mwana wa Mungu (Mk 8:29) na ni majuma machache tu kabla ya mateso na kifo chake msalabani. Tukio hili la kugeuka sura kwa Yesu linatokea mbele ya mitume watatu; Petro, Yakobo na Yohane ili kutoa ushuhuda na ushahidi kuwa ni tukio la kweli. Hata upande wa Yesu walitokea Musa na Elia, idadi ya watu watatu kwa ushahidi na ushuhuda halali. Tukio hili linatokea juu ya mlima, ishara ya uwepo wa Mungu. Ndiyo maana Musa na Elia walipomaliza kuzungumza na Yesu, wakatoweka, ishara kuwa wakati wao umepita sasa ni zamu ya Yesu ambaye ni utimilifu wa: Unabii na Sheria. Ni katika mzingira haya, wingu lilitokea, likawatia uvuli na sauti ya Mungu ilitoka katika lile wingu ikisema; “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu, msikieni yeye."

Maadhimisho ya Sinodi: Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana
Maadhimisho ya Sinodi: Ujenzi wa utamaduni wa kusikilizana

Kugeuka sura kwa Kristo Yesu ni wito na mwaliko kwetu wa toba na wongofu wa ndani yaani kugeuka kiroho, kutoka katika hali mbaya ya dhambi, kufanya toba ya kweli, na kuanza kuishi maisha ya kitakatifu. Ni mwaliko wa kuacha dhambi na sio kwenda likizo ya dhambi, wala sio kuahirisha kutenda dhambi bali ni kubadili kabisa mwenendo wetu, kuwa watu wapya, kuanza maisha mapya ya kumsikiliza mwana wa Mungu na kuishi kadiri ya amri za Mungu na kukua, kuimarika na kuokomaa katika imani. Kama imani ya Ibrahamu ilivyokuwa na kuimarika kadiri alivyozidi kuingia katika mahusiano na Mungu kwa njia ya Agano na matukio mbalimbali, ikiwemo tukio la kujaribu kumtoa sadaka mwanae Isaka. Kama Mtume Paulo alivyokuza na kuimarisha imani ya waamini wa Rumi kwa kuwakumbusha upendo wa Mungu kwao hata kumtoa mwanae Yesu Kristo ili kwa mateso, kifo na ufufuke wake ukombozi wa mwanadamu ufanyike. Na kama Kristo Yesu alivyoimarisha imani ya wanafunzi wake kwa kugeuka sura mbele yao. Nasi tujitahidi kukua, kukomaa na kuimarika katika imani yetu kwa sala, kufunga na matendo mema. Kumbe, kipindi hiki cha Kwaresima ni kipindi cha kukuza, kuimarisha na kukomaza imani yetu. Mazoezi ya kiroho ambayo Kanisa linayaweka mbele yetu ni mazoezi yanayohitaji imani. Bila kuongozwa na imani mtu hawezi kufunga, hawezi kujikatalia, hawezi kufanya toba, hawezi kusali na hawezi kusukumwa kuwasaidia wahitaji. Pamoja na mazoezi haya ya kiroho kupata msukumo wake kutoka katika imani, mojawapo ya matunda yake pia ni kuiimarisha imani ya anayeyashiriki. Imani iliyoimarika ni ufunguo wa kulielewa Fumbo la Pasaka na thamani ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo katika maisha yetu. Imani iliyoimarika ni nguvu ya kuliishi fumbo hilo la Pasaka.

Kristo Yesu Kugeuka Sura alipania kuwaimarisha Mitime wake katika imani.
Kristo Yesu Kugeuka Sura alipania kuwaimarisha Mitime wake katika imani.

Kumbe lengo kuu la Yesu kugeuka sura mbele ya Mitume wake watatu ni kuwafundisha kuwa utukufu unapatikana katika kuvumilia mateso. Ndiyo maana katika utangulizi wa domenika hii Mama Kanisa anasali akisema; “Yeye aliwaambia mapema wafuasi wake kwamba atauawa; na pale katika mlima mtakatifu aliwaonyesha utukufu wake, akaonyesha kwamba kama ilivyoandikwa katika Torati na Manabii, atapata utukufu wa ufufuko kwa kuteswa. Na katika sala ya kuombea dhabihu Mama Kanisa anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba sadaka hii ifute dhambi zetu na kuwatakasa waamini wako mwili na roho, wapate kuadhimisha sikukuu ya Paska”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali na kutuombea akisema; “Ee Bwana, baada ya kupokea mafumbo yako matakatifu, tunataka kukushukuru kwa maana ingawa tuko bado hapa duniani watushirikisha ya mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu kuu, kufika mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika ya 2 ya Kwaresima
21 February 2024, 15:34