Tafakari Dominika ya Pili Kipindi Cha Kwaresima Mwaka B: Mungu Apewe Kipaumbele Katika Maisha
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizajia na msomaji wa tafakari zetu kutoka radio vatican, karibuni katika tafakari ya Dominika hii ya pili ya kipindi cha Kwaresima cha mwaka B wa Kanisa. Tukiwa katika kipindi hiki cha Kwaresima, leo katika Dominika hii ya pili ya Kwaresima tunaletewa ujumbe wa Mungu unaotualika kuweka kipaumbele chetu katika kuisikia na kuitii sauti ya Mungu inayotudai tubadilike. Tunaalikwa kumpa Mungu nafasi ya kwanza katika kila kitu, maana ni kwa kufanya hivyo tu ndipo tunaweza kuufikia utakatifu na kuungana naye milele. Basi tuombe neema yake itusaidie kuisikia sauti yake na kuitii. Mwanadamu anaweza kulifikia lengo lake la kuwa mtakatifu na kuungana na Mungu muumba wake kwa milele yote ikiwa atakuwa tayari kuweka kipaumbele chake katika kuisikia na kuitii sauti ya Mungu daima; ndio kusema ampe Mungu nafasi ya kwanza katika kila kitu. Mungu awe kwanza, Mungu awe juu ya yote. Hilo ndilo lengo la kwanza kabisa la uwepo wa mwanadamu hapa duniani maana: “Mungu ametuweka duniani tupate kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho tuweze kufika kwake mbinguni. Katika ujumbe wake wa Kwaresima Baba Mtakatifu Francisko anasema “Katika Kwaresima tunapata vigezo vipya vya hukumu na jamii ambayo itaweka njia ambayo haijawahi kufikiwa. Hii inahusisha mapambano: katika Kitabu cha Kutoka na majaribu ya Yesu jangwani yanatuambia wazi juu ya Sauti ya Mungu, ambayo inasema: "Wewe ni Mwanangu mpendwa" (Mk 1:11) Mababa wa Sinodi katika Waraka wao kwa watu wa Mungu mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu wamejikita katika ushirika, Utamaduni wa ujenzi wa ukimya ili kusikilizana na kujielekeza zaidi katika ujenzi wa umoja na ushirika; wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Yesu inayosimikwa katika huduma; Upendo wa Kanisa unabubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Kanisa linahitaji ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote hasa wale wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; ni mwaliko wa kuwasikiliza waamini walei na familia na kuendelea kujikita katika utambuzi wake wa kisinodi; kwa kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kuimarisha mahusiano na mafungamano. Hii ndiyo njia hasa ya Sinodi ambayo Mwenyezi Mungu anaitarajia kutoka kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo. Kristo Yesu ndiye tumaini la pekee kwa waja wake.
UFAFANUZI: Kutoka Somo la Kwanza: (Mwz 22:1-2, 9a, 10-13, 15-18) tumesikia Abrahamu akiambiwa amtolee Mungu sadaka Isaka mwanawe. Hili lilikuwa jaribu kubwa sababu alikuwa mtoto wa ahadi na kwa njia yake Mungu angetimiza Agano lake na Abraham. Kumtoa sadaka lilikuwa jambo gumu lililodai imani. Mzee anakuwa tayari bila kusita na kwa sababu hiyo anaitwa Baba wa imani.. Sadaka ya Isaka ni mfano wa sadaka ya Kristo aliye Mwana pekee wa Mungu Baba kama Isaka. Masomo yetu tuliyoyasikia yanagusia vizuri dhamira hii. Katika somo la kwanza tumesikia juu ya Baba yetu wa imani, Ibrahimu, jinsi Mungu alivyomjaribu kwa kumtaka amtoe sadaka mwanae wa pekee, Isaka. Hii haikuwa mara ya kwanza Mungu kumjaribu Ibrahimu. Kabla, Ibrahimu alikuwa amejaribiwa na Mungu kwa kuambiwa aiache nchi yake, ndugu na jamaa zake na aende katika nchi asiyoijua. Katika yote hayo, Ibrahimu kwa utii na unyenyekevu mkubwa alikubali na kuyatii maagizo ya Mungu, na hivyo akajidhihirisha kuwa mfano bora kabisa wa imani, unyenyekevu na utii. Na kwa sababu hiyo, Mungu akamwahidi Ibrahimu na uzao wake mambo kadha wa kadha. Katika Injili dhamira ya kuisikia na kuitii sauti ya Mungu inajitokeza tena katika nafasi ambayo Yesu na watatu kati ya wafuasi wake yaani, Petro, Yakobo na Yohana, wako juu ya mlima mrefu naye Yesu anageuka sura yake mbele yao. Jambo hili linawavutia wafuasi hawa na hasa Petro ambaye anatamani kubaki huko mlimani. Katika mazingira hayo sauti ya Mungu inasikika ikisema: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye”. Sauti hii ni mwaliko kwa wafuasi hawa kutii kile ambacho Yesu, aliye Neno la Mungu, anawataka kukifanya. Wanapaswa kutii maagizo anayowapatia na kuupokea ukweli anaoufundisha ili wapate kuwa kweli wafuasi wake amini. Utukufu wanaoutamani unawezekana kwa njia ya utii. Mwinjili Marko (9:2-9) anasimulia kugeuka sura Kristo juu ya mlima akiwa na Petro, Yakobo na Yohane. Tofauti na walivyomzoea anaonekana tofauti, mzuri na mtukufu. Mitume wanapomtazama wanamuona aking’ara kama jua, mavazi yake meupe na mwili wake u katika nuru ya pekee, wanastaajabu na kuvutiwa na utukufu ule aliowafunulia kwa muda mfupi ili kuwajulisha hatima ya mateso yake. Ni tukio linalodhihirisha uwepo wa Mungu katika nafsi ya Yesu na mlimani panakuwa mahali pa kutamaniwa daima.
wanatokea Musa na Eliya na kuzungumza na Yesu: Utimilifu wa Sheria na Unabii katika Kristo Yesu. Mtakatifu Luka peke yake anasema walizungumzia kifo cha Yesu (Lk.9:31). Uwepo wa hawa wawakilishi wa Agano la Kale ni ushuhuda kuwa “sheria” na “manabii” vinapata utimilifu katika Kristo Mkombozi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Wakingali bado kupona mshangao uliowafunika inasikika sauti kutoka katika WINGU. Kwa Wayahudi wingu ni ishara ya uwepo wa Mungu. Waliongozwa na wingu jangwani (Kut 13:21), likaifunika hema ya kukutania (Kut 40:34), Musa alipokea amri za Mungu juu ya mlima uliofunikwa na wingu (Kut 24:16-18). Jinsi hii Yesu anaonesha ni utukufu wa namna gani alionao kama Masiha na njia ipi anapaswa kupita yeyote anayekusudia kumfuata. Sauti ile ilimtambulisha Kristo kama Mwana Mpenzi anayepaswa kusikilizwa na wote. Katika Somo la pili, Mtume Paulo anatualika tujiamishe kwake Mungu, na anatuhakikishia kwamba kwa kufanya hivyo tutakuwa ni wenye furaha na amani hata katika magumu na taabu. Maana: “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?” Tunaweza kushinda hofu na mashaka ikiwa tumaini letu liko kwa Mungu mweza wa yote. linadokeza kuwa Mungu akiwapo upande wetu ni nani aliye juu yetu? Alimtoa Mwanae kwa ajili yetu na anaweza kutujalia na mengine, muhimu ni kuwa na imani kwake kama aliyokuwa nayo Abraham. Mpendwa, masomo haya ni chakula cha roho kwetu sisi hususani katika kipindi hiki cha Kwaresima kwani yanasisitiza juu ya jambo msingi sana katika kipindi hiki ambapo tunaalikwa kuacha njia ya dhambi na kuifuata ile ya neema. Kama Ibrahimu alivyokubali kuachia hata kile alichokipenda sana na kukithamini, yaani, mwanae Isaka, na kama vile Petro na wenzake walivyokubali kushuka kutoka mlimani ambako walitamani sana kuendelea kuwapo huko, vivyo hivyo sisi tunaalikwa katika kipindi hiki tukubali kwa unyenyekevu na utii kuachia yale yote ambayo yanaweza kuwa kikwazo katika kujenga mahusiano mazuri kati yetu sisi na Mungu. Sauti ya Mungu inatuita tuiache dhambi, tujibandue na mambo yale yote ambayo tunayapenda sana na kuyapa kipaumbele badala ya yale ya Kimungu, tufanye toba ya kweli, na kuanza maisha ya utakatifu, kama ilivyo dhamira kuu ya kipindi hiki cha Kwaresima.
Nasi katika maisha yetu tunapoonja uwepo wa utukufu wa Mungu na tuvumilie masumbuo ya kila siku TUKIJENGA VIBANDA VITATU. Vibanda vya Mungu ni mfano wa familia bora ambayo kila kitu kipo wazi, wanafamilia wanapanga pamoja mustakabali wa maisha na kuweka vizuri mambo yao. Kibanda kimoja cha baba, kingine cha mama na kingine cha watoto, daima viwe mlimani kwenye utukufu wa Kristo anayeng’ara. Je, kibanda chako (nyumba yako) Ipo mlimani karibu na utukufu wa Mungu? Kama ni hivyo heri yako, wengi nyumba zetu zipo chini ya mlima ambako mitume 9 waliobaki bila Yesu wanahangaika kupunga pepo bubu bila mafanikio (Mk 9:14kk). Tukiisha kufaulu kuvijenga, tushuke chini ya mlima tuwachukue wenzetu tuje nao juu ili nao wafurahie utukufu wa Mungu na kuisikia sauti tukufu ya Mungu Baba… tusifanane na Petro aliyejisahau hata yeye mwenyewe katika vibanda ambavyo angejenga akawasahau na wenzake 9 chini ya mlima.. Nasi hapa na pale tumekuwa na roho ya uchoyo na ubinafsi, wivu, wizi uongo, kinyume na fadhila za ukarimu na upendo. Tuwashukie wenzetu kule chini tukishirikishana vipaji, mali na kuwa wamoja nyakati za raha (harusi, uzazi, kipaimara, mavuno, vinywaji nk) na za taabu (ugonjwa, misiba, njaa nk). Tukitenda hivi Kwaresima yetu itakuwa na manufaa na Kristo atafufuka mioyoni mwetu. Vinginevyo Pasaka itatukuta bila tofauti, leo kama jana, kesho kama leo, “msitu mpya Mbwa mwitu walewale!” Kwenu Wazazi/walezi/viongozi jengeni vibanda 3 ndio utayari wa kuvumilia magumu wanayoyapata katika kutekeleza wajibu za kikristo kama wanandoa/wazazi, kuvumiliana tofauti zao kitabia, kimaweza, kimtazamo, kiafya… na kupendana katika kweli, kutunza na kulea watoto bila kukata tamaa hata wakiwa wakorofi kupindukia. Pamoja nao walimu na walezi, makatekista na wote wenye mapenzi mema wana wajibu wa kuwaandaa vijana katika mengi.. si jambo rahisi, wanatumia nguvu, akili, muda, mali na moyo kuwaunda kimwili, kiroho, kiakili, kimaadili ili wawe watu wa kufaa. Hayo ni mateso walionayo kwa ajili ya Kristo na kwa hayo watafufuka pamoja naye wakati utakapotimia.
Kila mmoja wetu anapewa fursa ya kujichunguza na kutambua ni mambo gani ameyapa nafasi ya kwanza na ambayo yamekuwa ni kikwazo kwa mahusiano yake na Mungu. Je, uko tayari kuyaacha na kuifuata sauti ya Mungu inayokudai uishi kitakatifu? Je, tuko tayari kuacha urafiki mbaya, tuko tayari kuacha uongo, tuko tayari kuacha wizi, tuko tayari kuacha ulevi na ulafi, tuko tayari kuacha kuishi kimada? Hiyo ni baadhi tu ya mifano ya kutusaidia kujichunguza. Kila mmoja wetu anajua wapi amekamatika. Kwa kifupi tujiulize: Je, tuko tayari kuyaacha mambo yote yanayoharibu urafiki kati yetu sisi na Mungu, hata ikitupasa kutoa sadaka kubwa? Wakati huu wa kwaresma tujitahidi kumfuata Kristo katika njia ya msalaba kwa kuishi maisha ya sadaka na kubandukana na kila kinachozuia kujenga vibanda vya Mungu yaani kuandamana na Kristo. Tutekeleze wajibu zetu kwa uaminifu ili jitihada zetu za kumfuata Kristo mteseka zitupatie matunda mazuri ya Kwaresima. Basi tukibidishwa na maneno ya Mtume Paulo anayesema: “Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu?”, tumuweke Mungu upande wetu kwa kusali na kuomba neema yake, nasi tukishirikiana na neema hiyo tuweze kugeuza mienendo ya maisha yetu imwelekee yeye aliye kilele cha maisha yetu na cha mambo yote tufanyayo.