Tafakari Dominika ya Tano Mwaka B wa Kanisa: Imani na Matumaini
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wa Radio Vatican, ni siku ya Bwana dominika ya tano, tunatafakari mapato ya fadhila za matumaini na imani thabiti kwa Mungu ni ushindi dhidi ya mateso na changamoto zetu za maisha kila wakati, Tunapoangalia maisha yetu ya kila siku, tunaona binadamu anasumbuliwa na changamoto nyingi zikiwemo magonjwa na changamoto mbalimbali. Kati ya magonjwa hayo yapo ya kimwili na kiroho. Pamoja na juhudi zetu za kuondokana na magonjwa hayo na magumu mbalimbali, yatupasa kutambua kuwa Kristo ndio mganga wa kweli anayeweza kutuinua kutoka katika magonjwa yetu na magumu yetu, endapo tutakuwa tayari kumwendea Yesu na kumweleza bayana shida zetu, naye atatuinua kwa mkono wake na atatuponya. Ni hamu ya mioyo yetu kujikabidhi mikononi mwa Kristo, tujiachie kwake, tumsikilize katika neno lake, tumwambie ya kwetu.. Leo linachomoza wazo la mateso na shida za mwanadamu, lakini papo hapo inachanua faraja iletwayo na Bwana Yesu kwa wanaomwamini na kumfuata. UFAFANUZI: Katika somo la kwanza tumesikia kuwa, Ayubu anaonesha kukata tamaa kutokana na magonjwa pamoja na majanga mbalimbali yaliyomkuta alipokuwa anajalibiwa na Mungu. Zama zile,magonjwa na majanga mbalimbali yaliyomkuta mtu,yalitafsiriwa kuwa yalitokana na dhambi alizotenda mhusika (Ayu 4:7-9). Na hivyo ugonjwa na majanga yanayomkuta mtu yeyote yalimkumbusha atubu dhambi zake. Ilitegemewa baada ya mtu kutubu dhambi zake angeweza kupata nafuu katika ugonjwa wake au majanga yaliyomkuta (Ayu 8:1-6).
Katika Agano la Kale, waandishi wengi wa Maandiko Matakatifu na watu mbalimbali wenye hekima walionesha jithada zao za kutaka watu wasiunganishe kupatwa magonjwa na majanga mbalimbali na dhambi alizotenda mtu. Mwandishi wa Kitabu cha Ayubu ni mmojawapo aliyetoa mchango wake. Kwamba, Ayubu alikuwa mtu mwema lakini alipatwa na mateso. Wazo hili halikuingia vichwani mwa Wayahudi, na hivyo mpaka Yesu anazaliwa aliukuta mwono huohuo. Yesu naye katika kipindi chake aliwafundisha watu wasiunganishe magonjwa na matatizo mbalimbali na dhambi alizotenda mtu. Wanafunzi wa Yesu,walimuuliza, ni nani aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata akazaliwa kipofu? Yesu alijibu, alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake (Yoh 9:2). Ayubu anawakilisha wote walio katika dhiki na mateso, anaonekana kuelemewa na kusema, “nimepewa miezi ya ubatili iwe fungu langu, nami nimeandikiwa masiku yenye kuchokesha, usiku huwa mrefu, siku zapita bila matumaini na jicho langu halitaona mema tena!” naye Mt. Marko katika Injili anaweka bayana namna mwanadamu anavyoishi kwa mateso akiandamwa na mizigo... Mama mkwe wa Petro anaugua, jioni Yesu analetewa waliokuwa hawawezi, maradhi yanawanyenyekesha, pepo wanawababaisha, hofu imetanda pande zote, kila sehemu watu wanahitaji msaada.
Je, mateso na mahangaiko yetu yana maana yoyote? tunapoandamwa na shida tunamwona Mungu au tunatafuta nafuu mahali pengine? Lakini MATESO NI NINI? Mateso ni mambo ya kumwadhibu au kumtaabisha mtu/mnyama, madhila na wakati mwingine ni maonevu tu. Mateso ni tabu, hali ya kutokuwa na raha, masumbufu, adha, shida, mashaka, dhiki, udhia na kero... Kuna aina mbili za mateso; mosi ni mateso yanayotokana na maumbile ya dunia mfano mvua nyingi na mafuriko, ukame, matetemeko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko na wadudu waharibifu kama nzige, mbu, virusi, bacteria, minyoo nk... Aina ya pili ni mateso ya kimaadili yanayoletwa na matendo yetu mfano vita, mauuaji, mahusiano mabaya, siasa za kidikteta, tabia zisizofaa nk. Mateso ni changamoto kwa imani yetu, hata watu wenye imani hujikuta katika majaribu wawapo katika mateso. Wakana Mungu hutumia uwepo wa mateso na majanga duniani kusema hakuna Mungu, angekuwepo asingeruhusu majanga na mateso tena kwa watu wanaomcha, wasio na hatia, wanateseka wanaosali na wenye imani wakati watu jeuri wanastawi kama majani ya kondeni. Kwa nini? Mungu amesahau kuwa na huruma? haoni? amesinzia? haoni uchungu? kwa nini tunateseka? Kuna nafasi fulani katika maisha Mungu anaruhusu tuteseke. Hii ni kwa sababu “utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno, huruma zake hazichunguziki na njia zake hazieleweki” (Rum 11:33). Mateso yetu yanatufanya tukubalike, kukubalika kwetu kunatupa matumaini, na matumaini yetu hayatatudanganya. Kwa njia ya mateso na majaribu Mungu anatujalia mambo mazuri na makuu zaidi. Yosefu mwana wa Yakobo aliwaambia kaka zake “kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa kama ilivyo leo, basi sasa msiogope” (Mwz 50:20).
Katika Somo la Pili (1Kor 9: 16-19,22-23, Mtume Paulo anatuasa sisi sote tunaomfuata Yesu kuwa, kushuhudia na kutangaza Injili ni kazi yetu. Ni kazi yenye thawabu ikitendwa kwa hiari.Na yatupasa kwenda kuhubiri mahali pote,kwa watu wa kila rangi na makabila yote. Hivyo katika utume wetu, tusibaki mijini tu,kwa kuwa kuna miundo mbinu mizuri, kwa watu wenye uwezo kiuchumi na mali , bali twende mpaka vijijini, kukutana na wenye hali duni, fukara wa mahitaji ya kimwili na kiroho hapa Paulo anakazia dhana ya kimisionari amabyo alifanya katika utume wake, kama wamisionari wa kwanza walivyofanya nasi tufanye hiyo. Katika Injili, dominika iliyopita,Yesu alimponya mtu aliyepagawa na pepo kwa nguvu ya Neno lake. Uponyaji wa leo ni wa ndani zaidi na wa kirafiki. Yesu anatembelea nyumbani kwa Simoni mmoja kati ya wanafunzi wake wanne wa mwanzo, na huko anamkuta mgonjwa. Yesu anamwinua na mara homa inamtoka. Ni kwa kuinuliwa tu na Yesu mara anapona. Katika uponyaji huu wa mkwewe Simoni, mamlaka ya Yesu yameoneshwa katika kueleza namna alivyomtendea mgonjwa, akamshika mkono akamwinua na ile homa ikamwacha. Kuna ishara kubwa katika mtindo huu wa kuponya. Mgonjwa anainuliwa kutoka kitandani alipolala. Katika ulimwengu uliotazama ugonjwa kama athali za kukandamizwa na shetani, kuinuliwa kuna maana ya kuondolewa kutoka mikononni mwa shetani na kuwekwa mikononi mwa Yesu, kufunguliwa kongwa la shetani na kupewa uhuru wa kujimudu. Mateso yanatufanya tutambue udogo, udhaifu na unyonge wetu na hivi kujisogeza karibu zaidi na Mungu. Tunapoweka tumaini letu kwa Mungu tunapata heri iliyo kamili siku zote kwani tunajipatia uhakika kuwa yupo nasi katika nyakati hizo ngumu za maisha.
Mateso yana “lengo la kutuinua na kutuunganisha na mbingu sisi wenyewe pamoja na wenzetu.” Hii ni siri kubwa ya Mungu. Mateso ya namna hii ndiyo yale ambayo Mtakatifu Ignasi wa Antiokia anayazungumzia “Endapo tunayapokea kwa moyo wa unyenyekevu na imani, basi yanageuka kuwa Sakramenti [karama] kwa ajili ya utakaso wetu na wa ndugu zetu ambao Mungu amewaridhia. Kinachotakiwa daima ni kujiweka mikononi mwa Mungu; ili wakati wa teso ujapo, shetani asitumie maumivu yako kukufanya ukamwasi Mungu wa kweli na kumkumbatia yeye.” Yesu mwenyewe alipata uchungu alipoambiwa Yohane Mbatizaji ameuawa akaenda faraghani pasipokuwa na watu, bila shaka kumlilia Mtangulizi wake huyo hodari (Mt 14:13), alipata mateso na kulia kaburini kwa Lazaro (Yn 11:35), na kutoka jasho la damu Gethsemane akasema “roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa” na akasali “Baba, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke…” (Mt 26:38-39).. Nabii Isaya aliongea habari za Yesu akasema “alidharauliwa na kukataliwa na watu; mtu wa huzuni nyingi ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, alidharauliwa wala hatukumuhesabu kuwa kitu..”(Isa 53:3). Mama huyu katika Injili ya leo anatuwakilisha sisi sote tunaohitaji kuinuliwa na Bwana Yesu kutoka katika magumu na udhaifu mbalimbali.Familia nyingi leo zimesambalatika, na malezi ya watoto yamekuwa magumu,mfano ni uwepo wa watoto wa mitaani.Imani katika Mungu imeshuka, maadili yako chini, ugomvi na vita vipo kila mahali. Tumwombe Yesu atuinue kama alivyomuinua mama mkwe wa Simoni nasi tutakuwa salama.
Jamii inateseka udhanifu mbaya na hukumu zisizostahili, Mandishi wa mashairi kutoka huko Tanzania, katika kitabu chake kiitwacho Diwani ya Mloka katika anaandika “sione watu kulima ukadhani wanashiba, sione penye huruma ukahisi pana tiba, sione panapochoma, ukadhani pana mwiba, kila unachotazama usione ukadhani” (uk. 14-15). Serikali ikichoka majukumu yake watu huteseka. Wafanyakazi wakimchoka mkuu wao hufuata mateso na dhiki. Mapadre wakiwachoka waamini au waamini wakiwachoka mapadre huingia mateso. Watawa wakimchoka mkuu wa shirika au mkuu akiwachoka watawa wake, umisionari huzorota na wito hugeuka mzigo, Baba anapomchoka mama, mama anapomchoka baba, wazazi wanapochokana na watoto hupelekea mateso na dhiki. Walimu na wanafunzi wakafika kuchokana basi kila kitu huwa ni shida. Mwisho tunaweza kuteswa kisaikolojia kwa sababu kuna watu wanatutishia maisha, hawa hawajiamini katika shughuli zao za kisiasa, katika biashara zao, katika ndoa zao, katika mambo yao mbalimbali na hivi wanajihami kwa kuwatishia wenzao. Leo Neno la Mungu linatupatia dawa ya kutuponya na haya yote kusudi tuteseke kwa imani tukijua thamani ya mateso yetu na wakati huohuo tukijitahidi kutokuwa sababu ya mateso ya wenzetu. Kwa vile kila mtu ana mateso yake basi kila mmoja ajitahidi kuondoa tofauti zote na kuwa sababu ya faraja ya mwenzie. Faraja ipo katika somo II ambapo Mt. Paulo anasema Injili ni lazima ihubiriwe tena pasi masharti wala gharama, “ijapokuwa naihubiri Injili sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti, tena ole wangu nisipoihubiri Injili”(1Kor 9:16) Basi na tuhubiriane Injili ya faraja, tupeane maneno ya kutia moyo ili walau kupoza machungu ya dhiki zinazotuelemea, Injili hiyo ni Habari Njema ya Kristo Mponyaji wetu “aliyechukua masikitiko yetu, amejitwika huzuni zetu” (Isa 53:3).
Mpendwa, Kristo Bwana na awe ngao yako akutetee “Je, mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyae, hata asimuhurumie mwana wa tumbo lake? naam, hawa waweza kusahau tena wapo wengi au mpo wengi yawezekana hata wewe unayenisikia, lakini mimi sitakusahau wewe” (Isa 49:15). Amani yake idumu moyoni mwako uwapo katika mateso na dhiki kama Ayubu.. ndio, twayaweza mambo yote katika yeye atutiaye nguvu (Filp 4:13) Kwa jitihada zetu wenyewe hatuwezi kujinasua kutoka katika magojwa yetu ya kimwili na kiroho. Tunamhitaji Bwana wetu Yesu Kristo aliye mganga wa roho zetu na miili yetu, atuinue kutoka udhaifu wetu, atujalie nguvu ya kupokea magumu kwa imani. Tujue kuwa hata katika mateso yetu Mungu yupo pamoja nasi. Kwa upande wetu yatupasa kuwa watu wa sala,si tu wakati wa shida bali wakati wote (sala isichukuliwe kama ambulance,yaani inahitajika wakati wa shida tu.). Katika Jumapili hii tumwombe Bwana wetu Yesu Kristo atuinue katika magumu yetu,ili baada ya mahangaiko yetu ya hapa duniani,tupate nafasi ya kufurahi naye Mbinguni. Amina.