Tafuta

Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyowafukuza wanafanya biashara Hekaluni. Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyowafukuza wanafanya biashara Hekaluni.  

Tafakari Dominika ya Tatu Kwaresima Mwaka B: Yesu Ni Hekalu Jipya Na La Milele

“Nitakapotakaswa kati yenu, nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote; nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana” (Ez. 36:23-26). Ni utakaso wa kiroho tunaoupata kwa kufunga na kusali. Waisraeli wanakumbuka matendo makuu ya Mungu katika maisha. Ugumu na changamoto ya kulielewa Fumbo la Mateso, kifo na ufufuko kwa wafu, na hatimaye, Kristo Yesu anawafukuza wafanya biashara Hekaluni

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tatu ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka B wa kilitrujia katika kanisa. Ni siku ya kumi na tisa ya kujitakatifu kama wimbo wa mwanzo kutoka kitabu cha Nabii Ezekieli unavyosema; “Nitakapotakaswa kati yenu, nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote; nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, asema Bwana” (Ez. 36:23-26). Ni utakaso wa kiroho tunaoupata kwa kufunga na kusali ndiyo maana katika sala ya mwanzo (Koleta), Mama Kanisa anatuombea hivi; “Ee Mungu, wewe ndiwe asili ya rehema zote na mema yote. Umeonyesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali na kuwapa maskini. Utusikilize kwa wema sisi tunaokiri unyonge wetu, ili tunaponyenyekea moyoni, utuinue daima kwa huruma yako”. Ni katika tumaini hili mzaburi katika wimbo wa mwanzo anaimba akisema; “Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na kunifadhili, maana, mimi ni mkiwa na mteswa” (Zab. 25:15-16). Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut. 20:1-17). Somo hili ni kama ufupisho wa samulizi ya makuu ya Mungu aliyowatendea Waisraeli; Jinsi alivyowakomboa kutoka utumwani Misri, akafanya nao Agano na akawapa amri kumi ziwe mwongozo katika maisha yao. Amri hizi ni mwongozo wa maisha ya mwanadamu wote. Nazo zimejikita katika kujenga uhusiano mwema na Mungu na jirani. Kila azishikaye amri hizi anapata amani na heri katika maisha yake. Ndiyo maana mzaburi alipozitafakari aliimba wimbo huu wa katikati akisema; “Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi, ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia mjinga hekima. Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo na amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru.  Kicho cha Bwana ni kitakatifu, kinadumu milele. Hukumu za Bwana ni za kweli, zina haki kabisa. Ni za kutamanika kuliko dhahabu, kuliko wingi wa dhahabu safi. Nazo ni tamu kuliko asali, kuliko sega la asali” (Zab. 19: 7-10).

Kanisa ni Nyumba ya Sala
Kanisa ni Nyumba ya Sala

Kwa kufanya nao Agano Mungu alionesha mapendo makubwa kwa Taifa hii na taratibu alifunua mpango wake wa kuwakomboa wanadamu wote kutoka katika utumwa wa dhambi. Lakini wana wa Israeli kila mara walivunja Agano walilofanya na Mungu kwa kuabudu miungu mingine. Mungu aliwaadhibu kwa kuyaruhusu mataifa mengine kuwavamia na kuwachukua mateka. Hatimaye, Mungu aliaamua kufanya nasi Agano jipya na la milele kwa njia ya Mwanae Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 1:22-25). Somo hili linatueleza namna watu wa mataifa mbalimbali walivyopata ugumu katika kulielewa na kuliamini fumbo la ukombozi kwa njia ya msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Wayahudi walidhani Kristo alilaaniwa na Mungu kwa kufa msalabani. Maana kitabu cha Kumbukumbu la Torati kinasema hivi: “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utazikwa siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu, asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Nao Wayunani wanaofuata hoja za kiakili, waliona ni upuuzi na upumbavu. Lakini kwetu sisi, msalaba ni njia ya wokovu wetu na bendera ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Kwani Kristo kwetu ni nguvu na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.

Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.
Msalaba ni kielelezo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu.

Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 2:13-25). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyowafukuza wanafanya biashara Hekaluni. Lakini kwanini watu walifanya biashara hekaluni? Torati iliwaamuru Wayahudi wanaume kwenda Yerusalemu kuhiji katika sikukuu muhimu. Na moja ya tendo muhimu la kuhiji lilikuwa kutoa sadaka za wanyama wa kuteketezwa kama kondoo, ng’ombe au njiwa, kila mmoja kadiri ya uwezo wake. Sheria zilisema hivi; “Wanaume wenu wote lazima wajitokeze mara tatu kwa mwaka mbele za Bwana Mungu wenu mahali atakapopachagua: kwa ajili ya Sikukuu ya Mikate isiyotiwa chachu, Sikukuu ya Majuma na Sikukuu ya Vibanda. Hakuna mtu atakayejitokeza mbele ya Bwana mikono mitupu: Kila mmoja wenu ni lazima alete zawadi kulingana na jinsi ambavyo Bwana Mungu wenu alivyowabariki” (Kumb. 16:16; Walawi 5:7), pia walipaswa kulipa kodi au zaka (Kut. 30:13). Kwa kuwa watu walitoka mbali hawakuweza kusafirisha wanyama kwa ajili ya kutolea sadaka. Kumbe kulikuwa na watu wanaouza wanyama wanaostahili kwa sadaka hekaluni na wengine walikuwa wakivunja au kubadilisha fedha kutoka sarafu ya kirumi kwenda sarafu ya kiyahudi. Hii ni kwa sababu sarafu halali ya kutolea sadaka hekaluni ilikuwa ni sarafu ya Kiyahudi tu. Kadiri ya sheria, sarafu ya kiruma ilikatazwa kutolewa kama sadaka kwa sababu ilikuwa na chapa ya mtawala wa Kirumi. Lakini kwa vile walikuwa chini ya utawala wa kirumi, sarafu yake ilitumika katika biashara na maisha ya kawaida. Hivyo ilibidi kuibadilisha na kupata sarafu ya kiyahudi ili kutoa sadaka. Kwa hiyo baadhi ya wayahudi walifanya biashara hizi hekaluni. Kumbe, biashara zilifanyika katika sehemu ya kwanza ya Hekalu iliyokuwa kwa ajili ya watu wa Mataifa.

Kanisa ni nyumba ya sala
Kanisa ni nyumba ya sala

Yesu alipoingia Hekaluni kusali, alikutana na hali na mazingira haya. Ndipo akatengeneza kikoto cha kambaa, akawatoa wote hekaluni, akapindua meza za wavunja fedha na kuwaambia; “Msiifanya nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya Biashara. Nyumba hii ni nyumba ya sala.” Ukatimia utabiri wa nabii Zakaria usemao; “Katika siku hiyo hatakuwepo tena mfanyabiashara katika nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu” (Zak 14:21-22). Wayahudi walipotaka kudhibitisha nguvu na uweza wake, walimuuliza; “Ni kwa mamlaka gani na ni ishara ipi utakayotuonyesha kwamba unafanya haya”? Yesu aliwajibu; “Livunjeni hekalu hili na baada ya siku tatu nitalisimamisha” (Yn 2:21). Jibu hili hawakulielewa. Wao walifikiria Hekalu lililojengwa na Herode Mkuu nalo likachukua nafasi ya sanduku la Agano likiashiria uwepo wa Mungu. Hivyo Wayahudi waliamini kuwa Mungu anapatikana katika Hekalu la Yerusalemu tu, ndiyo maana walipaswa kwenda huko kusali na kutolea dhabihu. Lakini Yesu anaongelea Hekalu jipya, ambapo dhabihu safi zitatolewa na kukubaliwa. Ndiyo maana alimwambia mwanamke msamaria; “Saa inakuja, ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu, ila wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli” (Yn 4:21-24). Hekalu hili jipya ndio mwili wake Kristo. “Maana ukamilifu wote wa Mungu umo ndani ya Kristo katika umbile la mwili wa kibinadamu” (Kol. 2:9). Hu uni ufunuo wa fumbo la umwilisho la Mungu kuchukua mwili na kuja kukaa nasi. Baada ya mateso, kifo, ufufuko na kupaa kwake mbingu. Yesu sasa yupo katikati yetu katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Kanisa ni nyumba ya sala.
Kanisa ni nyumba ya sala.

Kwa Ubatizo sisi nasi tumekuwa hekalu la Roho Mtakatifu. Kila mbatizwa ni sehemu ya hekalu la Mungu. Ndani ya kila nafsi ya mbatizwa Mungu anaabudiwa katika Roho na Kweli. Ubani, manemane na dhabihu ya kweli katika hekalu hili jipya ni matendo ya upendo kwa wahitaji; maskini, yatima, wajane, wafungwa, wagonjwa, walio uchi na watu wote ambao utu wao unadhalilishwa kwa sababu ya dhambi. Ndiyo maana katika kipindi hiki cha kwaresma, Mama Kanisa anatuhimiza akirudia tena na tena kufanya bidii katika kusali, kufunga, kufanya toba na kutenda matendo ya huruma. Ni katika kufanya hivyo, tunastahilishwa kuushiriki uzima wa milele tukingali hapa duniani kama anavyotuombea katika sala baada ya Komunyo akisema; “Tumepokea amana ya fumbo la mbinguni. Nasi tumeshiba mkate wa mbinguni tukingali bado hapa duniani. Tunakuomba kwa unyenyekevu, Ee Bwana, hayo tuliyopokea katika fumbo tuyatimize kwa matendo.” Tukifanya hivi tunakuwa na heri mbinguni na duniani. Tumsifu Yesu Kristo. 

Dominika 3 Kwaresima
28 February 2024, 14:50