Tafakari Siku ya 32 ya Wagonjwa Ulimwenguni: Upweke
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 6 ya mwaka B wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya dominika hii ni mwendeleo wa tafakari ya fumbo la mateso na uwepo wa magonjwa katika maisha yetu. Tumaini na faraja yetu ni hii tukiwa waaminifu kwa Mungu aliye mwamba na nguvu yetu tutaponywa na taabu zote. Ndivyo unavyoimba wimbo wa mwanzo ukisema; “Uwe kwangu mwamba wa nguvu, nyumba yenye maboma ya kuniokoa. Ndiwe genge langu na ngome yangu; kwa ajili ya jina lako uniongoze, unichunge” (Zab. 31:2-4). Mama Kanisa anaadhimisha pia Siku ya 32 ya Wagonjwa Ulimwenguni inayoadhimishwa tarehe 11 Februari 2024, Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Lourdes. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya unanogeshwa na kauli mbiu “Si vizuri kwamba mwanadamu awe peke yake. Uponyaji wa wagonjwa katika kuponya mahusiano.” Baba Mtakatifu anaangalia vita kama gonjwa kubwa na la kutisha, uzee na upweke. Kumbe, kuna haja ya kudumisha ukaribu wa huruma na upendo ili kutibu majeraha ya upweke na kutengwa. Wagonjwa walioko hatarini pamoja na maskini ni kiini cha maisha na utume wa Mama Kanisa. Tunakumbushwa kuwa gonjwa baya kuliko yote ni la kiroho linalosababishwa na dhambi maana linatutenga na Mungu na ndugu zetu na hivyo kutufanya tuwe wapweke na upweke ndicho kitu cha kwanza kabisa Mungu kukiita “si kizuri.” “Si vizuri huyu mwanaume kuwa peke yake. Nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwanzo 2:18). Ndiyo maana mama kanisa katika sala ya mwanzo anatuombe tuwe karibu zaidi na Mungu akisema; “Ee Mungu, wewe wasema kuwa umo miongoni mwao walio wema na wanyofu. Utujalie kwa neema yako tuishi kitakatifu kusudi upende kukaa ndani yetu.”
Somo la kwanza ni la kitabu cha mambo ya Walawi (Walawi 13:1-2, 44-46). Somo hili ni sehemu ya sheria zilizowahusu wagonjwa wa ukoma katika Agano la Kale. Kadiri ya wayahudi ukoma ulijumlisha magonjwa yote ya ngozi (2Fal. 5:27). Nyakati hizo mtu mwenye ukoma alionekana ni mdhambi na najisi, hivyo alitengwa na jamii. Chanzo cha ujongwa huu wa ukoma iliaminika kuwa ni dhambi. Hivyo wakoma walichukuliwa kuwa ni watu wadhambi na huo ugonjwa ulikuwa ni ishara ya adhabu na laana kutoka kwa Mungu na hivyo kuhalalisha kutengwa kwao maana kama Mungu alikwisha kuwaadhibu, binadamu hakuwa na budi kufanya vivyo hivyo. Kwa hiyo yeyote aliyeathirika alipelekwa kwa kuhani ili kuchunguzwa. Kama kuhani akitangaza kwamba mtu huyu ana ukoma au ana dalili za ukoma, basi mtu huyo alitengwa na jamii, na kufukuzwa kutoka katika nchi ya ahadi. Wakoma walipaswa kuvaa nguo zilizoraruliwa, hawakuruhusiwa kuchana nywele zao na kila walipopita karibu na maeneo ya watu walipaswa kupiga kelele kwa sauti kubwa wakisema “ni najisi, ni najisi” ili wasio najisi wampishe wasije wakanajisika. Kwa aliyebahatika kupona, alipaswa kujionyesha kwa kuhani mkuu, achukungwe ili kuthibitisha kupona kwake na kutangazwa kuwa amepona na baada ya kutakaswa, alipaswa kutoa sadaka ya shukrani na kuruhusiwa kuchangamana na watu wengine. Hizi zilikuwa ni taratibu za afya za wakati ule, ili kuzuia ugonjwa usienee kama ilivyo nyakati zetu kuwa ukitokea ugonjwa kuambukizi, waathirika wanatengwa na kuwaweka karantini. Lakini nyakati hizo sheria hizi ziliongeza mateso na mahangaiko makubwa mno maana wagonjwa hawa walijiona kuwa ni watu waliolaaniwa na Mungu na kutengwa na jamii. Mbaya zaidi ni kwamba hata wao wenyewe, walijinyanyapaa kwa kujiita najisi. Hivyo waliteseka sio tu kwa maumivu ya ugonjwa wenyewe lakini pia kwa kukosa mahitaji muhimu kama chakula, maji, makazi au msaada wowote wa kibinadamu. Ni Mungu peke yake ndiye alikuwa na uwezo wa kumponya na kumtakasa mkoma kama ishara ya kumsamehewa dhambi zake kama angetubu na kuomba msamaha. Ndiyo maana katika zaburi ya wimbo wa katikati tunaimba hivi; “Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake. Heri Bwana asiyemhesabia upotovu, ambaye rohoni mwake hamna hila. Ndiwe sitara yangu, utanihifadhi na mateso, utanizungusha nyimbo za wokovu. Nalikujulisha dhambi yangu, wala sikuuficha upotovu wangu. Nalisema, nitayakiri maasi yangu kwa Bwana, nawe ukanisamehe upotovu wa dhambi yangu. Msifuni Bwana; shangilieni, enyi wenye haki. Pigeni vigelegele vya furaha, ninyi nyote mlio wanyofu wa moyo” (Zab. 31:1-2, 5, 7, 11).
Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 10:31-33, 11:1). Katika somo hili mtume Paulo anatufundisha kuwa katika kufanya jambo lolote tufuate kutimiza mapenzi ya Mungu na tuwe na busara ya kuepa makwazo kwa wenzetu. Ni lazima katika maisha yetu, tuungane na Kristo na kufanya mambo yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Paulo anatuhimiza kumwiga yeye jinsi alivyoishi katika kumfuata Kristo. Injili iwe ni dira ya maisha yetu, tuwe mfano mzuri wa maisha ya Kikristo kwa watu wengine. Imani yetu idhihirike kwa matendo mema yanayoongozwa na upendo. Injili ni kama ilivyoandikwa na Marko (Mk 1:40-45). Sehemu hii ya Injili inasimulia jinsi Yesu alivyomponya mkoma ishara ya kuuangamiza utawala wa shetani na kuusimika ufalme wa Mungu. Ni wazi wapo manabii walioheshimika katika Agano la Kale na waliweza kuwaponya wakoma. Musa alimuombea dada yake Miriamu, Mungu akamtakasa na ugonjwa wa ukoma (Hes 2) na Elisha kwa Neno la Mungu alimtakasa Naamani kutoka ugonjwa wa ukoma (2Waf 5). Yesu kumponya mkoma ni kudhihirisha ukuu wake wa kinabii na kimasiha. Yeye ni mkuu kuliko manabii wa kale. Shida haijui sheria wala utaratibu. Mkoma akiwa katika mahangaiko ya kutafuta kutakaswa alivunja sheria iliyomkataza kwenda karibu na watu. Yeye alimkaribia Yesu akapiga magoti na kumuomba amtakase. Yesu alimwonea huruma, akamsogelea, akanyoosha mkono wake, akamgusa na kumtakasa. Kadiri ya sheria Yesu kumsogolea na kumgusa mkoma tayari naye alijitia unajisi kadiri ya sheria. Lakini hii inatufundisha kuwa huruma ya Mungu haina mipaka, haifungwi na sheria za kibinadamu. Hata hivyo, baada ya kumponya alimuagiza akajioneshe kwa kuhani ili apate kutangazwa kutakasika kwake na kupewa ruhusa ya kuchangamana na watu wengine. Zaidi sana alimtaka aende kutoa sadaka ya shukrani kwa Mungu na kumuonya asitangaze habari hizi kwa yeyote. Lakini mkoma huyu hakutii agizo la Yesu la kutokutangaza aliyemponya. Bali aliendelea kumshukuru Mungu kwa kutangaza habari za Yesu.
Hali hii ilimfanya Yesu kujitenga na jamii kama mkoma. Ndiyo kusema Yesu anaonja adha waliyokuwa nayo wakoma. Lakini wagonjwa na wadhambi waliendelea kumfuata Yesu ili awatakase na kuwaponya. Kama ukoma unavyoharibu sura na mwonekano wa kimwili. Ndivyo dhambi inavyoharibu sura na mwonekano wa kiroho. Tunapotenda dhambi tunapoteza sura na mfano wa Mungu ndani mwetu. Kama vile ukoma ulivyowatengwa watu na jamii, ndivyo dhambi inavyotutenga na Mungu na jamii ya waamini. Adamu na Eva, baada ya kutenda dhambi walijenga na Mungu wakijaribu kujificha (Mwa 3:8). Kaini alipomuua ndugu yake Abeli alimwambia Mungu “Mimi nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani, hata ikiwa kila anionaye ataniua (Mwa 4:14). Yona alipokaidi mpango wa Mungu wa kwenda Ninawi kuhubiri habari za toba na wongofu, alikimbilia Tarshishi apate kujiepusha na uso wa Bwana (Yona 1:3). Mwana mpotevu, alitoroka akajitenga na familia yake akaenda kuishi mbali (Lk 15:13). Tukiwa mbali na Mungu chanzo cha wema wote, tunageukia maovu. Tukiwa mbali na Mungu chanzo cha mwanga katika njia ya uzima, tunatembea katika uvuli wa mauti. Tukiwa mbali na Mungu sababu ya furaha ya kweli, tunajawa na huzuni moyoni. Tukiwa mbali na Mungu uhai wetu tunanyemelea na uvuli wa mauti. Hivi vyote ni kutuonyesha kuwa kuishi katika hali ya dhambi ni chukizo kwa Mungu, kwa Kanisa, kwa jamii, jumuiya na familia. Basi kama mkoma nasi tunahitaji kutakaswa katika sakramenti ya utakaso na uponyaji, sakramenti ya upatanisho, msamaha na ondoleo la dhambi. Tuko mbioni kuanza kipindi cha Kwaresima kwa jumatano ya majivu. Tujitafiti nafsi zetu ili tuweze kujirekebisha tulipojitenga na Mungu, na wenzetu, na familia zetu.
Tuuvae ujasiri katika imani kama wa mkoma, tumwendee Yesu kwa moyo wa majuto na kumwomba atutakase na kutuponya na udhaifu wetu na kutufanya wapya tena. Ndivyo anavyotuombea mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu akisema; “Ee Bwana, tunakuomba kafara hii itutakase na kutufanya wapya; tena ituletee tuzo la milele sisi tunaotimiza mapenzi yako”. Tukiyazingatia haya tutapata heri mbinguni kama antifona ya wimbo wa komunyo inavyotuambia; “Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn. 3:16). Na Mama kanisa anahitimisha maadhimisha ya dominika hii akituombea hivi katika sala baada ya komunyo; “Ee Bwana, tumeshiba chakula cha mbinguni. Tunaomba utujalie tutamani sikuzote chakula hicho kinachotupa uzima wa kweli”. Nawatakieni maandalizi mema ya kuanza kipindi kwa cha kwaresima tutakachokianza kwa Jumatano ya majivu, kipindi cha toba na utakaso kwa kufunga, kusali na kutenda matendo mema ya huruma kwa bidii zaidi ili kujichotea neema za uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.