Tanzania,Ask.Mwijage:Kipindi cha Kwaresima ni kuzama katika mateso,kifo&ufufuko wa Bwana
Patrick Tibanga- Bukoba na Angella Rwezaula-Vatican.
Hivi karibuni tumeanza kipindi cha Kwaresima, kipindi kikuu ambacho Mama Kanisa anakiweka kwa ajili ya kujitafiti katika kufanya kukumbuka ya ile njia aliyopitia ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunaalikwa kusali sala ambayo ni njia inayofamfanya mtu aweze kujiweka katika usikivu na muungano na Mungu. Mungu anataka kuzungumza na mwanadamu kwenye jangwa lake la ndani, na utupu wake na ili mwadamu huyo apokee ujumbe wa hekima. Sala zinaweza kufanyika kwa njia ya maneno, lakini pia kwa njia ukimya, ambapo ni kutafuta namna ya kuruhusu Mungu aweze kuzungumza ndani ya nafsi ya binadamu. N a wakati huo huo sala hiyo inatendeka kwa ishara na tabia, lakini hasa kwa matokeo na tafakari juu ya neno la Mungu ambalo Aliye juu amekuwa akirudia wa karne nyingi na hata leo hii anaendelea kutangaza kwetu sisi ujumbe wa kweli.
Ndugu msikilizaji/Msomaji ni katika fursa hii ya kuanza kipindi kikuu cha toba ambapo Wakristo wengi na wenye mapenzi mema walitakiwa kujishikamanisha na Kristo kwa kufanya toba ya kweli, kufanya matendo ya huruma na huduma kwa wahitaji ili kuurithi Ufalme wa Mungu na kujikatalia vilema vingi vya kidunia vikiwemo vile vya wivu na masengenyo. Wito huo ulitolewa hivi karibuni mnamo tarehe 14 Februari 2024 na Askofu Jovitus Mwijage wa Jimbo Katoliki la Bukoba, katika Misa Takatifu ya Jumatano ya majivu misa iliyoadhimishwa katika Kanisa kuu lake la Bukoba Tanzania. Katika tafakari yake Askofu Mwijage ikiwa ni Kwaresima yake ya kwanza inamkuta kama Askofu mpya wa Jimbo la Bukoba alisema kwamba hali ya mwanadamu ni hali ya udhaifu licha ya kubatizwa, kila mara tunatenda dhambi na kuanguka na kuutupa msalaba wa Kristo na kutengana na Mungu kwa njia ya dhambi, hivyo Mungu humdai mwanadamu toba na kufanya malipizi ya dhambi alizozitenda na pia aliwahimiza waamini kumrudia Mungu kila mara na kuongeza kuwa Kipindi cha Kwaresima Mwanandamu anazamishwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Bwana.
“Kipindi hiki kinatuandaa kuadhimisha fumbo la Pasaka vizuri ambamo tunazamishwa katika mateso, kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na hali yetu ya kibinadamu ni hali ya udhaifu, ingawa tumebatizwa na tukaahidi kumfuata Kristo na kumkataa shetani, kila mara tunajikuta tunatenda dhambi tena na tena, tunatakiwa kumfuata Kristo na kuubeba msalaba wake hivyo kwa kutenda dhambi tunatengana na Mungu” Alisema Askofu Mwijage.
Askofu Mwijage aidha aliwahimiza Wakristo kusali zaidi na kufanya matendo ya huruma na huduma kwa wahitaji bila kuwadharau au kuwatangaza kwa wengine ili kupata tuzo walizowekewa na Mungu. “Katika Kipindi hiki tunaalikwa kusali zaidi kusikiliza neno na kulisoma neno la Mungu, na huu ndio msisitizo uliotolewa hata na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) hivyo inabidi tutafute njia ya kuelewa ujumbe huo. Pia tunaalikwa kutenda matendo ya Huruma kwa wenzetu wahitaji zaidi na tunapofanya hivyo tusijitangaze au kuwadharau kwamba mimi ndiye niliyemsaidia au nisingekuwa mimi huyu asingekuwa na hiki kitu hapana hizo tuache.” Alisisitiza Askofu Mwijage. Katika mahubiri hayo Askofu Mwijage aliongeza kwa kuwahimiza waamini kwenda katika Sakramenti ya toba yaani Sakramenti ya kitubio na kujipatanisha na Mungu na kwamba mwanadamu anapokaa muda mrefu bila kuungama husahau dhambi alizozitenda na kuihalalisha dhambi yake na kuongeza kuwa dhambi haiondoki kwa kuhalalishwa bali huacha makovu katika mioyo ya wasio ungama.
“Mwaliko wa Mungu unataka tuanze kwa sisi wenyewe kutubu kisha kuwaalika wengine watubu na kipindi hiki cha Kwaresima Mungu anatudai toba hivyo tuineshe nia ya kurudi kwake na baadhi yetu tunapitisha muda mrefu au mwaka mzima bia kuja katika Sakramenti ya kitubio na ukipitisha muda mrefu unasahau dhambi uliyotenda na dhamiri unaibutua, mtu anatenda dhambi naye anasema eti Mungu anajua hali yangu ilivyo ngumu, wengine wanakwenda mbali zaidi kwa kuhalalisha dhambi zikubaliwe na wengi wanadhani hapo dhambi zitaondoka na dhamiri zao zitakua huru, huko ni kujidanganya, dhambi haiondoki kwa kuhalalisha ila inatuletea makovu ambayo hayaponyeki.” Aliongeza Askofu wa jimbo la Bukoba Tanzania.
Askofu Mwijage alihitimisha homilia yake kwa kuwahimiza waamini kufunga na kujikatalia pamoja na kuachilia mbali vilema walivyonavyo ikiwemo masengenyo, uongo , wivu, uvivu , matusi, lugha mbaya, hasira udanganyifu, umbea na kujinyima furaha za dunia na hatimaye kufufuka pamoja na Kristo. “Katika kipindi hiki pia tunaalikwa kufunga chakula na vilema vyetu ikiwemo masengenyo, uongo wivu, uvivu, matusi, lugha mbaya, hasira udanganyifu, umbea na udanganyifu au kula rushwa na kujinyima furaha za dunia Fulani Fulani, wakati mwingine ulitakiwa kwenda kutembea unatakiwa kusoma neno la Mungu na kufanya hivyo tutakua tunaandaa njia safi itakayomkaribisha Kristo Mfufuka.” Alihitimisha Askofu Mwijage katika homilia yake.