Zambia,TUKUZA:Siku ya maombi na tafakari kuhusu biashara haramu ya binadamu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kila tarehe 8 Februari ya kila Mwaka, Mama Kanisa anamkumbuka Mtakatifu Josephine Bakhita, sanjari na Siku ya Kimataifa ya Maombi na Tafakari ya Kupambana na Biashara Haramu wa Binadamu. Katika fursa ya siku hiyo, hata watawa wa Mpango wa Talitha Kum nchini Zambia (TAKUZA) wamejikita kutoa ahadi ya uendelevu wa utetezi wa watu hao na kuwa karibu na waathirika wote. Katika kudhimisha siku kuu hiyo ambayo Makatifu osephine Bakhita, ni msimamizi wa wathiriwa wa Utumwa Mamboleo na bishara haramu ya binadamu, iliyoongozwa mwaka 2024 na mada:“ Safari katika hadhi: kusikiliza, kuota na kutenda”, Watawa wa Zambia walitoa ahadi zao za kupambana na janga hili baya sana la utumwa mamboleo.
Mtandao wa TUKUZA
Kwa mujibu wa Shirika la Habari za Kimisionari Fides, limebainisha kuwa, TAKUZA ilianzishwa mnamo mwaka 2021 na watawa watatu, Sista Kayula Lesa wa Shirika la Masista wa Upendo, Sista Mutinta Simaanza wa Masista wa Roho Mtakatifu na Sista Veronica Ramotse wa Shirika la Watumishi Wadogo wa Maria Safi. Watawa hao watatu walikuwa miongoni mwa washiriki 35 wa kozi iliyofanyika mnamo mwaka 2020 iliyohamasishwa na Mtandao wa Kimataifa wa Talitha Kum kwa ajili ya kuunda mitandao ya kitaifa na kikanda duniani kote ili kukabiliana na janga hilo la biashara haramu ya binadamu.
Mtandao wa kimataifa wa Talitha Kum
Talitha Kum iliyoanzishwa mnamo 2009 ndani ya Umoja wa Kimataifa wa Mama Wakuu wa Mashirika ya Watawa (UISG), unahamasisha ushirikiano kati ya mitandao iliyoandaliwa katika ngazi ya kitaifa, kikanda na bara, ili kupambana kikamilifu na biashara haramu ya binadamu na unyonyaji, kusaidia kwa dhati waathiriwa, waathirika na watu walio katika mazingira hatarishi. Kwa njia hiyo chombo hiki TAKUZA kilianza kufanya kazi rasmi mnamo Mei 2022. Kwa sasa kina wafanyakazi watatu wa kudumu nchini kote na vikundi vya uhamasishaji katika majimbo 11 ya Kikatoliki nchini Zambia. Mpango huo kwa sasa unatekelezwa na Masista wa Shirika la Upendo.
Kitovu cha biashara haramu
Kuhusiana na mtanado huo ni kwamba Zambia inabainika kuwa kitovu cha biashara haramu ya binadamu kusini mwa Afrika, hasa kwa upande wa wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali kama vile Ethiopia, Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rwanda na sehemu nyinginezo, wanaotafuta nafasi za kazi katika nchi tajiri kama vile Namibia na Afrika Kusini. Kanda hiyo ina makubaliano ya usafirishaji huru wa watu na bidhaa chini ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo inafanya iwe rahisi kwa wafanyabiashara wa binadamu kusafirisha watu kuvuka mipaka.
Vitisho vya wafanya biashara haramu
Yapo Mashirika mbambali chini ya vivuli vya kibiashara wakati wakifanya biashara haramu ya binadamu yanayofanya kazi nchini Zambia ambayo yanawanyonya wanawake na watoto kutoka nchi jirani ili kuwageuza kuwa vibarua vyao kwa kulazimishwa au kuwatuma wanawake katika ukahaba. Wanawake wa Rwanda ndio hasa walengwa. Wanashawishiwa hadi Zambia kwa ahadi kwamba watapata hadhi ya ukimbizi na kupata manufaa ya kiuchumi. Hatimaye, katika kudanyanywa huko wanakuwa watumwa wa ngono na wanashikiliwa kinyume na mapenzi yao. Wasafirishaji haramu wa binadamu, wanatishia kuwakabidhi wahamiaji haramu kwa maafisa wa uhamiaji iwapo watakataa kufanya kile wanachoambiwa. Hivi ni vitisho vikubwa ambavyo Watawa wa Mpango wa Talitha Kum- TUKUZA wanajaribu kuwanasua katika mtego huo, ili kuwarudishia hadhi yao na ikibidi kuwarudisha nyumbani kwao.