Ask.Mwijage:Ushemasi unadai utoke katika ratiba binafsi na utangaze habari njema!
Na Patrick Tibanga – Bukoba na Angella Rwezaula - Vatican.
Bwana anaendelea kuita wafanyakazi katika Shamba lake kwani Yeye mwenyewe aliwambia wanafunzi wake kuwa:“Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.(rej. Lk 10,2). Kwa neema Kanisa la Tanzania, linazidi kuongezeka miito ya Upadre na ya Watu waliowekwa wakfu. Ni katika muktadha wa shamba na mavuno ambapo Kanisa la Bukoba limewapokea mashemasi watano ambao sasa wanaelekea katika daraja la Upadre panapo majaliwa, mara baada ya kupeokea daraja la Ushemasi.
Katika tukio hilo Mwashamu Jovitus Mwijage, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba Tanzania, katika mahubiri yake katika maadhimisho ya MisaTakatifu ya Sakramenti Takatifu ya daraja la Ushemasi, iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama mwenye huruma, Bukoba tarehe 16 Machi 2024, alisisitiza juu ya maana ya wito. Katika mahubiri washemasi walishauriwa wawe na baraka na furaha kwa wale watakao wahudumia huku wakizingatia umakini ili wasikwame katika wito wao. Umakini huo uambatane na kuishi maisha ya Sala kila mara ili roho wa Bwana iambatane nao siku zote katika wito wao.
Mhashamu Mwijage aidha akiendelea alisitiza kuwa mara baada ya kuimarishwa, Mashamasi utambulika kama wafuasi wa Kristo hivyo wanakuwa wasaidizi wa Askofu kwa kutenda kama alivyotenda Kristo wakiwaimarisha Waamini kiimani na kuwainua kiroho. Askofu Mwijage alisema kuwa wito wa Mashemasi unawadai kila mmoja atoke katika maisha na ratiba zake azipendazo ikiwemo haki za kimwili, bali yote hayo wayatolee Mungu kwa ajili ya kutangaza habari njema. Hali kadhalika aliwahimiza wafuate maisha ya Ibrahimu, Baba wa imani, wamtumikie Mungu siku zote na kamwe wasiwaze kujiondoa kwenye shamba la mzabibu.
Waliowekwa wakfu katika Daraja hilo Takatifu la ushemasi ni: Shemasi Allanus Kabobo wa Parokia ya Kishogo, Shemasi Beatus Kaijage, wa Parokia ya Kagondo, Shemasi Cassius Rwelamiza wa Parokia ya Ngote, Shemasi Prudence Mujwahuzi wa Parokia ya Minziro na Shemasi Willbrord Ndyamukama wa Parokia ya Itahwa, wote ni wa Jimbo Katoliki Bukoba. Misa iliudhuriwa na mapadre,, watawa, waseminari, waamini wa Mungu, wazazi ndugu, marafiki na watu wenye mapenzi mema, kushuhudia makuu ya Mungu katika Wito huo na wao kuitikia wakisema “Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”(Heb 10:7) au kuitikia kama Mama Maria alisema “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.” (rej. Lk 1,38).
Ikumbumbwe Askofu Jovitus Mwijage Hivi karibuni, tarehe tarehe 27 Januari 2024 alisimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo hilo katika, Ibada iliyoongozwa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Tabora, Tanzania huku akisaidiana na Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, Msimamizi wa Kitume wa Jimbo hilo kabla ya tangazo la kustaafu ambalo lilitolewa mwishoni mwa maadhimisho ya Ibada ya Misa ya Askofu Mteule wa 5 mzaliwa wa Jimbo la Bukoba. Baba Mtakatifu Francisko alimteua Askofu Mwijage mnamo tarehe 19 Oktoba 2024.
Askofu Jovitus Francis Mwijage alizaliwa tarehe 2 Desemba 1966 Jimboni Bukoba baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 20 Julai 1997 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tangu wakati huo, alibahatika kutekeleza dhamana na utume wake kama Paroko-usu Parokia ya Mwemage, Mlezi Seminari Ndogo ya Rubya, Jimbo Katoliki la Bukoba. Mwaka 2011 alijipatia shahada ya uzamivu kwenye historia ya Kanisa toka Chuo Kikuu cha Gregorian, Roma.
Kuanzia mnamo mwaka 2005 hadi 2011 alitumwa na Jimbo Katoliki la Bukoba kwa ajili ya kujiendeleza katika masomo ya juu na hivyo kujipatia shahada ya uzamivu kwenye historia ya Kanisa kunako mwaka 2011. Kati ya mwaka 2011-2012 alikuwa ni Jaalimu wa historia ya Kanisa, Seminari kuu ya Segerea. Tangu mwaka 2012 hadi mwaka 2023 aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS, Tanzania. Na tangu mwaka 2012 hadi uteuzi wake, alikuwa ni Mkurugenzi mtendaji wa Umoja wa Mapadre Wazalendo Tanzania, UMAWATA na pia kuanzia mwaka 2020 alikuwa ni Mjumbe wa Kamati ya Kimataifa ya Uchumi ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS.