Askofu Sangu: Waamini Iweni Chachu ya Faraja, Amani na Matumaini
Na Moshi Ndugulile Jimbo Katoliki la Shinyanga.
Maadhimisho ya Dominika ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu ni kipindi cha: furaha na shangwe; mateso na huzuni; lakini pia ni kipindi cha matumaini kwa ajili ya ushindi wa Kristo mfufuka. Kanisa lina matumaini makubwa katika ile Siku ya kwanza ya Juma! Dominika ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho matukio makuu katika historia ya wokovu kadiri ya imani ya Kikristo. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni chimbuko la faraja; Imani, matumaini na mapendo kwa watu wote, lakini zaidi kwa wale wanaoteseka kutokana na changamoto mbalimbali za maisha badala ya baadhi ya watu ndani ya jamii kujinufaisha kutokana na shida pamoja na changamoto zao.
Huu ni wito uliotolewa na Dominika ya Matawi tarehe 24 Machi 2024 na Askofu Liberatus Sangu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga katika mahubiri aliyoyatoa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mama wa Huruma, Parokia ya Ngokolo, Jimbo Katoliki la Shinyanga. Amewataka waamini kuendelea kuwa ni vyombo vya ukarimu na upendo kwa jirani zao; kwa kusimamia na kutekeleza haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Waamini wawe ni chachu ya faraja, amani na matumaini kwa jirani zao wanaoteseka badala ya kujinufaisha kwa shida za jirani zao, hali inayomchukiza Mwenyezi Mungu.
Waamini waendelee kupyaisha upendo na huruma ya Kimungu katika maisha yao ya Kikristo kwa kutenda mema, kutafuta na kudumisha haki, amani na maridhiano kwa watu wote hasa kwa wagonjwa, watoto yatima wagane na wajane, bila kuwasahau wafungwa. Maadhimisho ya Juma kuu ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani; mwaliko na changamoto kwa waamini kuwa ni nuru na mwanga kwa wengine, huku wakisukumwa na upendo wa Kimungu kama ule uliotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu kwa mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu.
Kwa upande wake Padre Adolfu Makandagu Parokia ya Ngokolo, Jimbo Katoliki la Shinyanga, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwarithisha watoto wao: Imani, desturi na mila njema, tayari kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Amewaalika waamini kuendelea kuwategemeza Mapadre kwa moyo wao wa ukarimu na upendo kama ishara ya kutambua na kuthamini huduma za maisha ya kiroho zinazotolewa na Mapadre kwa watu wa Mungu.