Kardinali Ambongo:uchoyo usiofaa ndiyo mzizi wa ukoloni mpya!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Askofu Mkuu wa Kinshasa, pamoja na kuliongoza Jimbo kuu la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), pia anazo nyadhifa muhimu za Kanisa la Ulimwengu, kwa Afrika ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagascar (SECAM), na ni Mjumbe (jukumu alilipyaishwa mwaka mmoja uliopita na Papa) wa Baraza la Makardinali (C9), ambao ni washauri wa Papa. Zaidi ya hayo, mara kadhaa amekuwa akichukua nafasi za uongozi katika matukio ya kisiasa ya Afrika na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo Kanisa Katoliki hutoa maelfu ya waangalizi katika chaguzi za kisiasa na kufanya kazi ili kuwezesha na kukuza mazungumzo kati ya nguvu za kisiasa na kijamii za nchi. Kardinali Ambongo mwenyewe aliongoza mazungumzo ya kitaifa yaliyoiongoza DRC kwenye uchaguzi mpya mwishoni mwa 2018, shukrani kwa kusainiwa kwa Mikataba ya mkesha wa Mwaka Mpya. Hivi karibuni Kardinali Ambongo alishiriki mikutano na alifanya mkutano uliojikita juu ya mada: “Utume na mazungumzo ya kidini barani Afrika”, ulioandaliwa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Antonianum jijini Roma.
Mizizi na athari za kiuchumi za Ukoloni Mamboleo
Katika hotuba zake zake, Kardinali Ambongo mara nyingi anarejea kwa ukali zaidi mfumo wa uendeshaji wa sekta na vifaa vya Magharibi vyenye ushawishi kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na mataifa mengine ya Kiafrika. Na mfano wa wazi wa operesheni zilizofanywa kwa mwendelezo wa mawazo ya kikoloni unawakilishwa na makubaliano ya hivi karibuni yaliyotiwa saini na Umoja wa Ulaya na Rwanda kwa ajili ya unyonyaji wa maliasili. “Kama inavyojulikana majuma machache yaliyopita makubaliano yalitiwa saini kati ya Ulaya( EU) na Rwanda kwa ajili ya unyonyaji wa madini na rasilimali nyingine ambazo, kiukweli, hazipatikani Rwanda lakini nchini Congo. Hili halivumiliki na linazua mkanganyiko mkubwa katika eneo, lile la Maziwa Makuu, ambalo tayari linakabiliwa na mvutano mkubwa,”alieleza Kardinali Ambongo kwa Shirika la Habari za Kimisionari Fides. “Katika eneo lote, kiukweli, kuna vita hata kama haijatangazwa, vita baridi kati ya Burundi, Rwanda, Uganda na Congo. Vita ambapo uwanja pekee wa vita ni Congo, na mwathirika wa kwanza wa hali hii ni watu wetu. Mwishowe, sababu mbalimbali zinaweza kutumika lakini zote zinarudi kuwa moja la unyonyaji wa maliasili!
Congo ni kati ya nchi tajiri za rasilimali katika sayari
Congo ni kati ya nchi tajiri zaidi kwa rasilimali kwenye sayari. Hizi ni bidhaa ambazo zimeonekana kuwa muhimu kabisa kwa ulimwengu katika kila awamu ya kihistoria: mpira mwanzoni mwa karne iliyopita, kisha dhahabu, almasi, mafuta na sasa coltan na cobalt. Bidhaa za thamani, zilizojilimbikizia katika mojawapo ya nchi maskini zaidi duniani. “Tumeathiriwa na umaskini mkubwa na hii licha ya ukweli kwamba Congo ni nchi yenye uwezo mkubwa.” Kulingana na Kardinali, nchi inakabiliwa na mfululizo wa mambo mabaya sana, kuanzia na “nia mbaya ya watu walio madarakani kunyonya utajiri huu kwa manufaa ya wote, si kwa manufaa ya duru zilizozuiliwa tu.” alisema Kardinali Ambongo. Aidha Kardinali pia anaitilia shaka “njaa ya upanuzi na uchoyo usio na uadilifu wa wale wanaosimamia wanaume hawa, ambayo ni, Ulaya, Amerika Kaskazini, India, China.” Congo ni sahani ambayo kila mtu huja kula, isipokuwa watu wetu.” Mbali na umaskini, Askofu Mkuu wa Kinshasa pia anarejea hali ya ukosefu wa usalama ambayo huathiri hasa maeneo ya mashariki ya nchi, ambapo alisema “kipande muhimu sana cha Congo (mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini na Ituri, ed.) haidhibitiwi tena na Kinshasa, lakini kwa kiasi kikubwa kiko chini ya mamlaka ya Rwanda, Burundi, Uganda (eneo linalozidi kuwa kubwa la Kivu sasa liko chini ya udhibiti wa kundi linalounga mkono Rwanda la M23). Haya yote hayakubaliki pia kwa sababu yanatokea kwa baraka za jumuiya ya kimataifa.”
'Ondoeni mikono barani Afrika'
Zaidi ya mwaka mmoja umepita tangu ziara ya Papa Francisko nchini Congo na Sudan Kusini. Katika Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko wakati yuko mjini Kinshasa, alitoa neno ambalo limekuwa maarufu kuhusu: 'Ondoeni mikono mbali na Afrika'. “Ni maneno ambayo yalichangia kuchochea tafakari mpya ndani ya Kanisa na katika ulimwengu wa siasa za kimataifa. Baada ya Papa kupita Congo na baada ya hotuba yake hakuna anayeweza kusema: 'Sikujua' au kujifanya kuwa sivyo.” Alisisitiza Kadinali Ambongo. “Papa alianzia Congo, kuelezea ishara ya unyonyaji, ili kupanua mjadala kwa bara zima na ameamsha dhamiri. Ni mwaka mmoja tu umepita na mabadiliko ya kiutendaji yaliyoitishwa na Papa katika suala la unyonyaji bado hayajaonekana. Hata kama katika kiwango cha dhamiri, kwa maoni yangu, mengi yamebadilika.”
Maswali mengi kuliko majibu katika historia ya kusikitisha ya Balozi Attanasio
Mnamo tarehe 22 Februari 2024 iliyopita, katika hafla ya kuadhimisha miaka tatu tangu kuawa kwa Balozi wa Italia Dk Luca Attanasio, mlinzi wake Askari Vittorio Iacovacci na dereva Mustapha Milambo, Kardinali Ambongo waliadhimisha misa ya ukumbusho katika Kanisa Kuu la Kinshasa. Askofu Mkuu Ambongo alimfahamu Attanasio vyema na alikuwa na uhusiano mzuri naye. Kifo chake, na historia ya majaribu ambayo yaliacha mashaka zaidi kuliko uhakika, vinabaki kama jeraha wazi. “Hisotoria ya Luca Attanasio ni mateso ya kibinafsi kwangu. Luca hakuwa Balozi wa Italia mjini Kinshasa pekee bali pia alikuwa rafiki ambaye alikuja kunitembelea mara nyingi. Alikwenda kila mahali, alikuwa rafiki mkubwa wa watu na alifanya mengi kwa kiwango cha hisani kwa masikini. Mtu kama huyo, ambaye aliishia hivyo, bado ni mshtuko mbaya kwangu. Kwa bahati mbaya hadi sasa hatujui kilichotokea lakini nina uhakika serikali ya Italia inajua.” Alisisitiza, Kardinali Ambongo. Mnamo Aprili 2023, kesi iliyoendeshwa na mahakama ya kijeshi ya Kinshasa dhidi ya waandaaji na wahusika wa shambulio hilo ilimalizika kwa hukumu ya kifo kisha kubadilishwa, kupitia kuingilia kati kwa familia ya Attanasio na Serikali ya Italia, hadi kifungo cha maisha. “Ni historia ya ajabu, kuna maswali mengi zaidi ya majibu” alitoa maoni Kardinali Ambongo “lakini ninaweza kusema jambo moja kwa uhakika: wale watano waliokamatwa na kuhukumiwa walitumwa wa kuadhibiwa tu, sote tunajua kuwa mtu alihitajika kulaumiwa ili kufunga haraka kesi, lakini hawana uhusiano wowote nayo.”
Kuhusu hati ya Fiducia Supplicans
Kuchapishwa kwa waraka wa Fiducia Supplicans kumezua mijadala mingi barani Afrika na kwingineko lakini na maoni machache kabisa. Kardinali Ambongo, akiwa Rais wa SECAM, alitaka kufungua mashauriano ndani ya Makanisa ya Afrika, akasikiliza Mabaraza ya Maaskofu kisha akakutana na Papa moja kwa moja. “Tatizo lilikuwa kwamba majibu kwa Fiducia Supplicans yalikuwa ya mkanganyiko. Kulikuwa na maaskofu na mapadre ambao walimwandikia Papa, wengine ambao walimkosoa vikali. Mimi, kwa nafasi ninayoshikilia kama Rais wa SECAM, sikuweza, kuacha mambo yaendelee hivi, kwani kungekuwa na miitikio isiyo na vigezo. Ndiyo maana niliuliza Mabaraza ya Maaskofu na sio watu binafsi, wanifahamishe maoni yao.” Alisema Kardinali Ambongo. "Kwa hiyo tulifanya mukhtasari wa matokeo ya maoni na nikaenda kuonana na Papa. Tulizungumza kwa muda mrefu. Kwangu mimi kulikuwa na mambo mawili ya kuhakikisha: ilikuwa ni lazima kuwahakikishia waamini wa Kiafrika ambao walihisi kuumizwa sana na hati hiyo na pia kulinda ushirika na Baba Mtakatifu. Kwa hivyo, kutokana na mazungumzo yetu, iliibuka taarifa ambayo iliwekwa wazi na maandishi yenye kichwa: “Hakuna baraka kwa wapenzi wa jinsia moja katika Makanisa ya Kiafrika.” Kisha mambo yakatulia. Papa Francisko alipata suluhisho. Na ninamshukuru sana Papa ambaye alionesha uwazi mkubwa, hisia za kichungaji na kusikiliza sauti ya Kanisa Barani Afrika.”