Kardinali Pengo: Uongozi Ni Huduma: Mchagueni Kristo Ili Msimamie Ukweli na Haki
Na Celina Munde, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania
Dominika ya Matawi, ni mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Matawi ni ishara ya ushindi wa Kristo Yesu dhidi ya dhambi na mauti. Kumbe, Kanisa linaadhimisha Siku ile Yesu alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani huku wakiimba kwa shangwe “Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana” Mt 21:9 na Pili huu ni mwanzo wa mateso, kifo na ufufuko. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, Dominika ya Mateso, tarehe 24 Machi 2024 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Polycarp, Askofu na Shahidi, Kilamba, Mbagala, Jimbo kuu la Dar Es Salaam. Katika mahubiri yake, amewataka viongozi wa Kanisa katika ngazi mbalimbali kutambua dhamana ya utumishi wanaoutekeleza kwa kumbeba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu kama ilivyokuwa kwa yule Punda, Dominika ya Matawi. Waamini daima wajitahidi kumchagua na kuwa upande wa Kristo Yesu, ili kusimamia ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu na kamwe wasimchague Baraba kama ilivyotokea kwa Wayahudi. Ibada ya Misa Takatifu Dominika ya Matawi, imegawanyika katika sehemu kuu mbili.
Sehemu ya kwanza ni Maandamano ya waamini wakiwa wamebeba matawi ya mitende mikononi mwao, ukumbusho wa Kristo Yesu kuingia mjini Yerusalemu na hii ni kiri ya imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu alipanda Punda, kielelezo cha huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, kabla ya kuingia mjini Yerusalemu, Kristo Yesu aliwatuma wafuasi wake kwenda kumwandalia. Nafasi ya Punda ni muhimu sana kama kielelezo cha huduma kwa watu wa Mungu kuanzia kwa Maaskofu, Mapadre, Viongozi walei hadi kufikia katika ngazi ya familia. Viongozi wa Kanisa kamwe wasijisahau kwamba, heshima wanayopewa na watu wa Mungu ni kwa sababu ya huduma yao kama ilivyokuwa kwa yule Punda, kwa sababu wanambeba na kumchukua Kristo Yesu migongoni mwao. Hii ni heshima inayotolewa kwa Kristo Yesu na wala si kwa Punda, ili kumfikisha Kristo Yesu mjini Yerusalemu. Viongozi wakisahau na kumtupa Kristo Yesu nje ya vipaumbele vyao, wataweza kukiona cha mtema kuni na kamwe wasishangae kubezwa na hatimaye, kudharauliwa na watu. Kila mwamini anaheshiminika na kuthaminiwa kwa sababu ndani mwake amembeba Kristo Yesu, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu. Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha mateso makali aliyopitia Mwana wa Mungu. Katika mateso haya, mara nyingi kuna baadhi ya wahusika hawapewi uzito unaostahili hawa ni Pontio Pilato na Baraba. Pontio Pilato alitamani sana kumwachia huru Kristo Yesu ndiyo maana akawaletea mbele yao Baraba aliyetupwa gerezani kwa ajili ya fitina iliyotokea mjini na kwa ajili ya mauaji, lakini kwa mshangao mkubwa, watu wakaamua kumchagua Baraba na Kristo Yesu asulubiwe. Hakuona kosa, lakini sauti zilisikika zikisema asulubishwe.
Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa ni chanzo cha uhai na uzima, aliyewalisha watu, akawaganga na kuwaponya magonjwa yao; akawasamehe dhambi zao na hivyo kuwarudishia hadhi wale waliotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii kwa hakika Kristo Yesu alikuwa ni mtetezi wa wanyonge. Lakini Kardinali Pengo anasikitika kusema, watu wakaamua kumchagua Baraba, muuaji ili aendelee kukaa pamoja nao. Jambo hili lilimkwaza Pontio Pilato hadi kifo chake! Lakini hata leo hii, bado kuna watu wanaosimama upande wa Baraba na kutenda kama Wayahudi. Kuna watu wangapi wasiokuwa na hatia wanaoendelea kuteseka kwa sababu ya kuwabeba na kuwaenzi akina “Baraba” katika jamii? Hawa akina Baraba ni sababu na chimbuko la mateso ya watu kila siku. Uonevu, dhuluma, nyanyaso na mauaji ya watoto wadogo ni mambo yanayoendelea kufanyika ndani ya jamii. Lakini mbele ya sheria na haki, akina “Baraba” wanaendelea kupeta katika jamii. Kumbe, chaguo la Baraba katika jamii ni jambo linaloendelea kutendeka hata leo hii. Kardinali Polycarp Pengo anakaza kusema, Liturujia ya Neno la Mungu inatoa kipaumbele cha kwanza kuwa ni kumchagua Kristo Yesu na kwamba, uamuzi huu una gharama zake, ni kupoteza yale yanayopendeza katika maisha. Kardinali Pengo anawataka waamini wamchague Kristo Yesu kwa kusimamia na kutenda kwa haki na ukweli. Waamini wasimame kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaokoa wale wanaoteseka. Kamwe wananchi wasiwashabikie na kuwaenzi watu wanaoleta mateso na mahangaiko katika jamii kwa sababu ya rushwa, takrima, zawadi, hongo au ahadi hewa. Kwa kuendekeza mambo kama haya, watu wengi watajikuta wakiwa wanamuunga mkono Baraba badala ya kusimama upande wa Kristo Yesu ili kujenga na kudumisha haki, utu na heshima ya binadamu.
Kwa upande wake, Padre Timoth Nyasulu Maganga, ambaye anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu apewe Daraja Takatifu ya Upadre, amemshukuru Kardinali Polycarp Pengo kwa kuwatembelea na kuadhimisha Ibada ya Dominika ya Matawi Parokiani hapo. Hii ni baraka na amemwomba Kardinali Pengo kuendelea kuwaenzi kwa sala na sadaka yake ili kweli Parokia hii, iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake. Waamini waendelee kujisadaka kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya Mapadre ambayo kwa sasa iko katika hatua za mwisho mwisho.