Maadhimisho ya Ijumaa Kuu: Msalaba: Ishara na Alama ya Ushindi: Dhambi na Kifo
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, siku ya Ijumaa Kuu. Awali ya yote ikumbukwe kuwa siku ya Ijumaa Kuu Kanisa haliadhimishi Sakramenti zozote ikiwa ni pamoja na Sadaka ya Misa Takatifu kwa kufuata mapokeo ya tangu zamani za kale kabisa. Altare iko tupu kabisa, haina msalaba wala mishumaa, wala vitambaa. Hii ni kwa sababu ni siku ambapo Yesu Kristo alikufa msalabani – ndiyo kusema alijitoa Yeye mwenyewe Sadaka, kafara ya mwanakondo wa Agano jipya na la milele. Siku ya Ijumaa Kuu Mama Kanisa na wanae anaadhimisha mateso na kifo cha Bwana wake Yesu Kristo. Hali kadhalika, siku ya Jumamosi Kuu Kanisa haliadhimishi Sadaka ya Misa Takatifu, liko kimya likiyawaza-waza mateso na kifo cha Yesu, mpaka zitakapoanza sherehe za Pasaka baada ya Vijilia Takatifu katika Kesha la ufufuko. Ibada anayoadhimisha Mama Kanisa siku ya Ijumaa Kuu, imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Nayo inaanza kwa Padre na watumishi kuja altareni wamevaa mavazi mekundu kama kwa Misa. Wanatoa heshima mbele ya altare kama kawaida, wanajilaza kifudifudi, au wanapiga magoti kama inafaa, na wote wanasali kimya kwa kitambo. Kisha wanakwenda kwenye viti altareni, na Padre anasali sala ya mwanzo akisema; “Ee Mungu, kwa mateso ya Kristo Mwanao Bwana wetu, umetuondolea mauti tuliyorithi sisi binadamu wote kwa dhambi ya kale. Utujalie sisi tuliozaliwa na hali ya kibinadamu kwa maumbile, tuzaliwe na hali ya kimungu kwa kutakaswa na neema yake”. Sala hii anaisali akiwa amefumba mikono, bila kusema tuombe.
Kisha madhehebu hayo ya mwanzo, ndipo inaanza sehemu ya kwanza, liturujia ya Neno. Kiini cha sehemu hii ya kwanza ni simulizi la mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo kilichotuletea wokovu. Sehemu hii inahimishwa kwa maombezi kwa watu wote. Hivyo ni vyema katika sehemu hii kila mmoja ndani ya moyo wake kujiombea mwenyewe na kuwaombea wengine kila inapofika ile sehemu ya kutafakari Padre anapotualika kusali akisema, tuombe, tupige magoti, simameni. Haya maelekezo anayoyatoa Padre tusiyafanye tu kwa mazoea bali tusali na kuomba kweli tunapopiga magoti na tukisimama Padri anasali kwa niaba ya watu wote. Sehemu ya pili ni Kuabudu Msalaba, wokovu wa dunia uliotundikwa juu yake, ndiye Yesu Kristo. Na sehemu ya tatu ni ibada ya Komunyo Takatifu, tunda la mateso kifo na ufufuko wa Kristo kama sala kabla ya kumunyo inavyosema; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, wewe umetukomboa kwa kufa na kufufuka kwake Kristu Mwanao. Dumisha ndani yetu hiyo kazi ya huruma yako, ili tunaposhiriki fumbo hili tuishi katika uchaji sikuzote”. Tukianza na sehemu ya kwanza, liturujia ya Neno; Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 52:13-53:12). Somo hili ni tafakari ya wasifu wa mtumishi wa Mungu. Waamini wa Kanisa la mwanzo waliona uwakilishi wa Yesu Kristo katika sura ya mtumishi huyu wa Mungu aliyetukomboa kutoka utumwa wa dhambi kwa njia ya mateso. Uso wake uliharibiwa sana, hakuwa na umbo wala uzuri wa kumtamani, alidharauliwa na kukataliwa na watu wake, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko, na hakuhesabiwa kuwa si kitu.
Lakini ndiye aliyeyachukua masikitiko yetu, akajitwika huzuni zetu, alijeruhiwa kwa makosa yetu, alichubuliwa kwa maovu yetu, adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Bwana aliweka juu yake maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, hakufunua kinywa chake mbele ya watesi wake. Alionewa na kuhukumiwa, akapigwa kwa sababu ya makosa yetu, na akafanyiwa kaburi pamoja na wabaya. Ingawa hakutenda jeuri, wala hapakuwa na hila kinywani mwake. Bwana aliridhia kumchukua amehuzunisha, akaifanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi zetu. Kwa haki yake akawafanya wengi kuwa wenye haki, kwa kuyachukua maovu yetu na kwa kumwaga nafsi yake hata kufa ili sisi wakosaji tukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Katika mateso yake Yeye, Kristo Yesu Bwana wetu, aliyaweka matumaini yake yote kwa Mungu Baba kama Zaburi ya wimbo wa katikati inavyoimba; “Nimekukimbilia Wewe, Bwana, nisiaibike milele, kwa haki yako uniponye. Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. Kwa sababu ya watesi wangu, nimekuwa laumu, naam, hasa kwa jirani zangu. Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; walioniona njiani walinikimbia. Nimesahauliwa kama mfu asiyekumbukwa, nimekuwa kama chombo kilichovunjika. Maana nisikiapo masingizio ya wengi; hofu ziko pande zote. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana, nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. Umwangaze mtumishi wako, kwa nuru ya uso wako; Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako. Iweni hodari, mpige moyo konde, ninyi nyote mnaomngoja Bwana (Zab. 31 :1, 5, 11-13a, 14-16, 24).
Somo la pili ni la Waraka kwa Waebrania (Ebr 4:14-16; 5: 7-9). Somo hili linatuasa tumwamini Yesu Kristo kuhani wetu mkuu aliyeonja na kuvumilia taabu na mateso mengi kwa ajili ya wokovu wetu. Maana Yeye anafahamu taabu na matatizo yetu, daima Yupo tayari kutuombea kwa Baba. Sharti ni hili; kuyashika maangano yetu tuliyofanya naye kwa njia ya ubatizo. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 18:1-19, 42). Sehemu hii ya Injili inasimulia Yuda kumsaliti Yesu kwa busu, kukamatwa kwake na maaskari wakiwa na taa mienge na silaha katika bustani ya mizeituni. Baada ya kukamatwa, alipelekwa kwa kuhani mkuu Kayafa, mkuu wa baraza la wayahudi, “Sanhedri”, chombo chenye mamlaka ya juu ya kidini. Baraza likaamuru apelekwe kwa gavana wa Kirumi - Pontio Pilato - naye akaamuru apelekwe kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya - Herode Antipas - kwa alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya. Mahangaiko haya yote ni kwasababu kila mamlaka haikuona hatia yoyote juu yake. Kumbe ni dhambi zetu ndizo zilizomsulubisha kwa hukumu isiyo haki na kufanyiwa dhihaka nyingi na kuteswa sana. Alipigwa mijeledi, akavikwa taji ya miiba, akapigwa kwa mwanzi, akatemewa mate, akabebeshwa Msalaba, akavuliwa nguo, akasulubiwa msalabani, akafa, nchi ikatetemeka, jua likafifia, kukawa na giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili. Naye askari mmoja wapo akamtoboa ubavu kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji, chemchemi za Sakramenti za Kanisa. Matukio na mambo haya ya kutisha na kuhuzunisha yanatuelekeza kulitafakari fumbo la msalaba ambao juu yake umetundikwa wokovu wa ulimwengu, ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Mama Kanisa anatualika kuutazama msalaba kwa moyo wa toba na majuto, kuomba msamaha na kuanza maisha mapya ya kumpendeza Mungu.
Ni katika muktadha huu sehemu ya pili ya Ibada ya Ijumaa kuu, kuubadubu Msalaba, yaani wokovu wa ulimwengu uliotundikwa juu yake, ndiye Yesu Kristo, inapata maana. Ni juu ya Msalaba historia ya ukombozi wetu ilifikia kilele chake. Kumbe, hakuna utukufu bila mateso. Kwa kujua ukweli huu Mama Kanisa anatuhimiza tena na tena watoto wake kuvumilia mateso na magumu yanayotupata katika kumfuata Kristo ili tuufikie utukufu alioufikia yeye maana hakuna Ukristo bila Msalaba. Basi inatupasa kuona fahari ya msalaba wa Yesu Kristo. Mtume Paulo anasema; “Lakini mimi hasha, nisione fahari ya kitu chochote ila Msalaba wa Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu ulisulubishwa kwangu na mimi na ulimwengu” (Gal.6:14). Kumbe, basi Msalaba ni muhuri na kitambulisho cha mkristo. Msalaba ni bendera na bango la ushindi dhidi ya dhambi na mauti. Msalaba ni alama ya ukombozi (Yn.12:13-33), Msalaba ni alama ya upendo wa Kristo kwetu sisi (Yn.3:14-18). Msalaba ni alama ya maisha ya kikristo (Mk.8:34). Msalaba ni alama ya umoja na Kristo. Msalaba ni alama ya ufuasi wa kweli wa Yesu Kristo (Mk 8: 34). Msalaba ni sadaka ya Yesu Kristo, ni zao la upendo (Yn 13:1; 15: 13). Ni kwa njia ya Msalaba tumekombolewa. Msalaba wa Kristo Yesu ni tumaini na faraja yetu, japo kwao wanaopotea ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu. Basi na tuone fahari kwa msalaba wa Yesu Kristo, maana ni kwa njia ya huo, tunasamehewa dhambi zetu, tunaponywa majeraha ya ndani kabisa mwa mtima wa moyo na kupata faraja na amani katika maisha ya sasa na yajayo mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo!