Ijumaa Kuu: Utukufu wa Kristo Yesu Umetundikwa Msalabani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mama Kanisa katika adhimisho la Ijumaa kuu anafanya kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Siku ya kufunga kama kielelezo cha nje kinachoonesha ushiriki wa waamini katika mateso ya Yesu Kristo. Hakuna adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kwani Kristo ambaye ndiye chemchemi ya Sakramenti zote za Kanisa anateseka na hatimaye, kufa Msalabani. Ijumaa kuu jioni, Mama Kanisa anaadhimisha Mateso na Kifo cha Yesu, anayejionesha kuwa ndiye Mtumishi mwaminifu wa Mungu aliyetabiriwa na Manabii katika Agano la Kale. Ni Mwana Kondoo wa Mungu anaye yamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa wengi. Msalaba ni alama kuu inayochukua kipaumbele cha pekee katika Maadhimisho ya Ijumaa Kuu. Ni kielelezo cha Mti wa Ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti, ndiyo maana, waamini wanapata fursa ya kuweza kuabudu Msalaba wa Kristo Yesu. Mpendwa msikilizaji na msomaji, leo Kanisa limetuita na kutukusanya pamoja ili tutafakari kwa pamoja mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristo juu ya Msalaba kwa ajili ya kunikomboa mimi na wewe kutoka katika utumwa wa dhambi. Tunaalikwa tuunganike naye katika mateso haya makali na kufa kwake ili tupate uzima na kuimarishwa imani yetu. Katekesi msingi ya Mama Kanisa katika Ijumaa Kuu ambayo Liturujia yake huanza alasiri mchana madhehehu yake ni mosi, kuna Ibada ya Kifo cha Bwana, ambayo ina sehemu tatu: Liturujia ya Neno, Kuabudu Msalaba na Komunyo: tunaweza kupokea Ekaristi iliyobaki jana yake, lakini si katika umbo la divai, iliyo ishara ya furaha. Siku hiyo Sakramenti nyingine za Kanisa haziruhusiwi isipokuwa kitubio, mpako wa wagonjwa na ubatizo katika hatari.
Altare iwe tupu. Padri na watumishi wanapoingia hakuna wimbo wowote. Wakishafika mbele ya altare wanajilaza kifudifudi kama kwa kuishiwa nguvu mbele ya fumbo la mateso ya Bwana, huku waamini wakipiga magoti kimya kabisa. Mara baada ya hapo padri anaanza sala bila ya utangulizi. Yanafuata masomo (bila ya kuyapunguza) ambayo kilele chake ni Mateso kadiri ya Yohane. Baadaye yanafanyika kwa urefu mkubwa, kama yalivyokuwa zamani, maombi (kwa kawaida 10) yanayokumbatia watu wote, kwa kuwa ndiyo siku ya Yesu kujitoa kwa ajili ya wote. Katika sehemu ya pili tunaabudu si mti, bali fumbo la msalaba. Kanisa linataka daima ishara zote ziwe za kweli, hivyo haliruhusu maua ya karatasi au plastiki wala mishumaa ya umeme. La sivyo hata matendo na maneno yetu katika ibada hayatakuwa na maana halisi: yatafanana na yale ya Yuda alipombusu Yesu kwa kumsaliti. Basi, ishara yake iwe msalaba mmoja na mkubwa wa kutosha, si mingimingi midogo, kwa sababu aliyekufa kwa ajili ya wote ni mmoja tu. Watu wakiwa wengi mno, baada ya baadhi yao kuabudu Msalaba binafsi (k.mf. kwa kuubusu), padri anaweza kuuinua ili waliobaki wauabudu kwa pamoja (k.mf. kwa kuupigia magoti). Baadaye Altare inavikwa na Ekaristi Takatifu iliyobakizwa Alhamisi kuu zinaletwa ili kuwagawia watu, lakini zikibaki tena ni lazima zipelekwe nje ya kanisa, ili tuonje hali ya ukiwa kama ile ilivyowapata mitume: tumeondolewa Bwanaarusi. Kanisa linakumbuka lilivyozaliwa kama Eva Mpya kutoka ubavu wa Adamu Mpya aliyetokwa na damu na maji, ishara za sakramenti zake. Altare inavuliwa tena, kwa sababu haitakiwi kutumika. Tukipita mbele ya msalaba tunapiga goti hadi Jumamosi Kuu jioni.
UFAFANUZI: Tumesikia mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo kama yalivyosomwa kadiri ya Injili ya Yohana 18:1-9,42. Tumesikia kuwa Yesu anatoka na wanafunzi wake kwenda katika bustani ya mizeituni, sehemu ambayo alikwenda mara nyingi kulala. Kwanini alikuwa analala nje kama hapo? kwasababu kulala popote ilikuwa kawaida ya marabi na wanafunzi wao; mara nyingi walikuwa hawana vitanda na waliona vitanda haviwajengei mazingira ya kujinyima. Mazingira hayo yalitakiwa yajengwe wakati wa kujifunza mambo ya Mungu.Ndiyo maana Yesu alisema hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake.Mt.8:20; Lk.9:58. Yuda Iskariote akiwa mwanafunzi wa Yesu alipajua mahali pale alipo Mwalimu wake, hivyo mpango wake wa kumsaliti Yesu kwa ipande 30 vya pesa, hivyo nia yake, inakuwa rahisi, anauanza kwa kuwaarifu makuhani na mafarisayo waende kumkamata Yesu. Akiwa na askari,anamwonesha Yesu kwao kwa busu.Yesu anakamatwa kwa vile alikubali kuteswa kwaajiliya mpango mtakatifu wa kutukomboa wanadamu anaona hakuna haja ya kutetewa,anamkataza Petro asitumie upanga kwa watesi wake.Kwahiari na upendo mkubwa Yesu anaanza mchakato wa ukombozi wa mwanadamu kwa kupelekwa katika baraza la wayahudi-Hiki ni chombo kilichokuwa na madaraka ya juu ya kidini nchini wakati huo;kisha anapelekwa kwa gavana wa Kirumi;Pontio Pilato,ambaye baadaye anampeleka kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya,yaani Herode Antipas kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya.Kisha anahukumiwa .Hapa tujue kuwa Yesu hakuwa na kosa lolote.Alishtakiwa na wakubwa wa Wayahudi.Kadiri ya sheria za kiyahudi Alikutwa na makosa haya ya kutungwa dhidi yake:
Alionekana na hatia ya kuidhihaki nyumba ya Mungu-Ndiko kudai kuwa angeliweza kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu. Yesu alikuwa anazungumzia juu ya mwili wake mwenyewe. Kadiri ya Wayahudi kosa jingine lilikuwa ni kujiita Masiha. Kwani hakulingana na masiha waliyemtaka na kumsubiri wao yaani masiha mkombozi wa kisiasa ambaye mpaka leo bado wanamsubiri. Kadiri ya Wayahudi alikufuru kwa kujiita mwana wa Mungu. Ambapo ni kweli Yesu ni mwana wa Mungu.Lakini wayahudi hawakuamini eti kwa sababu ni mwana wa Yusufu na Maria watu ambao waliwafahamu. Alijiita kuwa ni Bwana wa sabato. Makosa yote haya kwa kufuata sheria za Wayahudi, Yesu alitakiwa auawe. Na kwa kufuata sheria za Kirumi hayakuwa makosa ya msingi hivyo haikumpasa kufa alitakiwa aachiwe huru.Wayahudi hawakuwa na uwezo wa kumuua mtu yeyote kwa vile walikuwa wakitawaliwa na sheria ya Kirumi,kama nilivyosema,hivyo Yesu hakuwa na hatia ya kuuawa,alitakiwa aachiwe huru. Lakini kwa hila ,bila huruma na upendo wowote viongozi wa Wayahudi ili kuitimiza nia yao mbaya ya kumuua Yesu wanamsingizia makosa ya kisiasa ambayo kwa sheria ya Kirumi angeuawa.
Wanamwambia Pilato kuwa Yesu amejiita mfalme wa Wayahudi wakati Wayahudi wanatawaliwa na mfalme mmoja tu, Kaisari. Pia wanadai Yesu amewakataza watu kulipa kodi. Wakati walipaswa kulipa kila mwaka. Anachochea migomo/mapinduz/maandamano ya kuipinga ya serikali ya kirumi. Makosa haya yalikuwa makubwa lakini Pilato bado hakuona hatia lakini kwa kushindwa kushikilia ukweli anamtoa wamtende watakavyo, kwa uonevu anahukumiwa na kusulubiwa kama mhalifu, kati ya wakosefu, juu ya Msalaba. Yesu kwa upendo na hiari anayapokea hayo yote. Anakwenda njia ya mateso hayo makali, anayapokea matusi, dharau, kutemewa mate, kupigwa mijeledi, kupigiliwa misumari na hatimaye kufa msalabani ili tukombolewe! Hakika hakuna utukufu bila mateso. Utukufu umefikiwa baada ya mateso, hivyo pande zote mbili ni muhimu na lazima kwa wokovu. Kwa kujua ukweli huu kanisa linahimiza waamini wote kuvumilia mateso na magumu yanayowapata katika kumfuata Kristu ili waufikie ule utukufu alioufikia yeye.Yesu ameyashinda, haya yote. Mateso ambayo ilitakiwa kila mmoja yamfikie binafsi. Msalaba ulio ishara ya aibu, dhuluma, uonevu na laana unapata hadhi mpya, kwa ishara hiyo ulimwengu umepata wokovu, watoto wa Mungu tumefanywa huru. Ishara ya Msalaba ni sala, saluti ya kila mfuasi wa kweli wa Kristo, ishara ya kujihami, ishara ya baraka, “atakapokuja kuwahukumu watu wote, msalaba utakuwa pamoja naye, kama beji ya heshima na sio aibu” (Fulton Sheen). Ishara ya Msalaba inatumika katika Sakramenti zote, tangu tunapozaliwa hadi tunapozikwa, mawio ya jua hadi machweo yake, usiku kucha mchana kutwa. Ishara hii kuu ipo katika namna mbili:
Mosi Ishara ndogo – kwa kidole gumba kwenye paji la uso, mdomoni na kifuani (na maneno Kwa jina…). Kwamba 1. Kwenye paji la uso tunaonesha kuwa Baba ni nafsi ya 1, Mwana mdomoni ndiye Neno wa milele, Roho Mt kifuani ni upendo wa Baba na Mwana. 2. Tunaungana na Mungu 1 katika nafsi 3 (Kwa hiyo ni Jina sio majina…) 3. Ukombozi ni kazi ya nafsi zote 3 (Baba aliupenda ulimwengu, Mwana akajifanya mtu, Roho anatupa nguvu, anatutakasa na kutufariji) 4. Tunaweka mikononi mwa Utatu Mtakatifu. Pili Ishara Kubwa – Kichwani, kifuani/tumboni na mabegani. Toka kulia kwenda kushoto ni ishara ya ukombozi toka kwa Wayahudi kwenda kwa Mataifa (Papa Innocent III), tumekombolewa toka upande wa kushoto wa dhambi kwenda upande wa kulia wokovu. Leo tunapofanya tafakari hii nzito ya mateso ya Kristo na kifo chake. Ni nafasi ya kuonyesha shukrani za pekee kwa Mungu. Kwani hatuna cha kumlipa kwa tendo hili kuu. Tuoneshe shukrani hizo kwa kumwabudu na kumpokea Yesu wa Ekaristi tukiwa katika hali safi kiroho Pia ni nafasi ya kujiuliza ni kwa namna gain tunaongeza mateso ya Kristo? Ni namna gani tuna kuwa chanzo cha mateso kwa wengine katika familia na jumuiya zetu? Mara ngapi tumewasaliti wenzetu wakapata mateso? Tunakumbushwa pia kubeba misalaba yetu ya maisha kwa upole na uvumilivu wote bila manung`uniko yoyote. Yesu aliye Mungu alipata mateso wewe na mimi iweje tusiteseke? Je, wewe Msalaba wako ni upi? jirani yako, ndoa, mzazi, mtoto, rafiki, ndugu yako, kiongozi wako, padre mwenzako, mtawa mwenzako au… ni nani? ni nini? mazingira unayoishi? kazi? kutoeleweka? tujipe moyo tutashinda. Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha misalaba hiyo yote. Umuone Kristo anavyoteseka msalabani na halafu utazame msalaba wako wewe, inalingana? hailingani. Mkristo unahitaji nguvu ya kubeba misalaba yako kwa imani, nguvu hiyo ipo katika Msalaba wa Kristo.
“Naona kiu”, ndio kiu ya kimwili sababu ya kupoteza damu na maji, uchovu na uchungu… hata hivyo kiu yangu ya kiroho ni kubwa zaidi, kiu ya mabadiliko yako wewe na taifa langu lote, kwamba muokolewe na yote yawezayo kuwaharibu, muipate neema na baraka ya Pasaka, damu yangu na kifo changu cha Msalaba visipotee bure bali viwasaidie nyote kupata msamaha na maondoleo ya dhambi zenu, mnijue, mnipende, muiamini Injili na kuokoka milele… Tunapohimizana kuibeba Misalaba yetu haina maana kuwa ni ruksa kuwasababishia wengine maumivu ya moyo, roho, akili, kihisia, kijamii, kiuchumi, kisiasa nk kwa vile tu watavumilia kama Msalaba. Sio utu wa kweli huo, kuwa chanzo cha huzuni ya mwingine, utamsababisha atende dhambi kwa kumkwaza kwa maisha yako, maamuzi yako, maneno yako, mwenendo wako, makosa yako, uongo wako, kukosa unyenyekevu kwako, kukosa uaminifu, kujidai kwako, kudharau kwako, kujikweza kwako... “majaribu hayana budi kuja lakini ole wake yeye ayaletaye. Yamfaa zaidi afungiwe jiwe la kusagia na kutoswa baharini kuliko kumkwaza mmojawapo wa wadogo hawa” (Lk 17:1-2). Hivyo tujihadhari tusiwe sababu ya huzuni ya wenzetu. Inama, fumba macho tafakari ni kwa namna gani umekuwa msalaba kwa mwenzako. Tutafanya tendo la nje la kuuheshimu mti na kuuwabudu wokovu wetu(Yesu) ulio juu ya msalaba ambao ni alama ya ukombozi.Yn.12:13-33;ni alama ya upendo.Yn.3:14-18 na alama ya maisha ya kila siku ya wakristo.Mk.8:34.Tuadhimishe tendo hilo kwa ibada na unyenyekevu tukiguswa na mioyo yetu kweli kwa sadaka hii kamilifu aliyojitoa Yesu msalabani.Katika sala zetu na ibada zetu tunatumia ishara ya msalaba, wengine tumeweka misalaba majumbani na wengine tunavaa misalaba shingoni.Tusifanye mambo haya kimazoea bila kutafakari maana na wajibu tuunaokabiliwa nao ambao umefichwa katika ishara hiyo na misalaba hiyo.Tunachokumbushwa ni kwamba HAKUNA UKRISTO BILA MSALABA.Yaani hakuna ukristo pasipo mateso,magumu na wajibu. Kifo cha Kristo Msalabani kitukumbushe kuwa inatupasa kuona fahari ya msalaba wa Yesu Kristo” Lakini mimi hasha, nisione fahari ya kitu chochote ila msalaba wa Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu ulisulubishwa kwangu na mimi na ulimwengu” Gal.6:14. Hivyo, msalaba ni muhuri na kitambulisho cha mkristo.