Pasaka ya Bwana: Mateso, Kifo na Ufufuko Kwa Wafu: Kiini cha Imani ya Kanisa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pasaka. Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ndiye kiini cha historia ya wokovu. Pasaka ni siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni siku ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti ambao sisi nasi kwa ubatizo tunakufa kuhusu dhambi na kufufuka pamoja na Kristo. Ndiyo maana katika wimbo wa mwanzo tunaimba; “Nimefufuka na ningali pamoja nawe; umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, aleluya (Zab.139:18, 5-6). Ni shangwe kuu kwani Bwana amefufuka kweli kweli. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele (Lk.24:34; Ufu.1:6). Pasaka ni “sherehe ya sherehe zote.” Sherehe hii tunaiadhimisha kwa majuma saba. Majuma haya saba Mama Kanisa anayaita “kipindi cha Pasaka”. Hitimisho lake ni Sherehe ya Pentekoste. Kila jumapili ya mwaka ni Pasaka ya Bwana, kwani Kanisa huadhimisha kifo na ufufuko wake. Hii ni kuonyesha kuwa Imani na matumaini yetu yote, msingi wake ni ufufuko wa Yesu Kristo. Ndiyo maana mtume Paulo anasema; “Kama Kristo hakufufuka kutoka wafu, basi imani yetu ni bure” (1Cor 15:14-19). Kwa ufufuko wa Yesu Kristo, njia ya kwenda mbinguni kwa Baba imefunguliwa. Ndivyo maana mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali akituombea kwa matumaini akisema; “Ee Mungu, umetufungulia mlango wa milele kwa njia ya Mwanao wa pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaodhimisha kufufuka kwake Bwana wetu, tufufuke katika nuru yako kwa kufanywa wapya na Roho wako.” Hivyo ni siku ya furaha. Ni siku ya shangwe kama wimbo wa katikati unavyoimba; “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tuishangilie na kuifurahia” (Zab 118:24).
Somo la kwanza ni la Matendo ya Mitume (Mdo.10:34; 37-43). Somo hili ni hotuba ya Mtume Petro akiwa nyumbani kwa Kornelio Jemedari wa jeshi la Kirumi aliyekaa katika mji wa Kaisaria. Kornelio alikuwa mtu mwadilifu na mkarimu kwa maskini. Alipata maono akiagizwa atume wajumbe waende katika mji wa Yafa alikokuwako Petro akisali, amualike ili aje kuwahubiria habari za Kristo mfufuka. Mungu alimwarifu Petro kwa njia ya ndoto kuwafuata wajumbe wa Kornelio na kwenda nao nyumbani kwake. Petro anatii licha ya kuwa ilikuwa ni kinyume na sheria ya kiyahudi ya kuingia katika nyumba za wapagani na kula pamoja nao. Petro alipoingia nyumbani kwake, Kornelio alimkaribisha na kumwambia; tupo hapa kusikiliza ujumbe ambao Mungu amekupa kwa ajili yetu (Mdo 10:33). Petro akawaeleza habari za kuja kwake Yesu Kristo duniani; jinsi alivyohubiri katika nchi ya Palestina na kutenda mema na miujiza mbalimbali, akiponya watu magonjwa yao ya kimwili na kiroho. Lakini alihukumiwa kifo cha msalaba pasipo na hatia (Mdo 10:39), na siku tatu baada ya kifo chake Mungu alimfufua kutoka wafu (Mdo 10:40). Petro akasisitiza kuwa Mitume ni mashahidi wa tukio hilo, maana walikula na kunywa naye baada ya kufufuka kutoka wafu. Na kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi. Ujumbe huu ndio kiini cha mafundisho msingi ya Kanisa tangu enzi za mitume hata leo. Ufufuko wa Yesu ni nguzo kuu ya imani yetu (1Kor 15:14). Katika dominika ya ufufuko wa Bwana, Misa ya mchana, Mama Kanisa ameweka masomo mawili ya kuchagua kwa somo la pili. Linaweza kusomwa somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4) au somo la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 5:6-8).
Katika somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4), mtume Paulo anayaweka wazi matunda ya ufufuko, kufanywa upya na kurudishwa katika maisha ya kweli katika Kristo. Hii inaonyesha jinsi gani sikukuu ya pasaka ilivyo na maana kubwa! Lakini kufufuka huku katika maisha mapya katika Kristo kusipofanyika ndani ya mioyo yetu, furaha yetu ya pasaka ni bure. Katika Ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristo; tukaahidi kumfuata daima katika taabu na raha. Yatupasa kuishi kadiri ya ahadi hiyo tukiacha mabaya na kutenda mema. Mtume Paulo anasisitiza kuwa mawazo yetu yalenge mambo ya mbinguni, na siyo ya duniani. Hii haimaanishi kuwa tupuuze ukweli wa maisha. La hasha! Tunapaswa kuchapa kazi na kujibidisha katika kuleta maendeleo katika maisha yetu. Maana asiyefanya kazi hapaswi kula. Lakini yote yanapaswa kutendwa kwa sifa na utukufu wa Mungu.Katika somo la Waraka wa Kwanza kwa Wakorintho (1 Kor. 5:6-8), Mtume Paulo anatufundisha kuwa; Kabla ya kula mwana kondoo wa Pasaka, Waisraeli walitoa chachu yote ya zamani nyumbani mwao kwa kujipatanisha wao kwa wao, na kujipatanisha wao na Mungu. Tendo hili ni alama ya kuacha maisha mabaya ya zamani na kuanza maisha mapya, maisha mema. Anasema hivi; “Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo. Basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”
Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:1-9). Sehemu hii ya Injili inasimulia ukweli mkuu wa imani yetu kwamba Kristo amefufuka. Ushahidi ni wazi: Kaburi li tupu, vitambaa alivyolalia vimezongwazongwa, na baadaye akajionyesha kwa wafuasi wake. Yesu amefufuka kweli, ameshinda dhambi na mauti. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatualika kusherehekea kwa moyo wa furaha akisema; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka kwa furaha ya sikukuu ya Paska, Kanisa lako linazaliwa upya na kulishwa kwa sadaka hizi.” Nao utanguli unashuhudia kuwa ni “shangwe kubwa zaidi; kwa kuwa Kristo ametolewa sadaka awe Paska yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za ulimwengu, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake. Na kwa sababu hiyo, watu wote wanaitukuza sikukuu ya Pasaka kwa furaha kubwa po pote duniani. Nao Malaika wote wa mbinguni wanaimba wimbo wa kukutuza, wakisema bila, mwisho.” Mama Kanisa anatualika tufurahi kwa sababu Pasaka ni siku ya Msamaha na furaha ni tunda la msamaha. Kwa kifo na ufufuko wa Kristo, Mungu ametusamehe dhambi zetu. Siku ya Pasaka ni siku ya kuwasamehe waliotukosea, ni siku ya kutua mizigo ya watu tuliowabeba kwa muda mrefu. Ni siku ya kuwatua na kusema acha tu, imetosha. Ni mda muafaka wa kusema pamoja na Yesu; Baba wasamehe maana hawakujua walitendao (Lk 23:34). Ni kweli inawezakuwa tumeonewa, na tumetendewa vibaya. Lakini maumivu ya kutunza hasira na kutaka kulipiza kisasi ni mabaya zaidi, maana ni moja ya sababu ya magonjwa yasiyo na tiba. Tumwombe Mungu atulegezee mioyo wetu tuweze kuwaachilia hao mikononi mwake, yeye awabebe kwa niaba yetu. Tuwasamehe hata kama hawajaomba msamaha.
Pamoja na hayo, Pasaka ni siku ya Upatanisho. Kwa kufa na kufufuka kwake, Kristo ameturudishia uhusiano wetu na Mungu. Mtume Paulo anasema; “Mungu alikuwa ndani ya Kristo akiupatanisha ulimwengu wote naye…na akatuachia neno la Upatanisho” (2Kor 5:19). Kama kulikuwa na kutoelewana kati yetu; katika familia zetu na jumuiya zetu. Mlo wa Pasaka ni muda wa kukaa pamoja, kula kindugu ili kujipatanisha maana siku zetu hapa duniani chache na mda wetu ni mfupi. Zaidi sana Pasaka ni siku ya Mwanzo Mpya. Tunapoadhimisha sikukuu ya Pasaka ni vyema umwambie adui yako tuanze upya. Ni siku ya kumwambia uliyemkosea, samahani tuanze upya. Ni siku ya kuambiana tuanze upya. Ni siku ya kuanza upya katika maisha yako. Ni kwa kuanza upya tutamshuhudia Kristo mfufuka kila mahali kama Mitume walivyomshuhudia kila walipokwenda. Tukifanya hivyo tutaishi kwa furaha na amani, tukiimba na kushangilia tukisema, Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya, tufurahi na tushangilie. Tumsifu Yesu Kristo!