Tafakari Dominika ya Nne ya Kwaresima: Uzima wa Milele
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima mwaka B wa Liturujia ya Kanisa. Ni siku ya ishirini na sita ya kujitakatifu. Ni Dominika ya furaha kama wimbo wa mwanzo unavyoimba; “Furahi Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake” (Isa. 66:10-11). Tunaalikwa kufurahi kwa sababu Pasaka i karibu, ukombozi u karibu, upatanisho umekaribia. Ndiyo maana Mama Kanisa katika sala ya mwanzo-Koleta anatuombea hivi; “Ee Mungu, umeleta kwa namna ya ajabu upatanisho wa wanadamu kwa njia ya Neno wako. Tunakuomba utujalie bidii ya kujiweka tayari kwa ibada na imani, kuadhimisha sikukuu ijayo.” Ni katika Dominika hii altare inaweza kupambwa na rangi ya mavazi ya kiliturujia yaweza kuvaliwa ya rangi ya pinki badala ya zambarau na vyombo vya muziki vyaweza kutumika. Somo la kwanza ni la Kitabu cha pili cha Mambo ya Nyakati (2Nya. 36:14-16, 19-23). Kitabu hiki kinasimulia kwa ufupi historia ya wana Waisraieli. Somo hili limegawanyika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inatueleza juu ya misiba, balaa na majanga ambayo Mungu aliruhusu yawapate Waisraeli kwa sababu ya dhambi zao kama adhabu kwao, adhabu aitoayo Baba mwema kwa wanae. Tunasoma kuwa; “Wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana…Mungu kwa huruma yake aliwaonya na kuwasahihisha kwa njia ya manabii. Lakini hawakusikia. Badala yake waliwadhihaki na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata kusiwe na kuponya.” Matokeo ya dhambi na machukizo haya ni; Kuvamiwa na kuharibiwa kwa mji wa Yerusalemu na mataifa ya kipagani, kubomolewa kwa Hekalu lake, watu wake kuteswa mateso mengi, wengine kuuawa na wengine kupelekwa utumwani. Huko utumwani, walilia kwa huzuni wakikumbuka uzuri wa kuishi nyumbani kama wimbo wa katikati unavyoimba: “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulipoketi, tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake tulivitundika vinubi vyetu, maana huko waliotuchukua mateka” (Zab.137:1-6).
Sehemu ya pili inaeleza kuwa wakiwa utumwani, Waisraeli waliyatambua makosa yao, wakayakiri na kuyajuta na kuomba msamaha kwa Mungu. Majuto na masikitiko yao yanajidhihisha pale walipoambiwa waimbe baadhi ya nyimbo za Sayuni wakiwa ugenini, nao wakasema: “Tuuimbeje wimbo wa Bwana katika nchi ya ugeni?” Basi wakamlilia Mungu kwa viapo vya maneno mazito wakisema; “Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, mkono wangu wa kuume na unyauke, ulimi wangu na ugandamane na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.” Ni majuto ya hali ya juu kabisa yanayotoka ndani ya mtima wa mioyo yao. Sehemu ya tatu ya somo hili inaeleza ukuu wa huruma na upendo wa Mungu kwa anayekiri na kutubu makosa yake. Waisraeli walipotambua na kukiri dhambi zao, Mungu aliwahurumia, akawasamehe dhambi zao na kuwarejesha katika nchi yao kwa mkono wa Koreshi, mfalme wa Uajemi. Nasi tukiyatambua makosa yetu, tukakiri dhambi zetu na kuomba msamaha kwa moyo wa majuto, Mungu Baba yetu atatuhurumia na kutusamehe. Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso (Efe. 2:4-10). Katika somo hili mtume Paulo anashuhudia kuwa sisi tumekombolewa kwa upendo na huruma ya Mungu kwa mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Nasi tunashirikishwa ukombozi huu kwa njia ya ubatizo. Kabla ya ubatizo tulikuwa kama wafu sababu ya dhambi. Ni kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo tumezaliwa upya na kuvalishwa uzima mpya na wa milele. Kwa ubatizo tunaishi pamoja na Kristo, tumefufuliwa na tumeokolewa naye. Mtume Paulo anatukumbusha kuwa hatukukombolewa kwa mastahili ya matendo yetu, bali kwa Neema ya Mungu. Na matendo mema tunayoweza kutenda ni ishara kwamba, neema ya Mungu inafanya kazi ndani mwetu. Basi hatuna budi kumshukuru kwa kujitahidi kutenda matendo mema kwa kuwahudumia wengine.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 3:14-21), nayo imegawanyika katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza (Yn. 3:14-15); inatukumbusha tukio la kuinuliwa kwa nyoka wa shaba na Musa jangwani. Itakumbukwa kuwa, Waisraeli baada ya kutoka utumwani Misri, wakiwa jangwani kuelekea nchi ya ahadi walikosa imani kwa Mungu, wakamnung’unikia. Mungu aliwaadhibu kwa kuwatuma nyoka wa moto wakawauma na watu wengi wakafa. Nao walipotambua kosa lao, walimlilia Musa awaombee msamaha kwa Mungu. Mungu akasikia kilio chao, akawahurumia, akawasamehe. Ndipo akamwamuru Musa atengeneze nyoka wa shaba na amtundike juu katika mti, ili yeyote atakaye umwa na nyoka wa moto, akimtazama nyoka wa shaba aweze kupona. Lakini ifahamike kuwa, sio nyoka wa shaba aliyewaponya, bali ni utii na imani yao kwa Mungu. Nyoka wa shaba alikuwa ni ishara tu kwao (Hek 16:5). Zaidi sana hii ilikuwa ni ishara ya kuinuliwa kwa Yesu Kristo msalabani “ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.” Nasi kila tumtazamapo Yesu Kristo aliyetundikwa msalabani kwa imani, tunapata uzima wa milele. Sehemu ya pili (Yn. 3:16-18) inaeleza upendo wa Mungu kwa mwanadamu uliomfanya amtoa Mwanawe wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Na sehemu ya tatu (Yn. 3:19-21) inaeleza ukinzani uliopo kati ya maisha ya nuru na maisha ya giza. Ukinzani huu ndio unaotoa hukumu. Na hukumu yenyewe ndiyo hii; “Nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.”
Mafundisho haya yanatokana na mazungumzo kati ya Yesu na Nikodemo, Farisayo, mmoja wa baraza mkuu la Wayahudi, yaani “Sanhedrin”, ndilo baraza la juu kabisa la utawala lililoundwa na wazee 70 pamoja na Kuhani Mkuu. Nikodemu alimwendea Yesu usiku kwa kujificha (Yn. 3:1-13), akiogopa asifahamike kuwa ni mfuasi wake. Aliogopa kufahamika kuwa yeye ni mtu wa nuru, mtu wa haki anayetenda mema, anayempendeza Mungu, anayeshika amri na maagizo yake. Hivyo anaamua kuenenda katika giza. Hali hii inawezamkuta mtu yeyote. Tukifanya hivyo, Yesu anatuambia tumekwisha kuhukumiwa. Iko hivi, ukipenda maisha ya giza, unamilikiwa na Ibilisi, unakuwa mtumwa wake. Naye akishakuchukua mateka anakutenda jeuri kadiri anavyotaka na anavyopenda. Atahakikisha amekuchakaza vilivyo, naye hatakuacha mpaka pale utakapotubu na kuirudia nuru ya kweli, Yesu Kristo, Bwana na mkombozi wa maisha yetu. Tujitahidi basi kuishi maisha ya Nuru ili tuwe watu wa amani na furaha. Nikodemu alimwendea Yesu kwa kificho kwa kuogopa kupoteza kazi, cheo, mali na heshima yake mbele ya watu. Nasi tunaweza kufanana naye tunaposhindwa kuuishi ukristo wetu ipasavyo, kuogopa kukemea maovu, kusimamia mafundisho ya imani yetu, kuuminya ukweli, kupindisha amri za Mungu na sheria za Kanisa ili tupendwe na watu, tuonekane wazuri na wema mbele zao. Tukumbuke kuwa Mungu anajua yote hata mawazo yetu, hadanganywi wala hadanganyiki. Tuuishi ukristo wetu, tuishuhudie kweli nasi tutakuwa huru. Nikodemu baada ya kuelewa maana ya fumbo la umwilisho na mateso ya Yesu akawa na ujasiri na nguvu ya kumshuhudia Kristo hata kumtetea waziwazi mbele ya Baraza la wasiohaki (Yn. 7:50-53). Na baada ya kifo chake alinunua manukato na manemane ratili mia kwa ajili ya maziko yake (Yn 19:39). Kwa kuwa imani bila matendo, imekufa (Yak 2,17). Basi, imani yetu na idhihirishwe katika maisha yetu ya kila siku tukimshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu ili tupate kustahilishwa kupata uzima wa milele. Nayo sala baada ya komunio anayotuombea Mama Kanisa akisema; “Ee Mungu, unayemtia nuru kila ajaye ulimwenguni humu, tunakuomba uitie mioyo yetu nuru ya neema yako, tuweze kuwaza daima yakupendezayo wewe Mwenyezi na kukupenda kweli”, itupe nguvu na hamu ya kumwamini siku zote Bwana na Mwokozi wetu aliyeinuliwa juu msalabani ili tupate uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo.