Mtume Paulo anatufafanua Fumbo la Agano Jipya na la milele lililosimikwa juu ya Msalaba. Mtume Paulo anatufafanua Fumbo la Agano Jipya na la milele lililosimikwa juu ya Msalaba.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tano ya Kwaresima Mwaka B: Agano Jipya Na La Milele

Mtume Paulo anatufafanua Fumbo la Agano Jipya na la milele lililosimikwa juu ya Msalaba. Mateso, na kifo cha Yesu vinaonyesha kuwa Yeye alikuwa kweli wakili na kuhani wetu. Utii wake ulimpendeza Mungu, hata ukaleta wokovu kwetu. Yesu alitolea maisha yake, dua na maombi na kulia sana na machozi, akawa mtii, akavumilia mateso hata kufa Msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani ili kuambata huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya tano ya Kipindi cha Kwaresima mwaka B wa Kiliturujia wa Kanisa, siku ya 33 ya kujitakatifu. Zimebaki siku 7 tuingie Juma Kuu. Pasaka imekaribia, tutakapoadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwan wetu Yesu Kristo, ndio ushindi wake dhidi ya dhambi na mauti. Mama Kanisa kwa siku arobaini za kipindi cha Kwaresima anatuhimiza kwa kurudia tena na tena mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali zaidi, kusoma na kutafakari neno la Mungu na kutenda matendo ya huruma kwa upendo, Ndiyo maana katika sala ya Mwanzo anatuombea hivi; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utusaidie tuwe na mapendo kama ya Mwanao, aliyeipenda dunia hata akajitoa auawe”. Tukifanya hivyo tutaweza kuimba na mzaburi wimbo huu wa mwanzo tukisema; “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe Mungu ndiye uliye nguvu zangu (Zab.  43:1-2). Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Yeremia (Yer. 31:31-34). Katika somo hili Mungu anaahidi kufanya Agano Jipya na la milele, Agano ambalo kwalo anaahidi kuwasamehe watu uovu wao, wala hataikumbuka tena dhambi yao. Kwa Agano hili jamii yote ya wanadamu itajazwa Roho Mtakatifu na kuwezeshwa kumjua Mungu kama Baba mwema na hivyo kupata ujasiri wa kusali na kuomba kama mzaburi katika wimbo wa katikati akisema; “Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu, unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, wala roho wako mtakatifu usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako, unitegemeze kwa roho ya wepesi nami nitawafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watarejea kwako” (Zab. 51:1-2, 10-13). Huu ni utabiri wa Agano Jipya alilokuja kulifanya Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, ndilo ukamilifu wa Agano la Kale. Kwa kumtuma Mwanawe, Mungu amefanya nasi Agano la milele, na kwa njia ya hilo ametusamehewa dhambi zetu. Tena ametupatia Roho Mtakatifu anayetutia roho mpya kila mara katika sakramenti ya kitubio. Ni mwaliko wa kufanya toba na kujipatanisha na Mungu.

Wokovu wa mwanadamu umetundikwa juu ya Msalaba
Wokovu wa mwanadamu umetundikwa juu ya Msalaba

Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Waebrania (Ebr. 5:7-9). Katika somo hili Mtume Paulo anatufafanua Fumbo la Agano Jipya na la milele lililosimikwa juu ya Msalaba. Mateso, na kifo cha Yesu vinaonyesha kuwa Yeye alikuwa kweli wakili na kuhani wetu. Utii wake ulimpendeza Mungu, hata ukaleta wokovu kwetu. Yesu alitolea maisha yake, dua na maombi na kulia sana na machozi, akawa mtii, akavumilia mateso hata kufa Msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn.12:20-33). Katika sehemu hii ya Injili kuna mambo makuu matatu. Jambo la kwanza ni Wayunani waliokwenda Yerusalemu kuhiji, wanamuomba Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya awasaidie waweze kumuona Yesu. Ilikuwa hivi: wakati wa Yesu wayahudi wengi waliishi uhamishoni, nje ya Palestina, nao walijulikana kama Wayahudi wa Diaspora. Popote walipokuwa walijenga masinagogi kwa ajili ya kusali na kusoma neno la Mungu. Watu wa mataifa yaani wapagani walivutiwa na namna ya ibada zao kwa jinsi zilivyojaa uchaji kwa Mungu, tofauti na ibada za kipagani. Hivyo wengi walijiunga na dini ya kiyahudi, wakajifunza maandiko matakatifu, namna yao ya kusali na wakawa wanashika mila na tamaduni za kiyahudi kama vile kwenda kuhiji Yerusalemu wakati wa sherehe kubwa za kiyahudi. Wapagani walioingokea dini ya kiyahudi waliitwa waproseliti (Proselytes) yaani WachaMungu au Watu waliokuja karibu na Mungu (Mdo.2:10). Mfano ni Nikolaus wa Antiokia, mmoja kati ya Mashemasi saba (Mdo 6:5) na Kornelio afisa Jeshi wa Kirumi (Mdo 10:11-12). Kundi hilo la wachaMungu ndilo lililokuja kuhiji Yerusalemu. Watu hawa Yohani anawaita Wayunani au Wagiriki. Hao ndio waliokuwa na shauku ya kumwona Yesu. Filipo alipomwambia Andrea juu ya hamu ya Wayunani hao kumuona Yesu, kisha walimwambia Yesu.

Ee Mungu unirehemu mimi sawasawa na fadhili zako
Ee Mungu unirehemu mimi sawasawa na fadhili zako

Jambo la pili ni jibu la Yesu kwa ombi la Wayunani kutaka kumwona. Yesu hatoi jibu la ndio au hapana. Kinyume chake anaeleze kiini cha fumbo la umwilisho kuwa ni fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu anaweka wazi kuwa saa imefika ya mwana wa Adamu kutukuzwa. Kadiri ya Yohana, “Saa ya Yesu,” ni mateso, kifo na ufufuko wake. Zao la matendo haya makuu ni wokovu wetu. Tukitaka kufaidi wokovu huo, yaani uzima wa milele, yatupasa kufuata njia ya mateso kama Kristo. Ni katika muktadha huu jambo la tatu linajitokeza nalo ni ushuhuda wa Mungu Baba kumtukuza mwanae Yesu Kristo, naye Yesu kumtukuza Mungu. Kumbe hamu ya Wayunani kumwona Yesu ingetimia kwa wao kuwa wafuasi wake, kuwa tayari kukishiriki kikombe chake, kukataliwa, kuteswa na kuuawa. Lakini hatima ya yote ni kushiriki taji ya utukufu mbinguni pamoja naye. Katika kutabiri kifo chake Yesu anasema; “chembe ya ngano isipoanguka chini ikafa, hubaki hivyo hivyo ilivyo peke yake, bali ikifa hutoa mazao mengi.” Sisi ndio mazao ya mateso, kifo na ufufuko wake Yesu Kristo. Tukitaka kufaidi wokovu huu yaani uzima wa milele, yatupaswa kumtumikia Kristo kati ya ndugu zetu. Maana yeye mwenyewe anasema; “Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu”. Sisi kwa ubatizo, kwa njia ya maji na Roho Mtakatifu tumefanya Agano na Mungu, tumezaliwa upya, tumekuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa. Agano hili limeandikwa ndani kabisa mwa Roho zetu, tumetiwa mhuri usiofutika milele.

Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba
Wokovu wetu umetundikwa juu ya Msalaba

Kwa kumkataa shetani na mambo yake yote na fahari zake zote, tumejiweka katika himaya ya mwenyezi Mungu. Lakini hii haina maana kuwa hatutakumbana na mateso na mahangaiko. Bali tunakuwa na nguvu ya kuyashinda. Yesu mwana wa Mungu alipokabiliana na mateso, kwa huzuni alisali na kuomba: “Baba chochote chawezekana kwako, ikibidi niondolee kikombe hiki. Lakini mapenzi yako yatimizwe. Mateso yalipozidi alilia kwa uchungu: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha” (Mk 15:34). Mwishoni aliyakubali mateso na kusema: “Baba, Mikononi mwako naiweka Roho yangu” (Lk 23:46). Nasi pia katika mateso na mahangaiko ya kila siku tujikabidhi kwa Mungu. Tumwombe atupe nguvu na ujasiri wa kuyakabili majukumu na mahangaiko ya maisha yetu kwa uvumilivu, huku tukitafuta kuyatimiza mapenzi yake. Basi tuchunguze dhamiri zetu ili tujue kama kipindi hiki cha kwaresima kimetuletea matunda mema ya kiroho au bado tumezama katika kilindi cha dhambi. Kama bado, huruma na upendo wa Mungu navyo bado vinatusubiri. Tufanye hima kuijongea kwa ujasiri Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya utakaso, Sakramenti ya upatanisho, Sakramenti ya ungamo la dhambi, tujipatanishe na Mungu na wenzetu. Tukifanya hivyo tutajiweka tayari kushereheka vyema Pasaka ya Bwana kwa ajili ya wokovu wetu na wa ulimwengu. Ndiyo ananyotuomea Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu kwa matumaini makubwa akisema; “Ee Bwana, tunakutolea kwa furaha dhabihu ziletazo wokovu wa milele. Tunakuomba sana utusaidie kuziheshimu kwa moyo wote na kuzitoa vema dhabihu hizi kwa jili ya wokovu wa ulimwengu”. Huku ndiko kumpendeza Mungu kwa ajili ya uzima wetu wa milele kama sala baada ya Komunyo inavyosisitiza; “Ee Mungu, unayemtia nuru kila mtu ajaye ulimwenguni humu, tunakuomba uitie mioyo yetu nuru ya neema yako, tuweze kuwaza daima yakupendezayo wewe Mwenyezi na kukupenda kweli”. Na hii ndiyo hamu ya mioyo yetu. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 5 Kwaresima
13 March 2024, 10:28