Tafakari Dominika ya Tatu Kwaresima Mwaka B: Nyumba ya Sala na Sadaka!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji leo Kanisa liaadhimisha Dominika ya 3 ya Kwaresima Mwaka B wa Kanisa. Himizo kubwa katika kipindi hiki cha Kwaresima ni toba na wongofu wa moyo na muunganiko na Mungu kwa njia ya sala. Yesu Kristo anapowakemea watu akisema, “Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara”, hamaanishi hekalu kama jengo tu, bali ibada safi ya mioyo mikunjufu ya sisi wanadamu mbele ya Mungu. Je, mioyo yetu ni mapango ya biashara huria? Mawazo haya yanasindikizwa na ujumbe wa Kwaresima wa Baba Mtakatifu Francisko anaposema “Mtazamo wa kutafakari wa maisha, ambao aktika kipindi cha Kwaresima utatuwezesha kugundua tena, utatuhamasisha nguvu mpya. Katika uwepo wa Mungu tunakuwa kaka na dada, hapa tunaona na kuhisi kuwa wengine wanapata nguvu mpya katika Maisha ya Imani na jamii: badala ya vitisho vya maadui, tunapata misaada na masahaba katika safari.” Hii ni ndoto ya Mungu, kututifikisha katika nchi ya ahadi ambayo tunajitahidi wakati huu wa siku 40 tunatoka utumwani. Mfumo wa Kanisa ambao katika miaka ya hivi karibuni tumekuwa tukiutambua na kuhimizwa nao, unaonyesha kwamba Kwaresima pia ni wakati wa maamuzi ya jamii, ya chaguzi ndogo na kubwa ambazo zinakwenda kinyume na wimbi la haki za watu na utu wa mwanadamu, wimbi hili lenye uwezo wa kubadilisha maisha ya kila siku ya watu na maisha ya jirani: tabia za ununuzi, utunzaji wa uumbaji, kuingizwa kwa wale ambao hawaonekani au kudharauliwa zinakomeshwa na kubadilishwa na kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri ya kuishi na kaendelea kuchuchumilia utakatifu ulio wito wetu wa msingi.
UFAFANUZI: Neno la Mungu leo linatuelekeza kutafakari kwa kina namna tunavyoyatumia mazingira yetu ya sala hasa jinsi tujiwekavyo mioyo yetu wakati wa sala ikumbukwe sala ni moja ya mafundisho matatu wwakati wa kwresma (Kufunga, sala na matendo ya huruma ka wahitaji). Injili tuliyoisikia hivi punde ni simulizi kwamba Yesu anachukua jukumu la kuwafukuza watu hekaluni. Ni watu ambao walilitumia vibaya hekalu. Ili kuweza kuelewa vizuri tukio hili nawaalikeni tulitazame hekalu la Yerusalemu ambalo lilikuwa ndilo kitovu cha imani kwa Wayahudi. Kila Myahudi alilazimika kufika katika hekalu hili walau mara moja kwa mwaka hasa wakati wa Sikukuu ya Pasaka, kwa ajili ya kusali. Hivyo hekalu lilikuwa ni sehemu muhimu kwa ajili ya sala na sadaka kwa Wayahudi. Ilikuwa ni nyumba ya Mungu kwa ajili ya sala (Somo I. Kut 20:1-17) Hekalu hili liligawanyika katika sehemu kuu tano. Sehemu ya kwanza ilikuwa na ua mkubwa uliozunguka majengo ya ndani. Katika ua huo watu wasio Wayahudi waliruhusiwa kuingia na hivyo walipasika kusali wakiwa sehemu hiyo tu. Ilikuwa ni marufuku kabisa kwa asiye Myahudi kwenda mbele ya hapo. Endapo mmoja angejifanya mbishi na akadiriki kwenda zaidi ya hapo, basi adhabu yake ilikuwa kifo. Sehemu ya pili ilikuwa ni kwa ajili ya wanawake wa Kiyahudi. Sehemu ya tatu ilikuwa ni kwa ajili ya wanaume wa Kiyahudi. Sehemu ya nne ilikuwa ni altare iliyofikiwa na makuhani. Na sehemu ya tano ilikuwa ni patakatifu pa patakatifu, mahali ambapo palifikiwa na kuhani mkuu tu tena mara moja kwa mwaka, siku ya utapatanisho.
Ndugu zangu katika Kristo, katika sehemu hizo tano za Hekalu la Yerusalemu; sehemu ambayo ilitia fora ni ile sehemu ya kwanza kwani ilikuwa na pilikapilika nyingi. Licha ya kwamba ilikuwa ni sehemu ya sala kwa ajili ya watu wasio Wayahudi lakini ilikuwa ni sehemu ya biashara pia. Kulikuwa na hoja za msingi za kufanyika kwa biashara sehemu hiyo. Sehemu hiyo kila aliyeingia au kufika hekaluni alipita hapo. Tena, kutoa sadaka ilikuwa ni lazima kwa Wayahudi. Walitakiwa kutoa sadaka za wanyama kama ng’ombe, kondoo na njiwa lakini wenye ubora wa hali ya juu. Hivyo, biashara ilifanyika hapo ili kuwasaidia wale waliotoka mbali waweze kuja na fedha tu na kupata wanyama hao katika mazingira yale. Isitoshe, sehemu hii ya hekalu ilikuwa nu sehemu ya kubadilisha fedha ya kirumi ili kupata fedha ya kiyahudi kwa ajili ya zaka. Kwa jinsi hii nyumba ya Mungu ilifanywa kuwa nyumba ya biashara. Uharamu wa biashara zilizokuwa zikiendelea hapo hekaluni ni kuwa mfumo wa biashara ulikuwa ni kwa ajili ya kuwatajirisha waandishi na mafarisayo, (hata leo tunaona sehemu nyingi bado ale watu wenye Madaraka na nguvu ya pesa wanaenelea kutajilika na wasio nacho wanaendelea kuwa masikini) hawa waandishi na mafarisayo amabo wakikuwa ni viongozi-kwani kwa kiasi kikubwa wao ndio walikuwa wamiliki wa zile biashara (hata leo viongozi wengi ndio wamiliki wa biashara kubwa na makampuni). Hivyo walitengeneza faida kubwa kwa kuuza wanyama kwa bei ya juu na kubadilisha fedha kwa viwango visivyolingana. Zilikuwa ni biashara zenye ulanguzi mkubwa.
Katika Injili (Yoh 2:13-25) Kikubwa zaidi kilichoibua hasira ya Yesu ni pale ambapo biashara ilipewa kipaumbele zaidi eneo hilo na kuwavunjia wengine haki yao ya kusali. Ni ulanguzi na kuwanyima wengine mazingira mazuri ya sala ndivyo vilivyomfanya Kristo awatoe wale watu hekaluni. Hivyo, Kristo akasema wazi “Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara." Ndugu wapendwa katika Kristo, Hekalu (kwa mtazamo wa Kiyahudi) au Kanisa (kwa mtazamo wa Kikristo) ni mahali patakatifu palipotengwa rasmi na kuwekwa wakfu au kubarikiwa kwa ajili ya lengo maalumu la kumwabudu Mungu. Ni mahali ambapo mtu hukutana na huonja uwepo wa Mungu. Nabii Habakuki alisema “Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake Takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele yake” (2:20). Hivyo ni sehemu inayohitaji utulivu mkubwa ili watu waweze kusali kwa amani. Ni mahali ambapo mawazo ya mtu hutakiwa yaelekezwe kwa Mungu. Kisiwepo chochote kile kitachoweza kuharibu mawazo ya mtu awapo Kanisani. Matumizi yoyote ya nyumba ya Ibada kwa shughuli isiyo ya kiibada hayakubaliki. Kwa kusema kuwa “msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa pango la wanyang’anyi” Yesu alitaka kusisitiza kuwa Mungu ndiye mmiliki wa mioyo yetu ambako ibada ya kweli inapaswa kufanywa. Hivyo, Kwa kulitakasa hekalu hili la “wafanyabiashara” Yesu alitangaza kuwa utawala wa Masiha umeshaanza na hivyo alilaani mchanganyo wowote ule kati ya dini na maslahi ya kiuchumi. Hapa anawajibika kibinadamu lakini akilenga kudhihirisha umungu wake.
Ili kuweza kusali vizuri na kwa utulivu, tunahitaji si tu mazingira mazuri ya nje bali zaidi tunahitaji utulivu ndani ya mioyo yetu. Ndiyo maana Kristo mwenyewe ameufananisha mwili wake na Hekalu. Ndivyo nasi tulivyo. Miili yetu ni hekalu. Tena Mtume Paulo anatuambia wazi kuwa Kristo ni kichwa cha mwili wake yaani Kanisa, nasi ni viungo vya huo mwili. Ndio kusema, nasi tunatakiwa tuwe “makanisa” ambamo ndani yetu sala ziendeshwe. Mioyo yetu iwe ni nyumba ya sala. Ndio maana hata Kristo mwenyewe katika mazungumzo yake na yule mwanamke Msamaria alikazia kuwa uabudu halisi ni ule ulio katika Roho na Kweli (Yoh 4:24). Je, tuwapo Kanisani au wakati wa sala hatuendeshi pia biashara mioyoni mwetu. Tupo tunaofanya “biashara” ya mambo ya kiuchumi ambayo tunataka tukayatekeleze mara tu baada ya kutoka hapa Kanisani. Wengine tunatumia muda wa sala kujikumbusha juu ya mambo ya darasani. Ndio maana kuna wakati mtu akitoka nje ya Kanisa hata ukimwuliza Injili ya leo imesomwa na nani, ilihusu nini? Kwake hilo ni swali gumu kwani wakati wa sala yeye alikuwa na “biashara yake” ikiendelea. Tutambue kuwa daima Yesu anaingia mioyoni mwetu na anatuona nini tunakifanya humo, kama ni majungu, tamaa, au tunapiga michapo tu, vyote hivyo Yeye huviona. Je, tunasubiri Yesu atengeneze bakora ili tuweze kubadilika? Hebu tumpe Kristo nafasi wakati huu wa Kwaresma atufanye tuwe watu tunaoyaheshimu Makanisa na tunaowapa wenzetu mazingira yasiyo na makwazo wawapo Kanisani ili waweze kusali vizuri.
Leo hii tunashuhudia mambo mengi ambayo yanaharibu umaana wa Kanisa kama nyumba ya Ibada. Tazama aina za nguo na mivao mbalimbali ya watu waendapo kanisani. Ndio kusema wapo wanaofanya biashara za matangazo wawapo kanisani. Tena, hata aina ya vipodozi vitumikavyo, kuna vingine vinawafanya wengine washindwe kuvumilia kuwepo kanisani. Tupo pia wengine tunaoamua kufanya biashara ya usingizi kanisani. Wengine tunaamua kuacha simu zetu “on” hata kama milango mingi imewekwa matangazo kwa herufi kubwa “ZIMA SIMU”. Hata kwaya zetu nyingi siku hizi zinafanya biashara ya nyimbo zaidi kuliko liturjia, ndio maana nyimbo nyingi si za Kiliturujia. Huku ni kuwakosea haki wengine. Kauli mbiu ya kipindi hiki cha Kwaresima ni kutubu na kuiamini Injili. Ili tuweze kuitekeleza kauli mbiu hiyo vizuri kuna mengi ya kuyafanya. Mojawapo ni hili la kuachana na “biashara” mbalimbali zinazoendelea mioyoni mwetu (jiulize biashara yako ni ipi. Inaendanda na amri za Mungu au ni kinyume, inafuata sheria za jamii au kinyume?) ili tuweze kujipatia msamaha wa dhambi na utakaso na hivyo Injili au ujumbe wa Injili utazidi kustawi ndani yetu. Sisi wenye maisha ya wakfu (mapadre, mashemasi, watawa) na viongozi wengine watarajiwa wa Kanisa (waseminari) tujihoji je, kwetu Kanisa ni kituo cha kupata maslahi binafsi ya kiuchumi au ni kwa ajili ya kuwasaidia watu waabudu na kusali na kwa utulivu? Sheria ya Kanisa namba 1221 inatukataza kuwatoza watu malipo kama kiingilio kanisani muda wa sala na ibada je sisi hatufanyi hayo kama hatufanyi heri kwetu kama kuna sehemu tulianguka na tukajikuta wajasiliamali wa wambo ya kiroho, na imani basi tutubu na kuiamini injili. Tukiyatimiza hayo, hakika hatutaifanya nyumba ya Baba yetu wa Mbingu yaani sehemu za Ibada na sala na mioyo yetu iliyo hekalu la Roho Mtakatifu zitakuwa ni sehemu nzuri kwa ajili ya sala.