Tanzania:Wavincent watengeneza nafasi ya Mungu licha ya kukosa nafasi!
Na Francesca Merlo–Morogoro,Tanzania na Angella Rwezaula-Vatican.
Wamisionari wa kwanza wa Mtakatifu Vincenti wa Paulo waliwasili nchini Tanzania mnamo mwaka 1993, na tangu wakati huo, utume huo umekuwa ukiongezeka mara kwa mara. “Kutangaza Neno la Bwana” ambalo ni karama na utaratibu wa kitawa wa Shirika la Wavincent nchini Tanzania wanayofanya hadi sasa. Hatukujua la kutarajia tulipokuwa ndani ya safari ya saa tano kutoka Dar Es Salaam hadi Morogoro. Jambo ambalo kwa hakika hatukutarajia tulipofika kwenye Seminari ya Mtakatifu Vincent wa Paulo lilikuwa ni kuona maegesho ya magari yanajazwa na waseminari 41 wenye kutabasamu, kucheza ngoma,na kuimba!
“Kuja kwenu ni baraka kwetu sote,” waliimba, huku wakiweka maua shingoni mwetu na kucheza nasi kwenye jumba lao la chakula, ambapo tulikula pamoja nao. Hapo ndipo tulipogundua kwa mara ya kwanza kwamba kunaweza kuwa na tatizo. Waseminari walijazana kuzunguka meza zao ndogo za mduara, wakibanana iwezekanavyo kwenye viti kila moja ili na sisi pia, tuwe na meza ya kulia. Hapakuwa na nafasi ya kutosha kwa kila mtu.
Baada ya chakula cha jioni, matembezi ya haraka ya kuzungukia seminari—hata gizani, unaweza kutambua kuta zake zilizopakwa rangi angavu, zenye furaha, kama vile tulivyokaribishwa, au “Karibu” kwa lugha ya Kiswahili, ilivyokuwa. Wanaseminari walikuwa wamekusanyika wote kutazama Ligi Kuu ya Tanzania: Simba dhidi ya Singhita Fountain Gate kwenye chumba cha mapumziko; wale waliobahatika walipata viti na wengine walikuwa wamesimama nyuma.
Tulitembea kwenye korido na kufika kwenye kikanisa, kila kiti kikiwa na vitabu na kalamu za waseminari, kila sehemu ilikuwa na mtu na wa mwisho kufika alipata viti nyuma. “Hatujui mahali pa kuwaweka,” alisema Padre Mushi, Mkuu wa Seminari hiyo. Kwa hiyo alielekeza kwenye viti vilivyokuwa nyuma ya kikanisa kwamba: “Hawa wamejaa, lakini mtu mpya akifika, hawana mahali pa kukaa.”
Kiukweli, pia alitoa maoni yake Padre Yuda, Mkuu wa Kanda ya Wavincent nchini Tanzania, “katika miaka michache iliyopita, Shirika limelazimika kuwakataa vijana wa kiume kadhaa ambao walitaka kujiunga.” “Hatuna shida na miito,” alielezea, “tuna shida ya uwezo wa nafasi.” Vijana tayari wanashiriki vyumba, na wengi wao wakiwa wawili-wawili, wengine hata wanne. Wameunda familia, jumuiya ya kweli, kufuatia urithi wa baba yao mwanzilishi, na ambao hawombi mengi.
Na ingawa vijana hawa hawaombi mengi pia ni wazi kwamba wanahitaji zaidi. Katika msimu wa mvua, baiskeli zao hazipitiki kwenye udongo wenye matope hadi kwenye vyuo vikuu vyao, na wakati wa kiangazi, ukosefu wa maji hauruhusu sehemu zao za kulima mboga zao kusitawi. Kuku na bata wao hutunzwa kwa ajili ya wageni maalum kwa sababu, kama Padre Mushi alivyotania, “hawa vijana wangewamaliza hata nusu siku!” Huku wakiwa wamekaa kwenye bustani wakiponda alizeti kavu ili kutoa mbegu, ambapo hutengeza mafuta yao ya kupikia, ni wazi kwamba vijana hao wanajitosheleza kadri ya uwezo wao unavyowaruhusu.
Humphrey, ambaye anasoma mwaka wa tatu wa falsafa alinitabasamu. Kwa aibu aliniambia kuhusu safari yake ya imani na kuhusu shauku yake ya kuweka wakfu ili kuwasaidia maskini kwa unyenyekevu. Humphrey ni mfano mzuri wa unyenyekevu, kwa kujikita katika safari yake ya imani kwenye nyayo za Mtakatifu Vincent wa Paulo.
Tukiwa na Waseminari wote, tulitembelea vyumba vyao, tukitazama mabango kwenye kuta zao na vitabu vyao. Wote 41 wanashirikishana kompyuta nane, na printer moja itakuwa nzuri, walisema. Wote ni wanafunzi,na husafiri na kutumia pesa kwenye uchapishaji ambao sio rahisi kila wakati. Lakini wanafanya kila kitu kionekane kinawezekana, wakiongozwa na mkuu wao, ambaye kwa upande wake anaongozwa na mkuu wa Kanda, kila mmoja akimjali mwenzake kwa kiasi kikubwa, na hii inaakisi uwazi.
Kisha, tuliaga. Viti vilisogezwa pembeni mwa chumba, vijana hao waliingia mmoja baada ya mwingine huku wakiimba wimbo wa kiutamaduni, wakiwa wamevalia mavazi ya kiutamaduni, huku wakiimba, wakicheza na kucheka.
Bila shaka walifurahia kutumbuiza, na tulifurahia sana kutazama. Mmoja wa mashemasi waliowekwa daraja hivi karibuni alitoa hotuba ya shukrani kwetu na kikundi kikaanzisha wimbo wa “Ave Maria”kwa Kilatini(Salamu Maria) iliyopatana kabisa, na kuunganisha tamaduni mbili nzuri kuwa wito mmoja wenye nguvu.
Kanisa, Tanzania na dunia nzima wanastahili kuwa na waseminari zaidi kama hawa, na vijana hawa wanastahili nafasi ya kuishi na kujifunza ili wawe viongozi wa ajabu ambao wamekusudiwa kuwa.