Askofu Flavian Kassala: Ujumbe wa Pasaka Kwa Mwaka 2024: Sinodi na Jumuiya Ndogo ndogo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ambaye pia ni Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika ujumbe wake kwa Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa Mwaka 2024 anasema, Sherehe ya Pasaka ni mwendelezo wa safari ya tafakari ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Hii ni Pasaka inayoadhimishwa sanjari na Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kwa nchi za AMECEA kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Jumuiya ndogo ndogo za kikristo: miaka 50 ya kujenga Kanisa kama Familia ya Mungu katika nchi za AMECEA.” Kanisa kama familia ya Mungu linapata chimbuko lake katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Huu ni ufunuo wa Kanisa ambalo linasalai, linatafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili na kwamba, amani ya Kristo Mfufuka ilijaze na kulipyaisha Kanisa katika muundo wa Kisinodi na katika sura ya Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Kimsingi huu ndio mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika msingi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo.
Askofu Flavian Matindi Kassala anasema, zawadi za kisinodi yaani: Umoja, Ushiriki na Utume zinajifunua kwa wazi zaidi katika maisha na utume wa Kristo Yesu katika Fumbo la Umwilisho na kuwafanya waamini kuwa ni washirika wa kazi ya ukombozi na hivyo wanatumwa kama wamisionari kuendeleza kazi ya ukombozi. Waamini wanaendelea kusali na kumwomba Kristo Yesu aweze kulijalia Kanisa zawadi hizi za kisinodi. Hii ni Pasaka inayoadhimishwa sanjari na Sherehe za Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo ndogo katika Nchi za AMECEA. Kanisa kama familia ya Mungu linapata chimbuko lake katika Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo. Huu ni ufunuo na ushuhuda wa Kanisa ambalo: linasali, Kanisa linalotafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.
Kumbe, amani ya Kristo Mfufuka ilijaze Kanisa zima na lipyaishwe kwa muundo wa Kisinodi na katika sura ya Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Sera, mipango na mikakati ya shughuli za kichungaji Kisinodi na katika Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo ileta amani na nuru kwa waamini na kwa ulimwengu wote. Nguvu ya Kristo Mfufuka iondoe mawe ambayo ni vikwazo vinavyowafunga waamini kwenye makaburi. Ikumbukwe kwamba, Kristo Mfufuka ndiye mwenye nguvu na jeuri ya kuwaondolea mawe, hata yale mawe yanayowaogofya; ndiye anaweza kuwapatia uhuru wa kweli. Huu ni mwaliko kwa waamini kuendelea kumtafuta Kristo Mfufuka wakiwa wamebeba manukato yao. Safari ya Kwaresima kwa muda wa siku arobaini katika jangwa la maisha yao ya kiroho na ushiriki wa waamini katika kazi ya ukombozi, iwasaidie waamini waweze kuwa ni wamisionari wa Habari Njema ya Ufufuko wa Kristo Yesu, ili kwa pamoja kama familia ya Kisinodi inayojengwa juu ya msingi wa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo iweze kufikisha Habari Njema ya Pasaka kwa ulimwengu mzima.