Dominika ya Huruma ya Mungu: Furaha ya Pasaka Na Amani Moyoni
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya pili ya Pasaka mwaka B wa Kanisa. Itakumbukwa kuwa katika maadhimisho ya Jubilei Kuu mwaka 2000, dominika ya pili ya Pasaka ilipewa jina la “Dominika ya huruma ya Mungu.” Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Hii ni kusisitiza juu ya huruma ya Mungu waliyoipokea waliobatizwa usiku wa Pasaka kama wimbo wa mwanzo unavyoashiri: “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu, aleluya” (1Pet. 2:2). Ndivyo sala ya Koleta inavyosisitiza ikisema; “Ee Mungu mwenye huruma ya milele, unawasha imani ya taifa lako katika sikukuu hii ya Pasaka. Uwazidishie hiyo neema uliyowajalia (wale waliobatizwa), wapate kuelewa vema kwamba wametakaswa kwa maji, wamepata uzima mpya kwa Roho, na kukombolewa kwa damu.” Ni Mtakatifu Faustina Kowalska ndiye aliyeaminishwa kuidhihirisha huruma ya Mungu kwa maono aliyoyaona ya miali ya mwanga ya rangi nyekundu ikiwakilisha damu ya Kristo na rangi ya bluu hafifu ikiwakilisha maji ya ubatizo. Masomo ya Dominika ya pili ya Kipindi cha Pasaka yanatualika kuihifadhi furaha ya Pasaka kama zawadi ya thamani kubwa na ya kudumu inayotiririka kutoka katika huruma ya Mungu Baba iliyo ya milele. Ndivyo anavyosisitiza Ezra akisema; “Pokeeni furaha ya utukufu wenu, mshukuruni Mungu aliyewaita kwa ufalme wake wa mbinguni, aleluya” (Ezr. 2:36-37). Msisitizo mkuu ni huu, ni katika jumuiya tunakutana na Bwana mfufuka na kupokeza zawadi ya ufufuko, Amani rohoni mwetu.
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 4:32-35). Katika somo hili tunapata simulizi la maisha ya Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliyojengwa na mitume kabla na baada ya Pentekoste. Ni picha halisi ya uzuri wa Kanisa la kwanza, jumuiya ya kwanza ya wakristo jinsi waliovyoishi kwa pamoja na upendo, na umoja wao ulivyojidhihirisha wakiishi kwa furaha kubwa, furaha waliyoipata katika Kristo Mfufuka. Hivyo wakawa na moyo mmoja na roho moja, wakiishi kwa kupendana. Kwa upendo, waliweka mali yao pamoja, wakagawana kadiri ya uhitaji wa kila mmoja, wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu chochote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote katika ushirika. Uchoyo kwao ulikuwa ni mwiko. Ulafi na wizi haukuwa na nafasi. Kupendana kati yao ndiko kulikuwa msingi wa kuhubiri Injili. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu Kristo kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa jamii ya jumuiya ya kikristo, kuishi kwa pamoja na umoja kwa kupendana. Upendo ni utambulisho wetu. Ni mwaliko kwetu tuliobatizwa na kukiri kuwa Yesu ni Bwana na mwokozi wa maisha yetu, kudumisha maisha ya kijumuiya kuishi pamoja tukisaidiana katika kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu katikati yetu, hasa kwa walio wadogo na dhaifu. Tuuvue utu wa kale na tuuvae utu mpya uliojaa wema na upendo wa Yesu Kristo.
Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Yohane (1Yn 5:1-6). Somo hili ni mashauri ya Yohani kwa jumuiya ya Wakristo walioishi miaka ya 60 hivi baada ya Ufufuko wa Kristo. Wakristo hao walikuwa katika madhulumu na mateso makali, na wengi walikuwa wameanza kulegea katika imani yao. Yohane aliwatia moyo akiwaambia kuwa watakuwa watoto wa Mungu wakisadiki kuwa Yesu ni “Kristo”, Mkombozi wao. Na ya kuwa watazishinda nguvu zimpingazo Mungu wakisadiki kuwa Yesu ni kweli Mwana wa Mungu. Hivyo wadumu katika upendo, wakipendana kidugu. Ndivyo tunavyopaswa kuwa na sisi, kuwa na ujasiri wa kuishuhudia Imani yetu bila kuogopa, huku tukiishi kwa kupendana. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn 20:19-31). Sehemu hii ya Injili inatueleza habari za mitume na Yesu kabla ya kupaa kwake mbinguni. Kwa kuwa Yesu alifufuka siku ya kwanza ya Juma, wakristo wa kwanza waliitukuza siku hiyo wakaifanya siku rasmi ya sala na kuadhimisha Ekaristi Takatifu wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Katika hali hii Yesu anawatoke na kusimama katikati yao. Maneno ya kwanza ya Yesu ni; “Amani iwe kwenu” nao wakajaa furaha walipomwona. Naye “akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa.” Ni habari njema ya kuwekwa kwa Sakramenti ya upatanisho, sakramenti ya ondoleo la dhambi. Nasi hatuna budi kuipokea kwa moyo wa shukrani ili tupate amani na furaha ya kweli ndani mwetu.
Roho Mtakatifu aliyewavuvia Yesu baada ya ufufuko wake, ndiye anayeliongoza Kanisa tangu wakati wa mitume, ndiye Kiongozi wetu hata leo. Ni kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kristo Yesu aliyewahakikishia mitume wake kuwa katikati yao mpaka ukamilifu wa Dahari, anaendelea kuwa kati yetu kwa njia ya viongozi wa Kanisa ambao wanatiririka katika mti ule ule na wanatumia mafundisho yale yale ya mitume. Sisi tunakutana na Yesu katika neno lake na katika sakramenti zake hasa ya Ekaristi Takatifu tunapoumega mkate. Kila Dominika tunakutana na Kristo Mfufuka anayekuja kati yetu kama alivyowajia mitume jioni ile ya kwanza alipofufuka. Kristo anakuwepo kila tunapokutana kwa sala, kila tunaposikiliza Neno la Mungu linaposomwa na kuhubiriwa, kila zinapoadhimisha sakramenti zake alizolikabidhi Kanisa hasa Ekaristi Takatifu ambayo Yeye mwenyewe yupo mzima kabisa katika maumbo ya mkate na divai. Tukumbuke daima kuwa ni katika jumuiya, ndipo tunakutana na Yesu. Tomaso baada ya kutoka nje ya jumuiya alikosa bahati ya kumwona Yesu Mfufuka. Lakini aliporudi na kuamua kukaa ndani ya jumuiya alimuona Yesu. Injili inasema wazi kuwa: “Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, “Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye.” Yeye ambaye hakuwaamini wenzake walipomjuza habari za kufufuka kwake Kristo, alikiri kiri kuu na kusema; “Bwana wangu na Mungu wangu!”
Kumbe, kila tunapojitenga na jumuiya ya kikristo, kila tunapokosa kushiriki katika sala za jumuiya na katika maadhimisho ya Sadaka ya Misa Takatifu siku za dominika. Tunakosa nafasi ya kukutana na Kristo Mfufuka, na tunakosa zawadi ambazo Kristo Mfufuka anazikabidhi kwa Jumuiya inayosali pamoja; amani, furaha, msamaha na haki ya kuwa wana wa Mungu. Ni katika jumuiya na ndani ya jumuiya tunakutana na kumwonaYesu Mfufuka na kujazwa furaha na amani ya kweli. Kinyume chake ni kweli, amani na furaha hutokomea tunapomfukuza Kristo mioyoni mwetu kutokana na dhambi hasa pale tunapojitenga na jumuiya zetu. Wito kwa mliojitenga na jumuiya zenu. Rudini katika jumuiya zenu hata kama zina mapungufu ni jumuiya zenu, ni mahali pa kukutana na Yesu mfufuka. Ili amani na furaha itawale mioyoni mwetu yatupasa kuiishi Amri ya mapendo. Kuharakisha kumsaidia kila mmoja anayehitaji msaada wetu. Kuishi katika umoja na mshikamano. Katika siku za mwisho wa maisha yake hapa duniani Yesu alitoa wosia; “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi” (Jn.13:34). Kumbe umoja na mshikamano wa mapendo vitahuisha amani na furaha ya kweli katika Jumuiya ya Kikristo. Tutambue kuwa Jumuiya zetu za Kikristo, hasa jumuiya ndogondogo ni mwendelezo wa Jumuiya ya kwanza ya wakristo baada ya ufufuko wa Yesu Kristo. Tuzidhamini na kuzienzi kwani kila tunapokutana, tunakukutana na Kristo mfufuka. Yeye yuko anatusubiri ili atubariki na kutujaza Neema na baraka zake. Hizi ndizo zawadi ambazo hatupaswi kuzificha bali kuwashirikisha wengine mpaka tutakapozipata katika utimilifu wake huko mbenguni. Tumsifu Yesu Kristo!