Romania:Ushirikiano ni mada ya Mkutano wa Baraza la Utoto wa Kimisionari Ulaya
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kuna watu wapatao hamsini watakaoshiriki katika mkutano ujao wa wawakilishi wa Shirika la Kipapa la Utoto wa Kimissionari Barani Ulaya unaopangwa kuanzia Dominika tarehe 7 hadi Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2024, kwenye Nyumba ya Watawa na Mapadre Wakarmeli wa (Bucharest). Mkutano huo umeandaliwa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa Romania (PMS) kwa ushirikiano na Baraza la Utoto wa Kimisionari wa Ulaya( CEME)”, shirika ambalo tangu mwaka 1973 limezikutanisha pamoja Sekretarieti za Jumuiya ya Kimisionari ya Kipapa nchi za Ulaya katika kuhamasisha, kushiriki na kusaidia shughuli za Kazi za utume wa kimisionari.
Wakati wa mkutano wa awali uliofanyika mnamo mwaka 2022 jijini Geneva, Uswiss, iliteuwa mkutano ujao kufanyika nchini Romania ambapo washiriki, kutoka nchi 23, watashirikisha shughuli maalum wanazofanya katika eneo hilo na kutafuta njia za pamoja. “Ushirikiano” ndiyo mada iliyopendekezwa na Sekretarieti ya Kimataifa ya Shirika la Kipapa la Utoto wa Kimissionari kwa mkutano wa mwaka huu 2024. Watakaohudhuria katika hafla hiyo, miongoni mwa wengine, Sista Roberta Tremarelli, Katibu Mkuu wa Shirika la Kipapa la Utoto wa Kimisionari, Nancy Camilleri, Rais wa CEME na Elke Grün, Katibu wa CEME.
Askofu Mkuu Aurel Percă, wa Jimbo kuu la Bucharest, ataongoza adhimisho la Ekaristi lililopangwa kufanyika tarehe 9 Aprili 2024 kwa kushirikisha watoto wamisionari ambao kwa tukio hilo wametayarisha wakati wa kisanii na ushuhuda wa shughuli zao za kimisionari. Mwishoni mwa kazi hiyo, Alhamisi tarehe 11 Aprili 2024 baadhi ya washiriki wakiandamana na Padre Eugen Blaj, mkurugenzi wa kitaifa wa PMS nchini Romania, watasafiri hadi Transylvania, ambako watakutana na watoto wamisionari wa makabila mbalimbali na madhehebu ya Kikristo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari za Kimisionari (FIDES) lnabainisha kuwa “Matilda Andrici Gabor, kiongozi mkuu wa Utoto wa Kimisionari, anayehamaisha nchini Romania tangu 2019, alibainisha kuwa ““Ilikuwa miaka mitano mikali sana kutoka kwa mtazamo wa kichungaji, ambapo tulijaribu kukuza mwamko wa kimisionari katika maisha ya vijana kwa kuwasaidia kufahamu ujumbe wa kiinjili wa Yesu: kuzaliwa upya kwa maisha ya kiroho. Shukrani kwa uwazi wa watoto, wazazi, mapadre wa parokia na maaskofu, lakini zaidi ya yote kwa msaada wa Roho Mtakatifu, iliwezekana kupanda upendo kwa ajili ya utume mioyoni mwa watoto wa karibu majimbo yote na makanisa ya Romania.”