Tafakari Dominika ya Tano Kipindi cha Pasaka Mwaka B: Yesu Ni Mzabibu wa Kweli!
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Leo tumeingia Dominika ya tano ya Kipindi cha Pasaka, Mwaka B wa Kanisa. Masomo yote yanatualika na kutueleza kwamba, ili tuweze kuzaa matunda mema, ni lazima kila mara tubaki tumeungana na Bwana wetu, kama matawi yalivyoungana na mzabibu. Katika Agano la kale ufunuo wa ufalme wa Mungu umetolewa mara nyingi kwa njia ya mifano. Vivyo hivyo sasa maumbile ya ndani ya Kanisa hujidhihirisha kwetu kwa ishara mbalimbali, zitokanazo na maisha ya wachungaji na wakulima, kama vile na kazi ya kujenga, au na maisha ya familia na arusi. Na ishara hizo zimewahi kutayarishwa katika vitabu vya Manabii. Hivyo Kanisa ni zizi, ambalo mlango wake mmoja tu na wa lazima ndiye Kristo (taz. Yn 10:1-10). Nalo ni pia kundi la kondoo, ambalo Mungu mwenyewe alihubiri tangu zamani ya kwamba atakuwa mchungaji wake (taz. Isa 40:11; Eze 34:11nk). Kondoo wake, ijapokuwa wanachungwa na wanadamu, huongozwa na kulishwa na Kristo mwenyewe aliye Mchungaji mwema na Mkuu wa wachungaji (taz. Yn 10:11; 1Pet 5:4), ambaye aliutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo (taz. Yn 10:11-15). Kanisa ni ardhi iliyolimwa, ni shamba la Mungu (taz. 1Kor 3:9). Katika shamba hilo mzeituni ule wa zamani hukua, ambao shina lake takatifu ni Mababu, na ndani yake upatanisho wa Wayahudi na wa Mataifa umeletwa na utaendelea kuletwa (taz. Rum 11:13-26). Mzeituni huu ulipandwa na Mkulima wa mbinguni kama shamba la mizabibu lililoteuliwa (taz. Mt 21:33-43//; Isa 5:1nk). Kristo ndiye mzabibu wa kweli anayeyajalia matawi, yaani sisi, uhai na uwezo wa kuzaa; nasi, kwa njia ya Kanisa, twakaa ndani yake, na pasipo yeye hatuwezi kufanya neno lolote (taz. Yn 15:1-5). Rej Lumen gentium, 6. Kristo Yesu ndiye mzabibu wa kweli. Maisha yake yote aliyatumia kwa kuwatendea wema wenzake. Ni hamu ya mwanadamu kujipatia ukamilifu na kuishi milele. Ukamilifu huo wa uzima upo katika Yesu Kristo Mfufuka aliye Mzabibu wa kweli. Yesu hakuwa wa kwanza kutumia picha ya mzabibu, ‘Nami nilikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje basi kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu? (Yer 2:21, Isa 5:1-4). Waisrael walijipambanua kama zabibu pori zisizozaa na hivi Mungu aliye Mkulima aliwaharibu na kupanda zabibu nyingine (Isa 5:5-7). Kristo Mzabibu mpya analeta matunda yasiyokuwapo bado yaani haki, uaminifu na upendo. Zabibu hizi zilipandwa siku ya Pasaka Baba alipomfufua Mwana kutoka kwa wafu.
UFAFANUZI: Tazama Mtakatifu Paulo katika somo I (Mdo 9:26-31) anavyoogopwa na wakristo, wanamuona adui sababu alilitesa Kanisa akawa tawi bovu lililokauka, sasa ameongoka na bado haaminiki. Ilibidi Barnaba aingilie kati kumtambulisha kwao ndipo walipompokea kama mwenzao. Je, mimi na wewe tunapokelekaje mbele ya wenzetu? Unaponiona unajisikiaje? Unapata furaha au hapana? Kama uwepo wetu kati ya wenzetu unaleta baraka, amani na faraja heri yetu, sisi ni matawi yenye kuzaa na Baba atatusafisha tuzidi kuzaa. Lakini kama muonekano wetu mbele ya wenzetu ni makwazo na machukizo halafu sisi ni matawi mabovu na hayo Baba huyaondoa kwa wakati wake, ‘ shoka limekwishawekwa penye mashina ya miti, basi kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa na kutupwa katika moto usiozimika’ (Mt 3:10). Binadamu ni kama matawi ya mzabibu, tunahitaji mti wa mzabibu ili tuweze kujishikiza. Mzabibu tuliyojishikilia unaonesha jinsi tunavyojiona, matarajio tuliyonayo na mkondo wa kimafanikio tuliojiweka. Mzabibu unakuja katika sura tofauti; Mwingine unakuja katika sura ya utaifa kama Unazi wa kule Ujerumani, kiitikadi kama Ujamaa au hata kidini. Wengi wetu mali na starehe ndio mashina tuliyojishikilia kwa dunia ya sasa. Pale tunapojishikilia na mizabibu ya uongo inaonesha jinsi tulivyo na tunavyoishi. Wayahudi ambao Yesu anaongea nayo kwenye Injili leo, walifahamu vyema mzabibu ambao walitakiwa kujishikilia. Mara nyingi kwenye Agano la Kale mambo ya kidini na ya kiserikali yalihusishwa na mzabibu. Zab 80:8; Is 5:7; Hos 10:1 ambayo umepandwa na mkono wa Mungu. Zab 80:15; Yer 2:21. Wamakabayo walitengeneza sarafu ambayo mzabibu ulitumika kuonesha Israeli. Kwa hiyo Yesu aliposema yeye ni mzabibu, Wayahudi walianza kufikiri kwamba sasa wanalazimika kuhama kutoka utaifa wa kiyahudi na kuufuata ujumbe wa Kristo.
Somo la Pili linafafanua kwamba ‘naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye naye ndani yake; na katika hili tunajua kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa’. Basi na tuzishike amri zake, tupokee sakramenti na tusali. ‘Kaeni ndani yangu nami ndani yenu, alleluia’, kukaa ndani ya Yesu kunahusisha sadaka na majitoleo. Ukristo ni dini ngumu, ni kujitoa, kujisadaka na wakati mwingine ni kutokueleweka. Ukristo sio simu za mikononi hapana! Tusirahisishe mambo, mbinguni hatuendi kwa ujanjaujanja. Hakuna dini kwenye simu za mikononi. Wengi tumeacha kuja kusali huku tukibadilishana pepo na baraka pasipo hofu, utasikia tuma ujumbe huu kwa watu 10 utaingia mbinguni, au tuma ujumbe huu kwa watu 15 halafu kesho jioni utapata fedha, ukidharau utapata mkosi. Mbingu sio mchezo. Yesu amesulibiwa na kuchomwa mkuki ubavuni kwa ajili yetu halafu wewe eti utume ujumbe kwa watu 10 tena message zenyewe za promosheni tu ya cheka toka Vodafone halafu uingie mbinguni au upate mafanikio katika maisha yako! Hapana, fanya ujanjaujanja mahali pengine lakini sio katika mambo ya Mungu. Ishi ndani ya Yesu na Yesu ndani yako utajipatia ukamilifu wa uzima wako. Tunakaa ndani ya Yesu kwa njia ya Sala, Neno na ibada. Katekisimu inafundisha kwamba sala lazima ibubujike kutoka chemchemi halisi ya Roho Mt anayewezesha neno la Mungu, Liturujia ya Kanisa na fadhila za kimungu. Familia zinaposali zinakuwa mfano mzuri wa mzabibu wa Bwana. Kwamba baba, mama na watoto wanaishi kwa umoja ni neno zuri.! Ni wazi tunafahamu pasi na shaka kuwa Familia imetelekwa juu ya mafiga 3 ya baba, mama na watoto katika Mungu. Kama vile harusi ya Kana ilivyomwalika Yesu na kupata neema ya kuongezewa divai hata familia zetu zinapomwalika katika sala zinapata neema mbalimbali kulingana na mahitaji.
Je, tuliwekeje swali hili? Ni nani mwenye matatizo, ni watoto wa siku hizi au wazazi wa siku hizi au wazaaji wa siku hizi? Ni vijana wa siku hizi? Au ni wazee wa siku hizi? mtoto umleavyo ndivyo akuavyo namba hazidanganyi. Hii ina maana kuwa maisha ya mtu hutegemea aina ya malezi anayopata. Leo suala la malezi ni changamoto pote duniani watoto wengi wamekuwa majuto kwa wazazi na wazazi wamekuwa mizigo kwa watoto wao kwa sababu hakuna uhusiano mzuri wa kimalezi na kutambua majukumu ya wazazi na watoto kutambua wajibu wao kwa wazazi wao kila mmoja ni mmgeni kwa mwingine kwa sababu hawakai pamoja, kama fsmilia Mungu mwema atuhurumie tuwe na familia zinazozaa matunda mema yaani fsmilia inayomwalika Kristo kukaa ndani yao. Kila mmoja hulaumu pande nyingine utasikia watoto wa siku hizi, Je walijizaa, utasikia wazazi wa sikuu hizii mmmmm amri ya nne ya Mungu ipo wapi? Msemo huu una maana kwamba watoto leo wamekuwa changamoto kwa wazazi, ni kama kero hivi, ni shida. Watoto leo tunaongea lugha ambazo wazazi wetu hawazielewi, Kiswahili si Kiswahili, Kiingereza si Kiingereza. Wakibaki nyumbani peke yao halafu wakaja rafiki zao huvuruga kila kitu. Yaani inakuwa paka ametoka hivi panya wanatawala. Hufungua Tv na radio sauti za juu utadhani mtaa mzima wanahitaji hilo. Hawasomi hadi walazimishwe kufanya mazoezi ya shule. Vijana tulio wengi hatupokei maonyo na maelekezo ya wazazi/walezi badala yake tunapokea maelekezo mitandaoni. Hatupishi wakubwa kwenye viti vya mabasi na tunawadharau wakubwa hao. Vijana ‘kaeni ndani yangu nami ndani yenu’ mtazaa zabibu njema na sio zabibu pori. Imenenwa pia, ‘wazazi wa siku hizi bwana!’ Eti wanatofautisha chumba chao na cha watoto kwa mapazia tu, kwamba wanawaogopa watoto wao, wanawabembeleza tu na kuwapa chochote wanachokitaka. Hawawaonyi juu ya mavazi yao wala juu ya tabia na mwenendo wao. Oh, wazazi wa siku hizi jamani, hawana umoja na kila mmoja anahusiana na watoto kivyake. Mtoto ni malezi, ili wali uupate sharti upike mchele, na mchele uupete, mpunga na chuya vitoke… ndio ngozi iwahi ingali maji, malezi ni jambo kubwa, ingawa elimu ni bora hekima ni bora zaidi, tujipe moyo, tukazane, naye Mungu atusaidie ili neno hili litukae, ‘kaeni ndani yangu nami ndani yenu, allelluia!!’ KRISTO TUMAIN LETU.