Tafakari Dominika ya Tano ya Pasaka Mwaka B: Muungano na Kristo Yesu
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu dominika ya tano ya Kipindi cha Pasaka mwaka B. Neno la Mungu dominika hii linatualika tuujenge muunganiko na Mungu wetu aliyemtakatifu katika Kristo Yesu, Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, ili tuweze kuzaa matunda mema na kustahilishwa kuingia katika ufalme wa mbinguni. Ili tuweze kufanikiwa katika kutenda matendo mema kwa kuishi kwa upendo, sharti ni moja, kuunganika na Kristo aliye kama mzabibu nasi tukiwa kama matawi. Haya ndiyo maajabu anayotutendea Mungu Baba kwa njia ya Yesu Kristo mfufuka. Ndiyo maana maadhimisho ya kiliturujia katika dominika 5 yaanza kwa wimbo wenye maneno haya; “Mwimbieni Bwana wimbo mpya, kwa maana ametenda mambo ya ajabu; machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake, aleluya” (Zab 98:1-2). Naye maana Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea wanawe akisali hivi; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristu tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele.” Somo la kwanza ni la Matendo ya Mitume (Mdo 9:26–31). Somo hili linasimulia maisha ya Paulo mara baada ya kuongoka kwake. Sauli ambaye alikuwa mtesi wa Kanisa, alipoongoka na kuanza kuhubiri neno la Mungu, haikuwa rahisi kwa mitume kumwamini. Ushuhuda wa Barnaba wa kuongoka kwake ndio uliowafanya mitume waamini kuwa kweli Sauli ameongoka nao wakampokea. Barnaba ni mfano wa kuigwa. Kama Barnaba nasi tunapaswa kushuhudia kuongoka kwa ndugu zetu kuwa sasa ni watu wapya. Paulo pia ni ishara wazi ya wongofu katika Kristo. Neema ya Mungu ni kubwa zaidi ya dhambi. Hakuna dhambi kubwa inayoweza kushida neema na huruma ya Mungu kwa mwongofu. Mungu anamsamehe kila anayetubu na kukiri makosa yake na anaweza kumchagua mtu yeyote awe chombo cha kueneza habari njema ya wokovu hata kama mwanzoni alikuwa ni mdhambi. Hii ni habari njema, hatuna sababu ya kukata tamaa kwa sababu ya dhambi zetu bali tufungue mioyo yetu, tumruhusu Kristo mfufuka aingie ili neema yake ifanye kazi ndani mwetu.
Mtume Paulo baada ya kupokelewa na mitume alihubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina lake Yesu, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao waliposhindwa kujibizana naye wakajaribu kumwua naye akakimbilia Kaisaria, akaenda mpaka Tarso akimhubiri Kristo. Paulo aliyatoa maisha yake yote, akawa tayari kuvumilia taabu zote (1Kor 4:9–13; 2Kor 6:4–10; 11:23–27) ili kumtangaza Kristo na kwake hakuna chochote kilichoweza kumtenganisha na upendo wa Kristo (Rum 8:35–39). Yeye aliipokea na kuitegemea neema ya Mungu ndiyo maana anasema; “Ni kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo, na neema ya Mungu haikuwa bure” (1Kor 15:10; 2Kor 3:5; 2Kor 4:7). Tumwombe Mungu kama alivyomteua mtume Paulo ili nasi tuwe ni vyombo viteule vya kueneza Habari Njema. Atujalie neema ya kueneza huruma na upendo wake katika familia, jumuiya, Kanisa na jamii kwa ujumla. Paulo alipodhulumiwa kwa sababu ya Injili, hakukata tamaa na kurudi nyuma bali alisonga mbele akiitumainia neema ya Mungu. Ni katika mazingira hayo “Kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kichwa cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu”. Nasi tuwe na ujasiri na tusione aibu wala kukata tamaa katika kuishuhudia Imani yetu kwa Kristo mfufuka kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu kama zaburi ya wimbo wa katikati inavyosema; “Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu, katika kusanyiko kubwa. Nitaziondoa nadhiri zangu mbele yao wamchao. Wapole watakula na kushiba, wamtafutao Bwana watamsifu; Mioyo yenu na iishi milele. Miisho yote ya dunia itakumbuka, na watu watamrejea Bwana; Jamaa zote za mataifa watamsujudia. Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu, humwinamia wote washukao mavumbini. Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake, wazao wake watamtumikia. Zitasimuliwa habari za Bwana, kwa kizazi kitakachokuja. Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake, ya kwamba ndiye aliyefanya (Zab. 22:25b-27, 29-31).
Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Yohane kwa watu wote (1Yn 3:18–24). Katika somo hili Yohane anasisitiza mapendo ya kweli yaonekane zaidi katika kutenda mema; kwani ni katika kutenda mema tunapata furaha na amani ya kweli katika maisha yetu. Tena tukitaka kuishi katika umoja na Mungu, yatupasa kumwamini Kristo na kumpenda jirani. Lakini mapendo yetu kwa jirani, yasiwe na unafiki wala hila, wala masharti. Yohane anasisitiza hivi; “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake…Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa. Matunda ya kuzishika amri za Mungu na kuishi kwa upendo ni kwamba; “lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake.” Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yoh 15:1–8). Katika sehemu hii ya Injili, Yohane kwa kutumia mfano wa mzabibu na matawi, anatueleza kwa kina kabisa uhusiano wetu na Yesu Kristo, Bwana na mwokozi wa maisha yetu. Mfano huu wa mzabibu na matawi yake unatuonyesha umoja uliopo kati ya Yesu na sisi wakristo-wafuasi wake. Kwa kujiunga na Yesu tu, tutaweza kuzaa matunda ya mapendo na kutenda matendo mema. Kwa nguvu yetu wenyewe hatuwezi kitu.
Yesu mwenyewe anaweka wazi ukweli huu akisema; “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lolote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni lolote mtakalo, nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wangu.” Basi tujitahidi kukaa ndani ya Kristo ili tuzae matunda mema ya wokovu. Tuweni vyombo vya kuleta amani na upendo kati yetu. Huku ndiko kuwa katika maisha mapya ambayo mama Kanisa anatuombea katika sala baada ya Komunio akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe na sisi taifa lako. Na kama ulivyotujalia mafumbo haya ya mbinguni, utufikishe kwenye uzima, utuondoe katika maisha ya zamani na kutuweka katika maisha mapya.” Ni katika kufanya hivyo tutastahilishwa kuurithi uzima wa milele anaotuombea mama Kanisa katika sala ya mwanzo akisali hivi; “Ee Mungu, umetuletea ukombozi na kutufanya watoto wako. Tunakuomba utusikilize kwa wema sisi wanao, ili katika kumwamini Kristo tupate uhuru wa kweli na urithi wa milele.” Tumsifu Yesu Kristo!